WAKATI
Sheria ya Makosa ya Mtandao inaanza kutumika leo, Serikali
imewahakikishia wananchi kuwa sheria hiyo haina lengo la kuwaogopesha
wala kuwanyima uhuru wa kuwasiliana, bali itawalinda dhidi ya wahalifu
wa mitandao.
Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa alisema jana
Dar es Salaam kuwa serikali haiwezi kuingilia uhuru wa watu wa
kuwasiliana, bali itafanya hivyo tu kama kuna sababu ya mambo ya usalama
wa taifa.
“Serikali
baada ya kujiridhisha kuwa maandalizi yote muhimu ikiwemo elimu kwa
umma na kujenga uelewa kwa watekelezaji wa sheria hizi yamefanyika,
sasa, sheria hizi zitaanza kutumika rasmi kesho (leo) Septemba mosi.
“Kwa
hivyo, natoa rai na wito kwa wananchi wote kuwa tuzingatie matumizi
salama na sahihi ya huduma za mawasiliano na mtandao kwa manufaa ya kila
mmoja na kwa maendeleo ya Taifa letu.
Mitandao
ikitumiwa vyema ina faida kubwa sana katika jamii yetu,” alisema Profesa
Mbarawa. Sheria ambazo zinaanza kutumika leo ni Sheria ya Makosa ya
Mtandao ya 2015 na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, ambazo
zilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la Agosti 14, mwaka huu.
Profesa
Mbarawa alisema Tanzania siyo nchi ya kwanza kutunga sheria hizo.
Alisema kuna nchi mbalimbali duniani, ambazo zimetunga sheria kama hizi
na alitoa mfano wa Uingereza, India, Malaysia, Uganda, Korea Kusini,
Singapore, Mauritius, Marekani na nyingi nyinginezo.
Alikiri
kuwa sheria hizi zimepokelewa kwa hisia tofauti kutokana na uelewa mdogo
kwa wengi wetu kuhusu sheria hizi. Vilevile, ni ukweli usiopingika kuwa
kumekuwa na tafsiri hasi kwa baadhi ya wananchi juu ya maudhui ya
sheria hizi na kuzifanya zitafsiriwe kama kandamizi zaidi, kitu ambacho
ni tofauti na dhana na maudhi ya sheria hizi.
Alisema
kwa kutambua hilo, wizara yake mara baada ya kupitishwa kwa sheria hizo,
ilianza kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari na kuwa na
mikutano na makundi mbalimbali ya watekelezaji wa sheria hizo ili
kuwajengea uelewa, ikiwemo Jeshi la Polisi, Waendesha Mashtaka,
Wachunguzi, Wapelelezi, Mahakimu na Majaji.
Alisema
ili kuhakikisha kuwa usimamizi na utekelezaji wa sheria hizi unakwenda
vizuri, Wizara itaendelea kuwajengea uelewa wadau mbalimbali.
Alisisitiza kuwa sheria hizo ni muhimu na zina manufaa makubwa kwenye
jamii haswa katika nyakati hizi ambapo matukio ya uhalifu wa mtandao
yamekuwa yakiongezeka na kukosekana kwa sheria hizi kumefanya wananchi
kutokuwa na mahala pa kukimbilia pale wanapokumbana na uhalifu kupitia
mitandaoni.
0 comments:
Post a Comment