METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 27, 2016

KATA 345 ZAFAIDIKA NA MRADI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO KWA WOTE

kamuzo
Katibu Mkuu  Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Faustine Kamuzora akiwa na mwakilishi kutoka Benki ya Dunia anaeshughulikia masuala ya Habari na Mawasiliano Bi.Boutheina Guermazi wakati wa warsha ya Habari na Mawasiliano  ikizungumzia mafanikio ya mradi wa kuboresha miundombinu ya Mawasiliano nchini na Serikali mtandao.

Na Daudi Manongi, MAELEZO

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Faustine Kamuzora amesema kuwa kata 345 zimefaidika na mradi wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini na Serikali mtandao kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote.

Profesa  Kamuzora  amesema  hayo  katika Warsha  ya Habari na Mawasiliano  iliyoandaliwa na Benki ya Dunia ikishirikiana na Wizara hiyo ikizungumzia mafanikio ya mradi wa kuboresha miundombinu ya Mawasiliano nchini na Serikali mtandao.

“Kupitia Serikali mtandao tunataka huduma za serikali ziwafikie wananchi kokote walipo na tunafahamu sasaivi wananchi wengi wana simu za mkononi na hivyo tunataka huduma kama za manunuzi kama tenda za Serikali na usajili wa vizazi na vifo kuanzia sasa  zipatikane kwa njia ya mtandao ,huduma hii itaongeza uwazi,ufanisi na ubora wa huduma katika shughuli mbalimbali za Serikali.”Alisema Prof Kamuzora.

Pia Profesa Kamuzora amesema kuwa Mradi huo ulilenga kufikisha mawasiliano vijijini na maeneo ambayo ni magumu kufikika na wafanyabiashara na ilipata mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 100 kutoka Benki ya Dunia ambao umesaidia kutoa ruzuku kwa makampuni mbalimbali ya simu ili yaweze kujenga minara kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara na hivyo kufanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 2.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia anaeshughulikia masuala ya Habari na Mawasiliano Bi.Boutheina Guermazi amesema kuwa wataendelea kusaidia sekta ya mawasiliano nchini kwa kuwa ni muhimu katika maendeleo ya nchi yeyote na hivyo hawatasita kutoa misaada mbalimbali iwapo watahitajika kufanya hivyo.

Akizungumzia mafanikio ya mradi huo amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na maboresho makubwa katika mawasiliano na upatikanaji wa vifurushi vya intaneti kwani sasa vimekuwa vya bei ya chini tofauti na mwanzo ambavyo vimesaidia upatikanaji wa mawasiliano katika maendeleo ya nchi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com