Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt.
Jakaya Kikwete amesema kuwa anapenda kuendelea kufanya shughuli
zinazosaidia kuleta maendeleo kwa watu na jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
Jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa akizindua Taasisi yake ya Jakaya
Kikwete (Jakaya Mrisho Kikwete Foundation) alisema kuwa kwa muda mrefu
amekua akipenda na kujihusisha na shughuli mbalimbali za maendeleo ya
watu na hivyo Taasisi yake itamsaidia katika kufikia malengo yake.
“Nimetumia muda wangu kwa ajili ya
maendeleo ya watu, baada ya shule, nilikitumikia Chama cha
Mapinduzi(CCM), nilitumikia Jeshi na baadae Serikali, kwangu Taasisi hii
imekuwa chombo kitakachonisaidia kuendeleza maono yangu na kutimiza
ndoto zangu katika kuendelea kusaidia watu” alisema Dkt. Kikwete.
Akiizungumzia taasisi hiyo Kikwete
alisema kuwa, Taasisi yake ina wajumbe 9 kutoka sehemu mbalimbali
duniani wenye nyadhifa na heshima kubwa katika nchi zao.
Ameongeza kuwa Taasisi hiyo imejikita
kusaidia jamii katika maeneo makubwa manne, maendeleo ya jamii hasa
katika kujikita kuondoa umaskini, mabadiliko ya hali ya nchi na kilimo
kwa wakulima wadogo.
Pia Taasisi hiyo imejikita katika huduma za afya, kutokomeza malaria na afya ya mama na mtoto.
Maeneo mengine ambayo Taasisi hiyo
inajihusisha nayo ni ni elimu kwa vijana ili kukuza vipaji vyao na
kuwapa mafunzo kuhusu uongozi bora, usawa wa kijinsia na namna ambavyo
Serikali inavyotoa huduma kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa Taasisi yake
itaisaidia Serikali, mashirika na Taasisi mbalimbali ili kushirikiana
kuwaletea maendeleo watanzania na watu mbalimbali duniani.
Dkt. Kikwete amewataja Wajumbe wa Bodi
ya Udhamini ya Taasisi yake kuwa ni Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Katibu
Mkuu Kiongozi, Profesa Rwekaza Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha
Dar es Salaam (UDSM), Profesa Willium Mahalu Mhadhiri Mwandamizi katika
Chuo Kikuu cha Tabibu cha Bugando.
Wengine ni Balozi Mwanaidi Maajar
aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Abubakar Bakhresa,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Bakhresa, Genevieve Sangudi
Mtaalamu wa Masuala ya kibishara ya Kimataifa kutoka Marekani.
Pia wapo Dato’ Sri Idris Jala, Waziri
asiyekuwa na Wizara Maalumu nchini Malyasia, Balozi Charles R. Stith
aliyekuwa Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania pamoja na Dkt.
Carlos Lopes ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taaisi ya Mafunzo na
Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).
Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya Kikwete
ilisajiliwa tarehe 17, Februari 2017, na hii ni mara ya kwanza kwa
wajumbe wa bodi ya wadhamini kukutana tangu kuanzishwa kwake.
0 comments:
Post a Comment