
Viongozi
na wadau mbalimbali wa uwekezaji Mkoani Simiyu wakifuatilia maandiko ya miradi yauanzishwaji
wa viwanda ikiwasilishwa katika kikao cha wadau wa uwekezaji kilichofanyika
Kata ya Lamadi Wilayani Busega
Mkurugenzi
wa Benki ya Azania Ndg.Charles Jackson Itembe akizungumza na waandishi wa
Habari (hawapo pichani) mara baada ya kikao cha wadau wa uwekezaji Mkoani
Simiyu kilichofanyika Kata ya Lamadi wilayani Busega
Kaimu
Meneja wa Mipango na Uwekezaji wa NSSF
Bibi. Radhia Tambwe (wa pili kushoto) katika akizungumza na waandishi wa
Habari mara baada ya kikao cha wadau wa uwekezaji Mkoani Simiyu kilichofanyika
Kata ya Lamadi wilayani Busega
Na Stella Kalinga, Simiyu
Bodi ya
Wadhamini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF imeridhia kutoa mkopo wa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya upanuzi
wa kiwanda cha chaki kilichopo wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.
Kauli hiyo
imetolewa na Kaimu Meneja wa Mipango na Uwekezaji wa NSSF Bibi. Radhia Tambwe katika mahojiano maalum
na waandishi wa Habari mara baada ya kikao cha wadau wa uwekezaji Mkoani Simiyu
kilichofanyika Kata ya Lamadi wilayani Busega ambacho kimewahusisha wadau
mbalimbali wa uwekezaji mkoani humo.
Bibi.Radhia amesema Bodi imefanya uamuzi huo baada
ya kupitia maombi ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na kuona kuwa mradi wa
kiwanda cha chaki una tija kwa kuwa umewashirikisha vijana hivyo kiwanda
kitakapopanuliwa kitaongeza wigo wa ajira kwa vijana, pato la wilaya na kuokoa
fedha za kigeni zinazotumika kuagiza chaki nje ya nchi.
Aidha, amepongeza utekelezaji wa Kauli Mbiu ya “Wilaya
Moja Bidhaa Moja” mkoani Simiyu katika Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda ambapo
amesema kupitia viwanda vitakavyoanzishwa katika kila wilaya chini ya Kauli Mbiu
hii mkoa utatengeneza ajira kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa.
Bi. Radhia pia ametoa wito kwa wadau wengine kuunga
mkono miradi ya ujenzi wa Uchumi wa Viwanda Mkoani Simiyu kwa kuwa ni miradi
yenye tija kwa kuzingatia kuwa malighafi
zinazotumika zinapatikana hapa nchini na soko lake kubwa liko hapa nchini.
“Watanzania tubadilike tusikubali kila mara kugeuzwa
supermarket, tuzalishe bidhaa zetu na kutumia bidhaa zetu wenyewe tujivunie
tulivyonavyo ili tuweze kuendeleza nchi yetu na hatimaye Tanzania na sisi tuwe
nchi yenye uchumi wa kati” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Benki ya Azania Ndg.Charles
Jackson Itembe amesema benki hiyo iko tayari na inaunga mkono uwekezaji katika
sekta ya viwanda unaofanywa na Halmashauri za Mkoa wa Simiyu chini ya Kauli
mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja” kwa kutoa uwezeshaji kifedha katika
miradi iliyoaanishwa na Halmashauri husika kupitia mikopo.
Kwa upande wake Mtaalam Mbobezi wa Viwanda, Ndg. Ndaki
Munyeti amesema Mkoa wa Simiyu umejipanga katika kuwashirikisha Wataalam
mbalimbali katika kuchagua teknolojia itakayotumika katika viwanda vilivyopo na
vitakavyoanzishwa ambayo ndiyo hatua muhimu katika ujenzi wa viwanda inayoweza
kusaidia kupata bidhaa bora na kufanya viwanda vikawa endelevu.
Awali akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha wadau
wa uwekezaji wa Mkoa wa Simiyu Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka amesema pamoja
na NSSF na Benki ya Azania kukubali kuunga mkono juhudi za Ujenzi wa Uchumi wa
Viwanda Mkoani Simiyu amesema Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
wameahidi kutoa fedha za upembuzi yakinifu kwa mradi utakaotekelezwa katika kila
wilaya.(Wilaya Moja Bidhaa Moja)
Mtaka amewataka viongozi kila mmoja awajibike ipasavyo
katika eneo lake kwa kuwa wale walioteuliwa waliaminiwa na Mhe.Rais na
waliochaguliwa waliaminiwa na wananchi hivyo watimize wajibu wao kuhakikisha
viwanda vinasimama na kero za wananchi zinatatuliwa.
“Viongozi wenzangu wa kuteuliwa tunapaswa kuwajibika,
Mhe.Rais aliacha watu wengi akatuamini akatuteua sisi, Waheshimiwa madiwani
wananchi waliwaamini kuwachagua, ni lazima tuioneshe dunia kuwa inawezekana;
natamani mwaka 2020 tutengeneze kura siyo mikutano ya hadhara, kila atakapo
pita Mhe.Rais kuwe na kitu ambacho wananchi wanajivunia kupitia kazi zetu sisi”
alisema.
Kikao cha wadau wa uwekezaji kiliwahusha wajumbe wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Watalaam wa Sekretarieti ya Mkoa, Wakuu wa
Wilaya,Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Halmashauri,Wakurugenzi wa
Halmashauri,Wajumbe wa Kamati za Fedha za Halmashauri, Maafisa Mipango, Wachumi,
Wataalam kutoka Benki ya Azania, NSSF na Watalaam wa Viwanda na Masoko.
Katika kikao hicho maandiko ya miradi ya uanzishwaji
viwanda kutoka katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu yaliwasilishwa kwa
wadau hao ambayo ni upanuzi wa kiwanda cha chaki na kiwanda cha kutengeneza
vifungashio vya karatasi (Maswa), upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa Meatu, kiwanda
cha kutengeneza sabuni za maji, mche na unga Itilima, kiwanda cha kutengeneza
tomato sauce na chili sauce (Busega) kiwanda cha kusaga nafaka na kufungasha unga pamoja na unga lishe
(Bariadi Mjini) na kiwanda cha kutengeneza bidhaa za Ngozi (Halmashauri ya
Wilaya Bariadi) lengo likiwa ni wadau wa Taasisi za fedha na watalaam kwa
pamoja kupitia maandiko hayo kujiandaa na utekelezaji.
Upanuzi wa Kiwanda cha Chaki ni agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli alilolitoa kwa
Uongozi wa Wilaya ya Maswa baada ya kutembelea kiwanda hicho wakati wa ziara
yake mwezi Januari wilayani Maswa Mkoani Simiyu, ambapo aliagiza uongozi huo
kukopa fedha kwa ajili kupanua kiwanda hicho ili kuongeza uzalishaji.
0 comments:
Post a Comment