Na Mathias Canal
Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango ameiongoza kamati hiyo kufanya msako wa matabibu wanaofanya huduma za afya pasina kuwa na kibali kutoka serikalini.
Kamati hiyo imemkamata Selemani Martin aliyekuwa Akiendesha huduma za matibabu bila kibali nyumbani kwake, nyumba ambayo ipo katika eneo la shamba lililopo mbali na makazi ya watu.
Mtuhumiwa huyo amekamatwa katika msako huo maalumu uliofanywa na kamati ya ulinzi na usalama nyumbani katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Nachingwea hususani katika Kijiji cha Stesheni kilichopo Kata ya Stesheni, Wilayani humo.
Akielezea Huduma alizokuwa zinatolewa na mtuhumiwa huyo, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Rukia Muwango alisema kuwa ni pamoja na upasuaji mkubwa ambapo vifaa tiba vilikutwa na damu nyingi.
Sambamba na vifaa tiba hivyo pia alikutwa akiwa na mgonjwa mmoja aliyekuwa amefanyia upasuaji ambapo kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nachingwea ilimkimbiza hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka ili kunusuru maisha yake.
Katika msako huo pia Kamati imezikamata pia dawa mbalimbali na vifaa tiba kama visu, mikasi, na vyombo vya kienyeji vinavyotumika kama vifaa tiba kwa ajili ya kuwatibu watu.
Aidha Kijana mmoja na binti mmoja wanaosemekana ni ndugu zake na mtuhumiwa huyo walikuwa wakimsaidia shughuli hizo ili hali hawana elimu wala mafunzo rasmi ya kitabibu.
Katika matibabu hayo mtuhumiwa huyo hufanya Upasuaji wa Henia ambapo kwa kila mgonjwa hutozwa Shilingi 220,000.
Martin ambaye anasadikika kuwa na wateja wengi kutoka Wilaya ya Masasi na wilaya zingine za karibu anashikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano na hatua zaidi za kisheria kutokana na makosa yanayomkabili.
0 comments:
Post a Comment