METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, October 25, 2016

JK ataka UDSM ilinde hadhi yake

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Jakaya Kikwete amekitaka chuo kikuu hicho (UDSM) kilinde hadhi yake ya kuendelea kuwa kiongozi katika utoaji wa elimu bora, ambayo itasaidia taifa kuwa na wataalamu wenye kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili kijamii.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Kikwete alisema hatua ya chuo hicho kufikisha umri huo ni wazi kuwa kimekomaa na kimetoka katika hatua mojawapo ya makuzi na kwenda nyingine, hivyo kinastahili kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa wahitimu wenye kuleta mabadiliko katika nchi.

Kikwete ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa mkuu wa chuo hicho, alisema licha ya chuo hicho kutoa mchango mkubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kutoa viongozi wa nchi na wataalamu ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kutunga sera za nchi, kinatakiwa kutoa wahitimu ambao wanakidhi soko la ajira.

"Nawasihi mafanikio ambayo mmeyapata kwa miaka 55, endeleeni kuwa kitovu cha kutoa elimu bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salam kiongoze wengine wafuate," alisema Rais Kikwete ambaye pia ni miongoni mwa wahitimu waliosoma chuoni hapo katika miaka ya 1970.

Alitoa mwito kwa uongozi wa chuo hicho kuhakikisha wanakuja na mambo mapya ya maendeleo ya kukijenga chuo hicho na sio mambo mapya ya kubomoa mambo mazuri ya maendeleo ambayo yamepatikana chuoni hapo miaka ya nyuma.

Akizungumzia uongozi wake kama mkuu wa chuo, alisema mara tu baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa chuo, alichofanya ni kukutana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya chuo ili kujua matatizo yanayokikabili chuo hicho na namna ya kutatua changamoto hizo.

Alisema licha ya kuelezwa changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa hosteli kwa wanafunzi, alichofanya ni kukutana na Rais John Magufuli kumwelezea changamoto hizo ambazo zinahitaji msaada wa serikali na ndio maana Rais alienda kuzindua ujenzi wa hosteli chuoni hapo. Aliahidi kushirikiana na Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kushughulikia kero mbalimbali zinazokikabili chuo hicho.

"Nitatumia uwezo wangu wote kuhakikisha tunapunguza kero hizo kwa manufaa ya chuo hiki,” alieleza Kikwete.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala alitaja changamoto zinazokikabili chuo hicho kuwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umesababisha kuwa kikwazo cha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya chuo hicho pamoja na kukwamisha shughuli za utafiti.

Pia alisema chuo hicho kinakabiliwa na uhaba wa maabara, ofisi na uhaba wa hosteli za wanafunzi na nyumba za wafanyakazi. Changamoto nyingine aliyoitaja ni uhaba wa wahadhiri wenye uzoefu katika fani mbalimbali.

"Tunaishukuru serikali na wahisani mbalimbali kwa kuendelea kushughulikia changamoto hizo, baadhi ya vyumba vikubwa vya mihadhara vimejengwa pamoja na maabara. Pia tunashukuru uamuzi wa serikali kuamua kujenga hosteli yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,000,” alisema Profesa Mukandala.

Profesa Tade Aina kutoka Chuo Kikuu cha Lagos, Nigeria ambaye ndiye aliyetoa mhadhara maalumu wa Mkuu wa Chuo katika mada yake iliyozungumzia taasisi za elimu ya juu za Afrika, alishauri vyuo vya afrika vitoe elimu inayoendana na mahitaji ya taifa na bara la Afrika.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com