Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Mhandisi Felchesmi
Mramba, (wapili kulia), akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Shirika
hilo mkoani Kagera, Mhandisi Francis Maze, (kulia), wakati alipotembelea
kituo cha Kabeta
Wateja
wakiwa wamepanga foleni kupata huduma za umeme kwenye kontena
lililowekwa nje ya ofisi za Shirika hilo mkoani Kagera, baada ya jengo
hilo kuathirika vibaya
Said, Bukoba
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba, amekagua miundombinu ya Shirika hilo iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi na kuzungumza na wafanyakazi mjini Bukoba mkoani Kagera leo Septemba 16, 2016.
Karibu jengo lote la Ofisi za makao makuu ya TANESCO, limepata nyufa nyingi na hivyo kuufanya uongozi wa Shirika hilo mkoani Kagera, kuhamishia shughuli zake nje ya jengo, ikiwa ni pamoja na kuwahudumia wateja kwenye makontena mawili ambayo yamewekwa nje ya Ofisi hizo.
Mhandisi Mramba ambaye amewasili mjini Bukoba mapema leo asubuhi Septemba 16, alianza ziara yake kwa kukagua vituo vya kupoozea na kusambaza umeme vya Kabeta, Kyaka na Misenyi na kuzungumza na wafanyakazi.
“Nianze kwa kuwapongeza wafanyakazi wenzangu kwa hatua za haraka mlizochukua mara baada ya kutokea tetemeko la ardhi, kwa kuhakikisha mnazima umeme, hiyo imepelekea kuepusha vifo ambavyo vingesababishwa na umeme wakati wa tetemeko hilo,” Alisema Mhandisi Mramba, wakati akiongea na wafanyakazi nje ya jengo la makao makuu ya TANESCO mkoani Kagera.
Mhandisi Mramba, pia alisema, “Baada ya kukagua vituo vyetu vya kupooza na kusambaza umeme, tunashukuru Mungu, hakuna athari katika mifumo yetu ingawa majengo yamepata nyufa na mengine yanahitaji kufanyiwa ukarabati wa haraka,” alsiema.
Mhandisi Mramba pia aliwataka wafanyakazi wa TANESO, kuwasaidia wenzao waliopatwa na athari kutokana na tetemeko hilo ambapo yeye mwenyewe alianzisha harambee na kufanikiwa kukusanya jumla ya shilingi milioni 3.3 zikiwemo fedha taslimu na ahadi zilichangwa.
“Sisi kama shirika tumekwisha toa mchango wetu wa jumla kusaidia waathirika wa tetemeko hili kupitia Msajili wa Hazina, lakini kwa vile waathirika wa tetemeko hili ni watanzania wenzetu, ni wadau wetu wakubwa, nimeagiza ofisi zetu kote nchini kuzungumza na wafanyakazi ili tufanye mchango kuwasaidia watanzania wenzetu.” Alisema.
Naye Meneja wa TANESCO mkoani Kagera, Mhandisi Francis Maze, aliwapongeza wafanyakazi wa wake kwa kufanya kazi kubwa katika kipindi chote tangu janga hilo litokee, na kuwataka waendelee kulitumikia taifa kwa moyo wa kizalendo na upendo.
Watu 17 walipoteza maisha, huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa na nyumba zaidi ya 5,000 zikiharibiwa na tetemeko hilo lenye ukubwa wa kipimo cha Richa 5.7 na lililotikisa umbali wa kilomita 10 chini ya ardhi. Tetemeko hilo lilitokea majoira ya jioni ya Septemba 10, 2016.
Mhansisi Mramba akiongea na waandishi wa habari baada ya kutembelea kituo cha Kabeta
Mhandisi Francis Maze
Mwangalizi msaidizi wa ofisi za Kituo cha kupoozea na kusambaza umeme cha Misenyi
Mhandisi Mramba, akikagua athari za tetemeko kwenye makao makuu ya TANESCO mkoani Kagera
Mhandisi Mramba, na ujumbe wake wakitembelea kituo cha Misenyi
Mhandisi Mramba (kushoto), akizungumza na wafanyakazi
Mfanyakazi wa TANESCO mkoani kagera ambaye nyumba yake iliathirika akizungumza kwenye mkuytano huo
Wafanyakazi wa TANESCO mkoani Kagera
Hili ndilo jengo linalotumiwa na TANESCO kama makao makuu yake mkoani Kagera, ambalo limepata nyufa nyingi na kupelekea huduma za umeme kwa wateja kutolewa nje ya jengo hilo ambapo wateja wanaonekana wakiwa kwenye foleni.
0 comments:
Post a Comment