Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limetambua mchango wa Mkoa wa Simiyu katika Utekelezaji wa Sera ya Viwanda na kutoa Tuzo ya kikombe na Cheti.
Tuzo hizo zilikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji lililofanyika Mjini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe Anthony Mtaka amesema Tuzo hizi ni hamasa kwa Viongozi na wananchi wa Simiyu kuongeza jitihada zaidi katika Utekelezaji wa Sera ya Viwanda kuelekea kwenye Uchumi wa Kati.
Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “WILAYA MOJA BIDHAA MOJA” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha kutengeneza Chaki kilichopo wilayani Maswa na Kiwanda cha kusindika Maziwa wilayani Meatu, ambapo upembuzi yakinifu unaendelea kwa ajili ya upanuzi wa viwanda hivi ili kuongeza uzalishaji.
Aidha, upembuzi yakinifu utafanyika katika Halmashauri nyingine kwa ajili ya kuanzisha viwanda mbalimbali kikiwemo kiwanda cha sabuni za maji, za unga na mche wilayani Itilima, Kiwanda cha kutengeneza Tomato Sauce na Chill Sauce Wilaya ya Busega na kiwanda cha kusaga nafaka na kupaki unga Bariadi Mjini.
Vingine ni kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kitakacojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na Kiwanda cha kutengeneza vifungashio kitakachojengwa Wilayani Maswa.
Pamoja na viwanda hivyo, Serikali imekusudia kujenga Kiwanda cha bidhaa za Hospitali zitokanazo na pamba, ambacho kitasaidia Taifa kuokoa fedha zilizokuwa zikitumika kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi.
0 comments:
Post a Comment