WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka Japan na kusema
kwamba kufanyika kwa Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu
Maendeleo ya Bara la Afrika (TICAD VI) jijini Nairobi kumetoa fursa kwa
Tanzania na nchi nyingine kukutana na wafanyabiashara wakubwa wenye nia
ya kuwekeza barani humo.
Ametoa
kauli hiyo Jumapili, Agosti 28, 2016 alipokutana faragha kwa nyakati
tofauti na viongozi wa makampuni makubwa ya Japan ambao walikuwa
wakihudhuria mkutano huo uliofanyika katika kituo cha Mikutano ya
Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini Nairobi, Kenya.
Mkutano
wa sita wa TICAD ambao umemalizika jana, ulilenga kuiwezesha Afrika
katika sekta ya uchumi na uwekezaji. Ili kufikia lengo hilo, mkutano huo
umewashirikisha wadau wa sekta binafsi zikiwemo kampuni binafsi zaidi
ya 300 kutoka Japan.
Katika
mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Rais wa kampuni ya Sumitomo, Bw.
Kuniharu Nakahura, alisema kampuni hiyo imeanza utekelezaji wa mradi wa
Kinyerezi II wa kuzalisha umeme wa MW240 kutoka gesi asilia (Gas Fired
Combined Cycle Gas Power Plant). Mradi huo ulioanza kutekelezwa Machi
2016, unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu.
Bw.
Nakahura ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, alisema
kampuni yao inajishughulisha zaidi na utengenezaji wa bidhaa za vyuma,
kemikali, ujenzi wa miundominu, na usafirishaji.
Naye
Makamu wa Rais wa kampuni ya Toyota Tshuso, Bw. Yasuhiko Yokoi
alikutana na Waziri Mkuu na kumweleza jinsi kampuni hiyo kubwa duniani
inavyoweza kushiriki na kuchangia maendeleo nchini Tanzania.
Alisema
kampuni yao inajishugulisha zaidi na masuala ya miundombinu ikiwemo
kuzalisha mitambo ya umeme na mitambo ya bandari. Pia inazalisha bidhaa
za kilimo (matrekta, mashine za viwanda vya mbolea na nguo, ujenzi wa
maghala ya nafaka), mitambo ya nguvu za umeme wa joto-ardhi na
uzalishaji wa magari ya aina mbalimbali.
“Kwa
mfano hapa Kenya, tumeweza kutengeneza mitambo midogo ya kisasa ambayo
inazalisha mbolea tofauti kulingana na hali halisi ya udongo wa mahali
husika. Huwezi kuzalisha mbolea ya aina moja na kuamua kuisambaza kwa
nchini nzima. Tunapima udongo wa sehemu moja na kuzalisha mbolea
inayofaa kwa udongo ule,” alisema.
Naye
Rais wa kampuni ya Marubeni, Bw. Fumiya Kokubu alimweleza Waziri Mkuu
kwamba maeneo ambayo wangependa kuwekeza ni kwenye viwanda vya nguo,
mbolea, saruji, uzalishaji wa sukari, umeme wa gesi na hasa miradi ya
LNG.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali
iko tayari kushirikiana nao na akawashauri watume timu za maafisa wao
ili wakutanishwe na wadau wa sekta husika.
Alisisitiza
kuwa Tanzania hivi sasa imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na
kwa sababu hiyo inahitaji kuwa na nishati ya kutosha ili iweze kumudu
kuendeleza sekta hiyo. “Serikali ya awamu ya tano imeamua kujenga uchumi
wa viwanda, tunahitaji kujenga viwanda vya kutosha ili tuweze kusindika
mazao ya wakulima ambao wanafikia asilimia 80 ya Watanzania wote.
Tunahitaji masoko ya uhakika kwajili ya mazao wanayozalisha,” alisema.
Akiwa
kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu pia alikutana na kufanya mazungumzo na
Balozi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi, Bw.
Filippo Grandi; Meya wa Jiji la Yokohama, Bibi Fumiko Hayashi; na Makamu
wa Rais wa Kwanza wa Sudan, Jenerali Bakri Hassan Saleh.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu alitembelea Maonesho ya Biashara ya Afrika na Japan
(Africa-Japan Expo 2016) ambapo Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania
(TANTRADE) na wadau wengine kama Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),
Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bodi ya Utalii Tanzania
(TTB), Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) walishiriki.
Akiwa
huko alitembelea pia mabanda ya Uganda, Rwanda, Sénégal, Kenya, Japan
na UN Habitat. Pia alitembelea banda la wajasiriamali wa nguo kutoka
Tanzania ambao walishiriki maonyesho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja
vya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Jomo Kenyatta (JICC) jijini
Nairobi, Kenya.
Waziri Mkuu alirejea jijini Dar es Salaam jana usiku.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 29, 2016.
0 comments:
Post a Comment