Mbunge wa
jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akikabidhi magodoro kwa wanafunzi
na mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Moreto ,Justine Lyamamu ,ambapo
bweni la wasichana katika shule hiyo liliungua wiki iliyopita.
Mbunge wa Chalinze Ridhiwani akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya chalinze, Mkurugenzi na maafisa wengine wa halmashauri ya Wilaya Chalinze.
Mbunge wa
chalinze ametimiza ahadi yake ya kuchangia magodoro 200 na Halmashauri
ya wilaya ya chalinze kwa shule ya Sekondari ya Moreto.
Mbunge akisema neno la ushauri na kuwatia moyo vijana kwa tukio lililowakuta na kwa utulivu uliotokea.
Wanafunzi
wa shule ya sekondari Moreto iliyopo Lugoba wilayani Bagamoyo,
Mwanahamis Msonde na Sekion Mponela wakimshukuru Mbunge wa jimbo la
Chalinze Ridhiwani Kikwete na mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze
Saidi Zikatimu kwa msaada wa magodoro.
MBUNGE
wa jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete kwa kushirikiana na halmashauri
ya Chalinze,wametoa magodoro 200 yaliyogharimu zaidi ya mil.8 ili
kuwasaidia wanafunzi wa shule ya sekondari ya Moreto iliyopo Lugoba
wilayani Bagamoyo.
Aidha
Ridhiwani ameahidi kushirikiana na wadau pamoja na halmashauri
hiyo,kujenga bweni jipya la wanafunzi wa kike,shuleni hapo baada ya
kuunguliwa na bweni wiki iliyopita.
Sambamba na hayo tathmini imebaini hasara ya sh.mil 74 baada ya bweni hilo kuungua na kusababisha mali zote kuteketea kwa moto.
Akikabidhi
magodoro hayo ,kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo,Justine Lyamuya ,mbunge
huyo alisema kati ya magodoro hayo 136 yatatumiwa na wanafunzi wa kike
na yatakayobaki yatatumika na wanafunzi wa kiume.
Ridhiwani alisema mara baada ya kutokea kwa janga hilo, alitoa magodoro 50 yenye thamani ya mil.2.2 kwa nguvu zake mwenyewe.
Hata
hivyo aliwataka wanafunzi hao kushirikiana na serikali na vyombo vya
dola kuwafichua waliohusika na tukio la kuchoma moto bweni.
Ridhiwani
alielezea kuwa serikali itahakikisha waliohusika kuchoma moto bweni
hilo,wanatafutwa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Alisema
tukio hilo linasikitisha na kurudisha nyuma juhudi za serikali na wadau
mbalimbali wa elimu wanaohakikisha wanafunzi wanakaa bweni .
“Tumeweka
mikakati ya kuhakikisha tunawakamata wale wote waliohusika na tukio
hili baya na matukio haya ni mwendelezo wa uunguzaji wa shule ambapo
Chalinze imechomwa mara mbili,” alisema Ridhiwani.
Ridhiwani aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kushirikiana kutatua changamoto zilizojitokeza shuleni humo.
Nae
mwalimu mkuu wa shule hiyo Justine Lyamuya alifafanua kuwa vitu vyote
viliungua ikiwa ni pamoja na vitanda na magodoro 75 vyenye thamani ya
mil. 24.
Alisema bweni hilo lilijengwa hivi karibuni kwa thamani ya mil.50 ambalo limeungua lote na halifai tena kutumika.
“Moto
huo uliunguza vitu vyote vilivyokuwemo ikiwepo magodoro, vitanda 75,
madaftari, vitabu, nguo na vifaa vingine lakini mungu alisaidia kati ya
wanafunzi 196 wanaolala bweni hili,hawakuwepo bwenini,” alisema Lyamuya.
Mwenyekiti
wa halmashauri ya Chalinze,Said Zikatimu alisema licha ya kuchangia
magodoro hayo tayari wameitisha kikao na wazazi, walezi na wadau wa
elimu ili kujadili namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
Baadhi
ya wanafunzi Sekion Mponela na Mwanahamis Msonde walimshukuru mbunge wa
Chalinze na halmashauri kwa msaada walioutoa na kuahidi kutunza
magodoro hayo.
0 comments:
Post a Comment