Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imetishia kuifuta kesi inayomkabili Mkurugenzi
Mtendaji wa mtandao wa JamiiForums, Maxence Mubyazi Melo na mwanahisa wa
kampuni ya Jamii Media Co Ltd, Mike William ikisema haifurahishwi na
mwenendo wa shauri hilo.
Hakimu
mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba alisema hayo jana mara baada
ya Wakili wa Serikali, Hamis Said kueleza kuwa wakili anayeendesha kesi
hiyo ni mgonjwa na kwamba jana ilikuwa siku ya washtakiwa kusomewa
maelezo ya awali.
“Haya mambo ya kuahirishaa- hirisha kesi siyafurahii. Wakati mwingine (kama) kesi haiendelei, nafuta,” alisema Hakimu Simba baada ya wakili huyo wa Serikali kuomba kesi hiyo iahirishwe hadi Machi 20.
Hakimu
Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 3, siku ambayo washtakiwa hao
watasomewa maelezo ya awali katika kesi hiyo ambayo washtakiwa wanadaiwa
kuzuia uchunguzi wa Jeshi la Polisi.
Washtakiwa
hao wanaotetewa na mawakili, Tundu Lissu, Jeremiah Mtobesya, Tika
Hamis, Hassan Kihangio, Fedrick Kihwelo na Masoud George, watasomewa
maelezo hayo ya awali baada ya upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi
wa kesi hiyo.
Katika
kesi hiyo, namba 456/2017, inadaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba
13 mwaka jana, wakiwa Mikocheni, wakiwa wakurugenzi wa Jamii Media
ambayo inaendesha tovuti ya Jamiiforums walishindwa kutoa taarifa kwa
Jeshi la Polisi ambalo lilikuwa likichunguza mawasiliano ya kimtandao
yaliyochapishwa katika tovuti yao. Washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana.
0 comments:
Post a Comment