Waziri
wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amesema hati ya shamba lililopo maeneo ya Bunju la aliyekuwa Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fredrick Sumaye liko katika hatua
ya kufutwa na kwamba Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kinondoni Rehema
Mwinuka ameshatoa barua ya notisi ya siku 90.
Lukuvi ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wandishi wa habari.
“Shamba la Sumaye hati yake iko katika hatua za kufutiwa,
Afisa
Ardhi Mteule wa Wilaya ambaye anajukumu la kutoa notisi, ameshatoa
notisi kwamba hajaendeleza eneo hilo kwa muda mrefu hivyo kwa mujibu wa
sheria hati yake inatakiwa kufutwa,” alisema.
Alisema serikali haitofumbia macho wamiliki wa ardhi na mashamba ambao hawajayaendeleza kwa muda mrefu.
Pia,
kufuatia ongezeko la matapeli wanaotumia nyaraka za kughushi za barua
za toleo (ofa) zinazodaiwa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam, Lukuvi alitoa
agizo hususani kwa wakazi wa jiji hilo wanaomiliki ardhi pasipo kuwa na
hati miliki, kujisalimisha kwa kupeleka barua zao za ofa kwa Kamishna
wa Ardhi ili wapatiwe hati halali.
“Wamiliki
wote wanaomiliki ardhi kwa karatasi za ofa halali wazibadilishie ili
wapewe hati halali, na atakaegundulika kumiliki ofa feki polisi
watawakamata na kupelekwa mahakamani,” alisema.
Alisema
asilimia 60 ya watu wanaopeleka kesi za migogoro ya ardhi wizarani,
chanzo cha migogoro hiyo ni karatasi za ofa zinazotoka katika
halamshauri za jiji na manispaa.
“Natoa
miezi mitatu ili karatasi hizi zisitokee tena kila mtu alete barua ya
ofa watapewa hati zao ndani ya mwezi mmoja ,wazilete kwa kamishna wa
ardhi wa mkoa, baada ya hapo sitasikiliza malalamiko ya watu walioibiwa
ardhi wakiwa na ofa ya namna hii.
“Tumieni miezi mitatu vizuri kubadilisha ofa,” amesema.
Hali kadhalika, Lukuvi alipiga
marufuku vitendo vya uvamizi wa ardhi na mashamba vinavyofanywa na
baadhi ya wananchi, na kuwataka wananchi kutoa taarifa pindi
watakapobaini kuwa kuna shamba au ardhi isiyoendelezwa.
“Serikali
ina laani uvamizi wa ardhi na mashamba unaofanywa na baadhi ya wananchi
sababu baadhi yao yanamilikiwa kihalali na yana hati, serikali ipo na
sheria zipo zitafanya kazi yake,” alisema.
0 comments:
Post a Comment