Ndugu Zangu,
Uvumi wa mumiani wanyonya damu ndio uliopelekea watafiti wetu na dereva wao kuawa kinyama na wananchi wasio na uelewa na walioaminishwa kwenye abrakadabra, mambo yasio ya kweli wala maana yeyote.
Mfalme Suleiman aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; “ Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?”
Hivyo, Mfalme Suleiman aliomba apewe hekima. Alifahamu, kuwa watu wake wanaangamia kwa kukosa hekima.
Inasikitisha sana kuona, kusoma habari za mauaji ya kinyama yaliyofanywa kwa watafiti kwenye kijiji cha Mvumi, Dodoma.
Kuna shida sana ya uelewa miongoni mwa watu wetu. Abrakadabra nayo imetamalaki kwenye jamii. Tumeona, hata viongozi wa dini wameshiriki katika kusukuma kilichotokea kwa imani potofu na kimsingi za kishirikina.
Ni wakati sasa wa kuchukua hatua ikiwamo kuwadhibiti wale wenye kutumia imani kwenye kuwapotosha wananchi. Wengine wao wana uwezo hata wa kununua vipindi vya redioni na kwenye televisheni kusambaza mambo ya abrakadabra.
Nimechokoza mjadala.
Maggid Mjengwa.
0 comments:
Post a Comment