METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, May 16, 2017

Muhongo: Utafiti mafuta kutofanywa kisiasa


WIZARA ya Nishati na Madini imesisitiza kuwa itaendelea kutumia watalaamu kupata ushauri wa maeneo yanayohitaji kufanyiwa utafiti wa mafuta na gesi na haitaliacha suala hilo liingiliwe kisiasa.

Msimamo huo ulitolewa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (pichani) wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalum, Susan Lyimo (Chadema). Lyimo alitaka kujua ni kwanini serikali haimtumii mzee maarufu katika mji wa Mlimba anayedaiwa kuwa na taarifa kamili kuhusu uwepo wa mafuta kwenye bwawa lililopo mjini hapo ili lifanyiwe utafiti.

Akijibu maswali hayo, Profesa Muhongo alisema serikali haiwezi kwenda kwa mzee yeyote kuuliza taarifa za utafiti wa mafuta na gesi kwa kuwa suala hilo ni la kitaaluma zaidi na utafiti wake hufanyika baada ya wataalam kuwa na uhakika wa uwezekano wa kupatikana kwa nishati hizo.

Alisema katika utafutaji wa mafuta duniani, wakati mwingine utafiti huonesha kuwepo au ukosefu wa nishati hiyo na kwa sasa Tanzania ina mpango wa kubadilisha mbinu ya utafutaji wa mafuta hayo.

 “Naomba tu nisisitize hili ni suala la kitaaluma na si la kisiasa,” alisema Profesa Muhongo.

Katika swali la msingi, mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema) alitaka kujua ni kwanini serikali inafanya utafiti wa mafuta na gesi asilia kimya kimya katika jimbo la Mlimba bila kutoa taarifa rasmi kwa wananchi na inatoa kauli gani kuhusu utafutaji huo wa mafuta katika mji huo. Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Kilosa-Kilombero unafanywa na kampuni ya Swala Energy na ulianza tangu Februari mwaka 2012.

Alisema kutokana na utafiti huo, kampuni hiyo ilibaini uwezekano wa kuwapo kwa mafuta na gesi katika eneo hilo. “Februari mwaka huu serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ilianza kutoa elimu kuhusu utafiti huo na fursa zitakazopatikana kwa wananchi wa Mlimba hasa maeneo yanayozunguka mradi huo,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com