Picha
juu na chini ni Ofisa wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ngusekela Karen Nyerere
akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza
Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN-2017) unaofanyika kwenye
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) mjini
Arusha.
Vijana kutoka mataifa mbalimbali
waliokusanyika katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la
Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN), mjini Arusha wametakiwa kuchambua
masuala yaliyopo mbele yao kwa makini ili kutoa jawabu kwa matatizo ya
dunia yanayohitaji ushiriki wao.
Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa
serikali katika mkutano huo Ngusekela Karen Nyerere, Ofisa
anayeshughulikia dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Aliwataka vijana wanaoshiriki TIMUN
kuhakikisha wanaangalia kwa makini mambo yanayogusa nchi zao na
kuyatafutia ufumbuzi kwa kuwa ndio njia pekee ya kutekeleza malengo
endelevu ya dunia ambayo yanahitaji ushirikiano wa ndani na wa
kimataifa.
TIMUN ambayo kirefu chake ni Tanzania
International Model United Nations hufanyika kila mwaka na ujumbe
mbalimbali na mwaka huu ujumbe wa TIMUN ni: “kuwawezesha vijana katika
diplomasia na uongozi”
TIMUN huandaliwa na Shirikisho la vijana
wa Umoja wa Mataifa (YUNA) taasisi ya vijana isiyotengeneza faida
inayotangaza shughuli za Umoja wa Mataifa na kushirikisha vijana katika
utekelezaji wa shughuli hizo.
Aidha aliwashukuru waandazi wa mkutano
huo kubwa unaofanana na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (General
Assembly) wenye lengo la kukutanisha vijana kujadili mustakabali wa
malengo ya dunia.
Alisema vijana wana nafasi muhimu katika
utekelezaji wa malengo hayo ya maendeleo endelevu jukumu ambalo dunia
imejipa kwa miaka 15 hadi mwaka 2030.
Pamoja na kuwashukuru Taasisi ya Sayansi
na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) kwa kukubali kuwa
mwenyeji wa kambi hiyo, hali iliyoonesha kwamba wanajali vijana,
mwakilishi huyo wa serikali alisema kwamba Tanzania ipo tayari kusukuma
mbele ajenda ya ushirikishaji vijana katika maendeleo endelevu kwa kuwa
inaamini juu ya hilo.
“Wakati serikali inafanyakazi kwa karibu
na taasisi nyingine kuhakikisha kwamba malengo ya maendeleo
yanatekelezeka, baraza la vijana ambalo litakutana litakuwa na kazi
kubwa ya kutengeneza sauti ya pamoja namna ya kukabiliana na changamoto
zilizopo”
Alisema kwamba malengo ya dunia ambayo
yapo 17 yanagusa kila sehemu ya maisha na hivyo ni vyema kama vijana
watatoka na majibu ya maswali yanaoumiza vichwa kuhusu malengo hayo hasa
mazingira na dunia endelevu.
Aliwataka vijana kutumia nafasi yao
vyema katika jukwaa hilo kwani maisha ya watu bilioni 7 duniani
wanategemea namna ambavyo wanajengwa na vijana, wenye mchango muhimu wa
kulinda mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa
Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akifungua rasmi
Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa
(TIMUN-2017), unaofanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya
Nelson Mandela (NM-AIST) mjini Arusha
Awali Mratibu Mkazi wa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini,
Alvaro Rodriguez alisema kwamba zaidi ya vijana elfu 20 nchini Tanzania
wamefunzwa malengo endelevu ya dunia, toka ulipofanyika uzinduzi Juni,
2016.
Akizungumza katika hafla ya kambi ya
mwaka huu ya Tanzania International Model United Nations (TIMUN),
inayofanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela,
Arusha (NM-AIST), Bw. Rodriguez alielezea kufurahishwa na idadi hiyo ya
vijana waliohamasishwa na kusema kwamba malengo ya maendeleo endelevu
2030 yanahitaji kila mmoja kushiriki.
Aidha alielezea umuhimu wa ushiriki wa
vijana katika masuala ya maendeleo kutokana na uwingi wao hapa nchini.
Asilimia 67 ya watu nchini ni vijana.
Mkutano ukiendelea katika ukumbi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini Arusha.
Bw. Rodriguez alishukuru machampioni kwa
kuwezesha vijana wenzao kutambua malengo endelevu ya dunia na kuwataka
kuendelea kufanya vizuri zaidi katika kuwashawishi vijana wenzao kuelewa
na kushiriki katika malengo hayo.
“Nataka kuwatafadhalisha kwamba huu ni
mwanzo tu, kuna mengi ya kufanya. Kama Umoja wa Mataifa, tunawataka wote
mshiriki, si tu katika kuelimisha kuhusu malengo haya ya dunia, lakini
pia katika kuangalia mwenendo wa maendeleo hayo katika jamii na namna
yanavyotekelezwa. Tukio kama hili la TIMUN linasaidia kuongeza uwezo wa
kufikia malengo ya dunia,” alisema Bw. Rodriguez.
Vijana 50 wa kwanza machampioni
walifunzwa mwaka jana katika TIMUN 2016. Kwa sasa kuna vijana
machampioni 500 nchini Tanzania ambao wamepeleka ujumbe kwa vijana
wenzao 20,000.
Mratibu wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la
Umoja wa Mataifa (TIMUN 2017), Tajiel Urioh akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mkutano huo unaoendelea jijini Arusha.
Ujumbe ambao umekuwa ukisambazwa na
machampioni kwa wenzao umeelezwa kulenga kuchochea hamasa ya kuelewa
malengo kwa ajili ya maendeleo.
“Kama watu hawatajua malengo ya
maendeleo endelevu, hawataweza kufanya malengo hayo kuwa ya kweli,”
aliusema ujumbe huo Gloria Nassary, ambaye ni mmoja kati ya vijana 50
waliopewa mafunzo ya kwanza ya kuwa machampioni wa malengo ya dunia.
Naye Tajiel Urioh ambaye ni Mratibu wa
Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa
(TIMUN 2017), pamoja na kusisitiza amani kama sehemu muhimu ya kusukuma
mbele utekelezaji wa malengo 17 ya maendeleo endelevu aliwahimiza
vijana kutokata tamaa katika kuhimiza utekelezaji wa malengo hayo.
Ofisa wa Mawasiliano NUNV anayeshughulikia tovuti na mitandao ya
kijamii katika ofisi ya Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa
Mataifa nchini, Edgar Kiliba akiendesha kipindi cha maswali na majibu
wakati wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja
wa Mataifa (TIMUN 2017) unaoendelea jijini Arusha kwenye ukumbi wa
Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini
Arusha.
Alisema bila amani kuanzia katika ngazi
ya familia, uwezekano wa kutekeleza malengo hayo unakuwa mgumu kwa kuwa
kuna uhusiano mkubwa kati ya amani na utekelezaji wake.
Alisema amani ni kionjo muhimu cha
maendeleo kinapokosekana hata jukumu la vijana kulinda mazingira kwa
ajili ya maendeleo endelevu halitawezekana.
Alisisitiza kulinda mazingira kwa ajili
ya maendeleo na kufikiwa kwa malengo ya Umoja ya Mataifa ambayo ni
malengo ya dunia katika kuimarisha ustawi wa jamii na kuinua uchumi .
Urioh katika mazungumzo yake alisema
suala la uchafuzi wa mazingira ni suala gumu na mtambuka na kwamba
mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na kuvurugwa kwa tabaka la
ozoni halihusu Ulaya pekee, ambao wanachafua bali kila mmoja duniani;
akiongeza kuwa mwishoni mwa siku wanaoathirika ni zaidi nchi
zinazondelea akitolea mfano nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
Championi wa Malengo ya dunia (Global Goals) nchini, Rio Paul akitoa
maoni katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la
Umoja wa Mataifa (TIMUN-2017) unaoendelea jijini Arusha.
Alisema suala la kukabilina na
mabadiliko ya tabia nchi si kutulia bali kuwajibika kutekeleza wajibu
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna uharibifu wa mazingira
unaofanyika katika taifa la Tanzania.
Alisema vijana wanaweza kufanya zaidi ya
yale ambayo kwa sasa wameyafanya katika kutekeleza malengo ya maendeleo
endelevu kwa kuhakikisha kwamba wana elimu ya kutosha kuhusu malengo
hayo na kushirikiana kuyatekeleza kwa kuangalia changamoto mbalimbali
ambazo wanazipatia majibu.
Alisema lengo la malengo hayo ni
kusaidia jamii vivyo hivyo vijana nao wanatakiwa kujitoa mhanga
kuhakikisha kwamba jamii inaendelea kustawi na kuendelea kwa manufaa ya
kizazi kijacho.
Mmoja wa washiriki kutoka nchini Uingereza akiuliza swali kwa Mratibu
Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (hayupo pichani) wakati wa
ufunguzi wa mkutano huo.
Aliwataka vijana kutafuta majawabu ya
mambo yanayoikabili dunia kwa namna ya busara na kitaalamu zaidi huku
wakizingatia diplomasia.
Septemba 2015, wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa walikubaliana juu ya malengo mapya ya dunia, malengo ya maendeleo endelevu.
Malengo hayo yanatarajiwa kufanyiwa kazi
katika kipindi cha miaka 15 ijayo na kuleta mabadiliko makubwa katika
jamii, uchumi na mazingira kwa namna ya kuwa endelevu.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa
Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiteta jambo na
Mwenyekiti wa Shirikisho la vijana wa Umoja wa Mataifa (YUNA) nchini,
Jacqueline Kamwamu wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa
Baraza Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN-2017) unaoendelea
mjini Arusha. Kushoto ni Mratibu wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza
Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN 2017), Tajiel Urioh.
Wakati akiwa Arusha, Mratibu pia
alifuatilia matokeo ya mafunzo yaliyofanyika Novemba mwaka jana katika
chuo kikuu cha Tumaini Makumira yaliyofanywa kwa pamoja kati ya Umoja wa
mataifa na Jumuiya ya Ulaya.
Katika mafunzo hayo machampioni 80
walifunzwa wakiwemo wanachuo 30 kutoka Taasisi ya Uhasibu ya Arusha
(Institute of Accountancy Arusha -IAA).
Mkutano huo umefadhiliwa Umoja wa
Mataifa (UN), Serikali, Covenant Bank, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha
(NM-AIST) pamoja PIU.
Katibu wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ngusekela Karen Nyerere akijibu baadhi
ya maswali kutoka kwa washiriki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa
mkutano huo.Pichani juu na chini ni sehemu ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wanaohudhuria Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN-2017) unaoendelea mjini Arusha.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) akisalimiana na Kaimu Makamu Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) anayeshughulikia Fedha, Mipango na Utawala, Dr. Musa Chacha (kushoto) baada ya kuwasili ofisini kwa Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Karoli Njau (katikati) jijini Arusha.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) Prof. Karoli Njau akiwa kwenye mazungumzo ofisini kwake na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kulia) aliyeambatana na Mkuu wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa nchini, Hoyce Temu (wa kwanza kulia), Ofisa wa dawati la Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ngusekela Karen Nyerere, Ofisa wa Mawasiliano na Ushirikiano NUNV kutoka Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Didi Nafisa pamoja na Ofisa wa Mawasiliano NUNV anayeshughulikia tovuti na mitandao ya kijamii katika ofisi ya Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Edgar Kiliba.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akikabidhi Makamu Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) Prof. Karoli Njau kitabu chenye taarifa na ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN-2017) unaoendelea mjini humo.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akiwa na mwenyeji wake Makamu Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Arusha (NM-AIST) Prof. Karoli Njau wakieleka kwenye eneo maalum la kupiga picha kwenye taasisi hiyo.
Meza kuu kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Baraza Kivuli la Vijana la Umoja wa Mataifa (TIMUN-2017) katika picha ya pamoja.
Meza kuu katika picha ya pamoja na waandaaji wa TIMUN 2017.
Picha ya pamoja na washiriki wa TIMUN 2017 kutoka nje ya Tanzania.
Picha ya pamoja na washiriki wa kambi ya TIMUN 2017 inaoendelea jijini Arusha.
Mkuu wa Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa nchini, Hoyce Temu (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na washiriki wa TIMUN 2017 akiwemo Mshiriki wa taji la Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu (katikati).
0 comments:
Post a Comment