Waziri
Kassim Majaliwa amesema safari ya kuhamia Dodoma imeiva na amewataka
watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wajipange kisaikolojia.
Ametoa
kauli hiyo leo Agosti 18, 2016 alipokutana na kuzungumza na watumishi
wa ofisi yake kutoka taasisi, idara na vitengo mbalimbali waliopo Dar es
Salaam.
Waziri
Mkuu amewataka watumishi hao watambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia
Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao
chimbuko lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano
Mkuu wa 16 wa chama cha TANU.
“Tangu
wakati huo kumekuwa na juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuandaa
miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji
wa miundombinu hiyo,” amesema.
“Pia
tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai
23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena
Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo
hiyo nikaweka msisitizo,” amesema.
“Napenda
kuwatoa hofu, mambo yanaenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva
sasa. Kikubwa ni kwamba tutakwenda kwa awamu kama ambavyo imepangwa,” amesema.
Amewataka
watumishi hao wazidishe mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa
wana dhamana ya kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu.
“Watumishi
wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo. Tufanye
kazi kwa bidii. Tuhakikishe kila kilichopangwa kinafanyika kwa ufanisi
na kinafanikiwa,” amesema.
Julai
25 katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, Waziri Mkuu aliwataka
mawaziri wote kuhamia Dodoma mara moja na kusema kuwa yeye atakuwa wa
kwanza ifikapo Septemba.
0 comments:
Post a Comment