Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amekiri bunge
hilo kusambaratika na kuwa vipandevipande kutokana na vurugu za mara kwa
mara zilizopelekea wabunge wa upinzani kususia vikao hivyo anawaalika
wabunge hao kwenye mazungumzo.
Ndugai,
ambaye kipindi kirefu cha Bunge la Bajeti lililomalizika hivi karibuni,
alikuwa India kwa matibabu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza kwenye kipindi cha Funguka kinachorushwa na televisheni ya
Azam.
Ndugai
alisema ili bunge lifanye kazi yake yake, linahitaji kuishinda
changamoto iliyopo ya bunge kutokuwa kitu kimoja, huku akielezea wazi
kuwa chanzo kikuu kinachosababisha bunge hilo kusambaratika ni pamoja na
"u-vyama" kuzidi na wabunge kutojali maslahi ya taifa.
Sababu
nyingine aliyoitaja Ndugai, ni ugeni wa wabunge ambapo kila
unapofanyika uchaguzi sehemu kubwa ya wabunge huwa ni wageni hivyo wengi
wao wanakuwa hawajaelewa kanuni na tamaduni za kibunge.
Alisema yanayotokea sasa kwa kiasi kikubwa siyo mageni, yalikuwepo tangu wakati wa bunge la 10.
"Hali
hii imeanza zamani kidogo tangu enzi za spika Makinda, wabunge walikuwa
wakitoka nje, wakigomea vikao, wakiadhibiwa n.k. Ugumu ambao tunaupata
ni kwamba kila baada ya uchaguzi wanakuja wabunge wengi wageni ambao
hawajui mambo mengi na mfano ni bunge hili ambapo karibu 70% ya wabunge
ni wapya" Alieleza Ndugai na kuongeza kuwa hata suala la kumsusia
Rais anapokwenda kuhutubia bungeni, limewahi kutokea katika bunge
lililopita.
Pamoja na hayo, Spika Ndugai alisema kuwa hakuna kanuni inayomzuia mbunge kutoka nje ya bunge kwa kuwa ni haki yake
"Hakuna
kanuni inayomkataza mbunge kutoka nje, ni sehemu ya demokrasia yao,
lakini hii ya sasa imezidi, ni jambo lisilopendeza... maana watanzania
wamewatuma kwenda kuwakilisha hoja zao, wanapotoka inakuwa haipendezi".
Aliwasihi
wabunge wa Upinzani kurudi bungeni na kueleza mambo yaliyowaudhi ili
wakae wajadili na watafute ufumbuzi badala ya kuendelea kususia.
Alisema "Wabunge kutoka nje ni jambo ambalo halipendezi hata kidogo, nisingependa niendelee kuliona.
"Nawaomba katika bunge lijalo kama wanahisi tunakosea watueleze, na sisi tuwaeleze wanakosea wapi ili twende sawa"
Kuhusu
malalamiko ya wapinzani dhidi ya Naibu Spika, alikiri kupokea
malalamiko hayo kupitia kwa mbunge james Ole Millya, na yeye
aliyawasilisha kwenye kamati husika lakini hoja zote ambazo walikuwa
wakizilalamikia zilizonekana hazina uthibitisho, hivyo maamuzi ni kwamba
Naibu Spika Dkt Tulia Ackson hana hatia yoyote.
Kuhusu hoja ya Naibu Spika kuendelea kukalia kiti kwa muda wote Ndugai anasema "
Uongozi ndiyo unapanga nani akae pale, sioni tatizo la mtu kukaa kwenye
kiti kwa muda mrefu, lakini kama mtu anakosea, zipo fursa za kupeleka
jambo kwenye kamati badala kulalamika bila kufuata kanuni"
Alisema
haoni tatizo la Naibu Spika na hajui ni mambo gani amewaudhi ila
anadhani kinachowasumbua wapinzani ni hisia za jinsi Naibu Spika
alivyopatikana
"Wabunge
wa upinzani wanapitia changamoto nyingi kabla ya kuingia Bungeni, wengi
wao wanahangaika sana kupata ubunge hadi kufikia hatua ya kulala sana
selo (polisi) kwaiyo namna ya 'kudeal' nao inahitaji uvumilivu kidogo.
Naibu Spika siyo mbunge wa jimbo, na wao wamezoea mbunge wa jimbo ambaye
anafanana nao, Naibu Spika ni mbunge wa uteuzi kwahiyo wanahisi
anafanya kazi kwa kufuata maelekezo kutoka nje ya bunge au anatumikia
mabwana wawili jambo ambalo siyo kweli. Pia adhabu zilizokuwa zinatolewa
zinawafanya wahisi wanaonewa kila wakati"
Pia Spika alikemea tabia ya baadhi ya wabunge wa CCM kutumia muda mwingi bungeni kurusha vijembe kwa wabunge wa upinzani
"Kwa
wabunge wa chama tawala siyo jambo zuri kurusha vijembe, tukienda
bungeni nitakaa nao, na nitawaeleza kuwa siyo jambo jema kuwa na bunge
la vijembe, nawaasa tubadilike, tuheshimiane ... matusi kelele vijembe
kanuni haziruhusu na haipendezi"
Kuhusu mwenendo wa baadhi ya wabunge kutoheshimu kanuni, Ndugai alisema "Kanuni
zimetungwa kwa watu wazima, lakini tatizo wabunge wanaokuja sasa hivi
wengi ni vijana, na wako chini ya kiwango cha kanuni. Bado sijajua nini
cha kufanya ili hali hii isiendelee, kwenye bunge la katiba angalau
kulikuwa na kitu kinaitwa kamati ya maridhiano, nafikiri inabidi tuige
kitu hicho tupate watu hata wastaafu watakaokuwa wanakaa kuyaweka mambo
haya sawa"
Kuhusu
sakata la Lugumi, Ndugai alisema kuwa kamati ndogo iliyoundwa
kufuatilia suala hilo itatoa taarifa yake katika mkutano ujao wa bunge.
Kuhusu
uamuzi wa serikali kuzuia Bunge LIVE, Ndugai alisema uamuzi huo ni
mzuri na anauunga mkono kwa kuwa unasaidia kupunguza vurugu kwa wabunge.
Kuhusu
suala la posho za wabunge Naibu Spika alisema kuwa posho za wabunge
wanazolipwa sasa, ni za kawaida na siyo kubwa kama watu wanavyodhani
huku akiunga mkono uamuzi wa wabunge kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo.
0 comments:
Post a Comment