METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 22, 2016

Majaji watakiwa kuzingatia maadili

MAJAJI wa Mahakama Kuu nchini wametakiwa kufanya kazi yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo wakati wote, kwa kuwa watanzania wanategemea kutendewa haki na kwa wakati mahakamani.

Akifungua Mkutano wa Majaji Wafawidhi na Majaji Waliosikiliza Kesi za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, unaotathmini usikilizwaji wa kesi hizo jijini Arusha jana, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ferdinand Wambali alisema watanzania wana imani na mahakama, hivyo ni muhimu kwa majaji hao kutenda haki wakati wote.

Alisema majaji hao wamekutana ili waweze kupata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali, zilizojitokeza wakati wa kusikiliza kesi zilizohusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kubadilishana mawazo namna ya kuzimaliza kwa haraka kesi zinazohusu uchaguzi kwa siku za mbele.

Jaji Wambali alisema jumla ya kesi 53 za ubunge, zilizotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, zilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda za Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza. Kanda nyingine ni Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Tanga.

Jaji Wambali alisema kati ya kesi hizo, kesi 31 zilimalizika katika hatua za awali na kesi 22 ziliendelea. Mpaka sasa kesi 19 zimemalizika na kuongeza kuwa kesi tatu bado ziko mahakamani.
Alieleza kuwa ni jambo la kujivunia kwa Mahakama ya Tanzania, kwa kuwa kesi zote 196 zilizotokana na uchaguzi wa madiwani zilimalizika mapema katika mahakama mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu nchini, zaidi ya asilimia 94 ya kesi za uchaguzi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu, zimemalizika wakati asilimia 100 ya kesi zote za udiwani zimemalizika.

Jaji Kiongozi aliwapongeza majaji na mahakimu wote, kwa kumaliza kesi kwa ufanisi na kwa wakati, licha ya changamoto mbalimbali wanazozipitia watumishi hao wa mahakama wakati wanaposikiliza kesi zinazotokana na uchaguzi.

Aidha, Jaji Wambali alilishukuru Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kufadhili mafunzo mbalimbali ya majaji na mahakimu, yaliyotolewa kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Mkutano wa siku nne wa Majaji Wafawidhi pamoja na Majaji waliosikiliza kesi za uchaguzi, ulianza jana jijini Arusha na umefadhiliwa na shirika hilo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com