METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 23, 2017

KWA CCM NI CHUKI NA VISASI… LAKINI WAPINZANI WAKITIMUANA “WANAFUKUZA WAASI, WASALITI!”



Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
JUMAMOSI ya Machi 11, 2017 Chama cha Mapinduzi (CCM) ‘kiliondoa woga’ na kufanya jambo ambalo halikutarajiwa na wengi nchini baada ya kuwatimua baadhi ya wanachama na kuwavua uongozi wengini huku baadhi yao wakisimamishwa na wengine wakionywa, MaendeleoVijijini inaripoti.
Waliofukuzwa uanachama ni pamoja na mwanachama mkongwe na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Sophia Simba ambaye amepoteza rasmi nafasi yake ya Ubunge wa Viti Maalum na Uenyekiti wa UWT kwani nafasi hizo zinahitaji mtu ambaye ni mwanachama wa chama cha siasa.

Wenyeviti wa mikoa waliofukuzwa ni Ramadhan Rashid Madabida (Dar es Salaam), Christopher Sanya (Mara), Erasto Izengo Kwirasa (Shinyanga), na Jesca Msambatavangu (Iringa).
Wenyeviti wa CCM Wilaya waliofukuzwa ni Salum Kondo Madenge (Kinondoni), Assa Harun Simba (Ilala), Makoi S Laizer (Longido), Wilfred Saileli Ole Mollel (Arusha Mjini), Omary Awadh (Gairo), (Muleba), Ally S. Msuya (Babati Mjini), na Mwenyekiti wa Wilaya ya Bunda.
Wajumbe wa Halamshauri Kuu (NEC) ya CCM waliofukuzwa ni Ali Khera Sumaye (NEC Arumeru), na Mathias Erasto Manga (Arumeru).
Mjumbe wa NEC, Adam Kimbisa, kutoka Dodoma Mjini amesamehewa wakati Dk. Emmanuel Nchimbi amepewa onyo kali, ambapo hataruhusiwa kugombea nafasi yoyote kwa miaka minne.
Wengine waliopewa onyo kali kwa makosa mbalimbali ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Ahmed Kiponza ambaye pia ameondolewa madarakani, Hamis J. Nguli (Mwenyeviti wa Wilaya ya Singida Mjini) ambaye ameachishwa uongozi, Hassan Mzala (M-NEC Singida), Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke, Ali Mchumo (M-NEC Kilwa), Chief Ally Kalolo (M-NEC Tunduru) ambaye amevuliwa ujumbe huo na kupewa onyo kali, Muhaji Bishako (Mwenyeviti wa Wilaya ya Muleba) amepewa onyo kali, na Valerian Alemreta (M-NEC- Kibaha Vijini) ambaye ameachishwa uongozi.
Katika hatua ya kushangaza sana, wapinzani wa CCM wameiona hatua hiyo ya kukisafisha Chama kama ni namna ya kukomoana, visasi na chuki na wengi ndio wamekuwa wasemaji wa wanaCCM huku wakigeuka kuwa watabiri wa ‘kifo cha CCM’.
Wapinzani siyo tu kwamba wanafurahia kwa CCM ‘kujimaliza yenyewe’, lakini tayari wamekwishawafungulia milango wanachama hao waende kujiunga na vyama vyao.
Vyombo mbalimbali vya habari – magazeti, runinga na radio – vimekuwa vikiendesha mijadala mbalimbali kuzungumzia hatua hiyo ya CCM na karibu waandishi na wachambuzi wengi wanasema CCM imefanya makosa.
Mitandao ya kijamii hiyo ndiyo usiseme, kwani imejaa ‘waandishi na wachambuzi’ wengi wanaoendelea kuikosoa CCM kana kwamba jambo lililofanyika ni geni.
Ajabu ni kwamba, wapinzani hao wanaolalamikia mambo yasiyowahusu wanashindwa kuelewa kwamba hata wao wenyewe wamekuwa wakifukuza, tena wengine bila hata kufuata vikao halali wala katiba zao, lakini katu hawasemi.
Wapinzania wanasema uamuzi wa CCM kuwatimua na kuwaadhibu wanachama ambao wamekwenda kinyume na Katiba ya Chama ni wa chuki na visasi, lakini kumbe wao wakifukuzana “wanasafisha vyama vyao kwa kuwaondoa wasaliti”.
Tatizo la wapinzani wa Tanzania ni moja: wanapenda sana kutumia fursa (Opportunists) hata mahali pasipostahili. Tena ni wasahaulifu na hawataki kukumbushwa.
Potelea mbali, mimi nitawakumbusha, na nitawakumbusha kwa mifano ili hata hao wafuasi wao waweze kuelewa, hata kama hawataamini. Potelea mbali!

Migogoro CUF
Mpaka sasa Chama cha Wananchi (CUF) kinaendelea na migogoro na agenda kuu inayozunguka ni ‘kutimuana’. Wapinzani hawalioni hilo bali wanaliona la CCM.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Haruna Ibrahim Nguyulu Lipumba, ametangaza hivi karibuni kuwatimua wakurugenzi mbalimbali, wengine wamevuliwa madaraka yao.
Hivi sasa mkakati wao ni kumtimua Katibu Mkuu, ‘kisiki’ Maalim Seif Sharrif Hamad, na inaelezwa kwamba wako tayari kutumia hata nguvu ya polisi kumng’oa.
Lakini haya yanafanyika baada tu ya Profesa Lipumba kurejea madarakani kwa nguvu ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini baada ya kiongozi huyo kutimuliwa tangu mwaka 2016 alipotaka kurejea kwenye uongozi baada ya kuwa amejiuzulu mwenyewe mwaka 2015. Hakuna anayesema kuhusu timua timua hiyo ya CUF, bali wanaiona ya CCM tu.
Ni CUF hao hao ambao mwaka 2012 waliwatimua akina Hamad Rashid Mohammed na wenzake, kutokana na mgogoro uliokuwepo kabla ya mbunge huyo wa zamani wa Wawi, Pemba hajaenda kuanzisha chama chake.
Lakini naukumbuka mkutano wa mwaka 1994 kule Raskazone, Tanga, ambapo CUF walimtimua mmoja wa waasisi wake, mzee wangu James Mapalala, katika mkakati uliokuwa umewekwa na baadhi ya viongozi wa juu kuhakikisha ‘Mkristo hawi mwenyekiti’.
Ndiyo maana mwaka 1995 wakaamua kumchukua msomi Profesa Lipumba, ambaye awali alikuwa ‘amedakwa’ na Chama cha NRA, lakini akakitosa. CUF wakampa nafasi ya kugombea urais.
Leo hii hakuna anayethubutu kukumbuka hayo ya CUF isipokuwa wanaishambulia CCM kwamba inafanya kwa chuki na visasi!

NCCR-Mageuzi na TLP
Hakuna asiyefahamu kwamba NCCR-Mageuzi ndicho kilichokuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara tangu mwaka 1995. Nguvu kubwa ambayo chama hicho kiliipata ni baada ya ‘kumsajili’ Augustine Lyatonga Mrema muda mfupi baada ya kuondoka CCM Februari 1995.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wa wakti ule, Mabere Nyaucho Marando, aliamua kumkaribisha na akampisha hadi kwenye kiti chake kabla ya kumpatia nafasi ya kuwa mgombea urais.
Kutokana na mvuto mkubwa aliokuwa nao Mrema wakati huo, aliweza kuleta ushindani mkubwa kwenye uchaguzi huo mkuu wa kwanza wa vyama vingi na akashika nafasi ya pili nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM.
Lakini mgogoro ukaanza mwaka 1996, tena baada ya Mrema kupata ubunge wa Temeke katika uchaguzi mdogo kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Ramadhan Kihiyo wa CCM, kuvuliwa na mahakama.
Mgogoro huo ukashika kasi hadi walipokwenda Tanga mwaka 1997, ambapo mkutano wao uliingia dosari baada ya taa kuzimwa usiku na ‘waasi’ wa NCCR-Mageuzi wakaanza kurusha viti kumshambulia Mrema ambaye alikuwa anataka kukifanya chama mali yake, kwa mujibu wa taarifa zao.
Mrema amshukuru sana kaka yangu Kagenzi, aliyekuwa mlinzi wake, ambaye mara taa zilipozimwa, akitumia mbinu za hali ya juu, aliweza kumwingiza Mrema chini ya meza halafu yeye akaanza kupangua viti ambavyo vilikuwa vikirushwa kuelekea meza kuu kwa lengo la ‘kumpopoa Mrema’. Baadaye aliweza kumtoa nje na hivyo kumnusuru na zahama hiyo.
Tangu wakati huo Mrema akaapa kuwatimua waasi. Na kweli aliwatimua wote, akiwemo Marando ambaye ndiye aliyemkaribisha, pamoja na wanachama wengine kama Dk. Masumbuko Lamwai na wengineo.
Mgogoro ulivyozidi kupamba moto wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, Mrema akaondoka – kwa ‘kutimuliwa na wanachama’ – pamoja na akina Msafiri Mtemelwa.
Leo Herman Lwekamwa, aliyekuwa mwenyekiti na mwanzilishi wa Chama cha Labour (TLP), akamkaribisha Mrema na wenzake, akiwemo Thomas Ngawaiya.
Lwekamwa akamkabidhi uenyekiti, yeye akawa mwanachama wa kawaida. 

Mrema akashika nafasi ya tatu mwaka huo nyuma ya Ben Mkapa na Profesa Lipumba. Ngawaiya akawapata TLP ofisi pale kwenye mjengo wake Manzese-Argentina.
Lakini ghafla mambo yakabadilika. Mgogoro ukatokea, na Mrema akaamua kuwatimua wanachama wengi ‘wakorofi’ akiwemo Leo Lwekamwa aliyemkaribisha.
Tangu wakati huo hajabanduka madarakani na hana dalili za kuondoka leo, kesho au mtondogoo. 
David Kafulila, mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kujenga ushawishi naye wakati akiwa kiongozi na mbunge ndani ya chama cha NCCR-Mageuzi alikutana na dhoruba hiyo baada ya kufukuzwa kabla ya kusamehewa na kurejeshewa uanachama wake. Hivi sasa ameelekea tena Chadema ambako awali walimletea figisu!
Hakuna anayesema isipokuwa tu CCM ni watu wa chuki na visasi!

Chadema
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kwa sasa ndicho kikuu cha upinzani nchini, ndicho kinachoongoza kejeli hizi za CCM kuwatimua wanachama wake.
Wafuasi wa Chadema, ambao wanashinda na kukesha kwenye mitandao, wengi wakiwa ni vijana ‘wasiojitambua wala kuelewa siasa ni nini isipokuwa tu kuongozwa na mihemko’, wanaendelea kujaza kurasa za mitandao kwa hoja muflisi kwamba CCM imejimbia kaburi kwa kuwatimua wanachama wake.
Hakuna hata mmoja miongoni mwao anayekumbuka namna Chadema ilivyowatimua akina David Kafulila na wenzake mwaka 2009 kwa madai kwamba walikuwa wafuasi wa Zitto Kabwe ambaye wakati huo alikuwa ameanzisha kampeni ya kutaka kuwania nafasi ya uenyekiti.
Hakuna hata mmoja ambaye anakumbuka kwamba mwaka 2008 Chadema walimsimamisha u-makamu mwenyekiti Chacha Zakayo Wangwe (R.I.P.), aliyekuwa mbunge wa Tarime, kwa sababu tu alihoji kuhusu masuala nyeti yaliyomgusa moja kwa moja Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, yakiwemo ya upendeleo, ukabila, ukanda pamoja na mapato ya chama na madeni ambayo Mbowe alidai alikuwa anakidai chama.
Hata wakati mauti yanampata Wangwe alikuwa safarini kutoka Dodoma kuja kujitetea kwenye Kamati Kuu. Hakuna ajuaye nini ambacho kingetokea kama ajali ile isingetokea.
Wafuasi wa Chadema, ambao siku hizi wamebatizwa jina la ‘nyumbu’, hawataki kuzungumzia lolote kuhusiana na kutimuliwa kwa akina Mtera Mwampamba na Juliana Shonza na wenzao, ambao waliwatuhumu kwamba walikuwa wakiunda Kundi la PM7 – Pindua Mbowe lililokuwa likiundwa na vijana ama wanachama 7.
Kilichowaponza pia ni ‘ukaribu’ wao na Zitto Kabwe, ambaye aliendelea kuonekana kama mwiba mkali kwa Chadema na walikuwa wakimtafutia nafasi kama mchezo wa ‘kuotea’ (Offside-Trick).
Na hatimaye walimpata Zitto na school-mate wangu Profesa Kitila Mkumbo mwaka 2013 baada ya kusema waliudaka waraka uliokuwa umelenga kufanya mapinduzi ndani ya chama.
Zitto na Profesa Kitila wakatimuliwa pamoja na ‘wafuasi’ wao na Chadema hao hao wakasema ‘wanasafisha chama kwa kuondoa waasi’.
Sasa iweje leo hii CCM, ambayo wapinzani hao hao wamekuwa wakisema inawaleta wanachama ‘waovu’, inapoamua kujisafisha hawa wapinzani waseme ni ‘chuki na visasi’? Ina maana ni wao tu wapinzani wanaoweza kujisafisha?

Wengi waliondoka CCM
Waliotimuliwa hivi karibuni si wa  kwanza kuondoka ndani ya CCM. Utamaduni huo umekuwepo kitambo tangu enzi za uenyekiti wa Mwalimu Julius Kambarage Burito Nyerere.
Tena ni jambo la kawaida kwa vyama vya siasa kuwafukuza, kuwasimamisha, kuwavua madaraka wanachama ama viongozi wake, si hapa Tanzania pekee, bali hata katika mataifa mengine.
Miaka ya nyuma kabisa enzi za Tanganyika African National Union (Tanu), walifukuzwa akina Fortunatus Masha, Balozi Christopher Kasanga Tumbo, Oscar Saratiel Kambona, James Mapalala na wengine wengi, baada ya kupishana na Mwalimu Nyerere kutokana na kwenda kinyume na misingi ya chama.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1985, akina Maalim Seif Sharif Hamad, Hamad Rashid Mohamed, Juma Duni Haji walifukuzwa ndani ya CCM baada ya kudaiwa kuufitini uchaguzi wa mwaka huo.
Walikuwa wakipinga ama hawakuridhika na uamuzi wa CCM kumpitisha Idris Abdul Wakil Nombe kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Matokeo yake, kwa kuwa ilikuwa enzi ya chama kimoja, wakafungiwa kujihusisha na siasa. Wangekwenda wapi kufanya siasa wakati CCM pekee ndiyo ilikuwa imeshika hatamu?
Ujio wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 ndio uliowatoa kifungoni na moja kwa moja wakaingia upinzani kwa kuanzisha vyama vyao.
Kama ilivyo kwa wapinzani ambao daima huangalia kasoro za serikali ama kuanzisha choko choko, vivyo hivyo wapo baadhi ya wanachama wakorofi, wasiojua itifaki, wasiojua falsafa na itikadi za vyama, ambao kazi yao ni vurugu, kutukana na hawaheshimu hata viongozi wao.
Wapo watu ndani ya vyama, kwao busara na maslahi ya chama si kitu, jambo litafanyika kwenye vikao vya ndani, yeye kazi yake ni kusambaza nje hata taarifa za vikao vya ndani, hawa huwadhihaki viongozi wao mpaka mitandaoni bila kujali athari inayoweza kukikuta chama.
Niwafananishe na nani wapinzani jamani? Nitawafananisha na watoto wadogo, ambao walisema: “Tuliwapigia ngoma, hamkucheza. Tuliwaimbia nyimbo, hamkuitikia!”
Kwa nini kila baya ni la CCM? Kwa nini hata pale inapojikosoa na kijisafisha bado mnaiona kwamba ni mbaya? Propaganda hizi inabidi zifike mwisho! Mwenye masikio na asikie, na mwenye macho na aone!

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com