Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaalika
wafanyabiashara wa Cuba na Serikali ya nchi hiyo kuja hapa nchini
kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na kujenga viwanda vya kutengeneza
dawa za binadamu.
Rais Magufuli ametoa mwaliko huo leo tarehe 30
Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Jorge Lopez Tormo.Dkt.
Magufuli amemhakikishia Balozi Jorge Lopez Tormo kuwa Serikali yake
itatoa ushirikiano wa kutosha endapo mfanyabiashara yeyote wa Cuba au
Serikali yenyewe ya Cuba itajitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa
sukari na utengenezaji wa dawa za binadamu, na kwamba licha ya Tanzania
kuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa hizo kuna nchi nyingi jirani na
Tanzania zitanufaika.
"Mhe. Balozi ukiniletea huyo mwekezaji hata
kesho nitamkabidhi shamba la kuzalisha miwa na kujenga kiwanda cha
kuzalisha sukari mara moja ili uzalishaji uanze, tunataka kumaliza
tatizo la sukari, uzalishaji wa sasa wa sukari hautoshelezi mahitaji
yote ya Tanzania na pia majirani zetu wana upungufu wa sukari" Amesema
Rais Magufuli na kuongeza kuwa yapo maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo
cha miwa likiwemo eneo la Bagamoyo ambako kuna hekta takribani 10,000.
Hali
kadhalika Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kutoa ardhi kwa
mwekezaji yeyote kutoka Cuba atakayekuwa tayari kujenga kiwanda cha
kutengeneza dawa za binadamu na vifaa tiba hapa nchini.
Kwa
upande wake Balozi Jorge Lopez Tormo amempongeza Rais Magufuli kwa
juhudi kubwa anazozifanya katika uendeshaji wa Serikali na
amemhakikishia kuwa Cuba itaendeleza na kuimarisha uhusiano na
ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Tanzania, na
ameahidi kufanyia kazi yote waliyoyazungumza.
Wakati huo huo,
Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa India hapa
Nchini Mhe. Sandeep Arya ambapo Balozi huyo ametoa taarifa ya hatua
zinazoendelea kuchukuliwa baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa India Mhe.
Narendra Modi iliyofanyika Mwezi Julai mwaka huu.
Katika
mazungumzo hayo Balozi Sandeep Arya amesema wawekezaji kutoka India
wanaendelea na majadiliano na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) juu
ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza gesi majumbani kwa ajili ya
matumizi ya wananchi na pia wanajadiliana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi juu ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya jamii ya kunde ili kulisha
soko kubwa la mazao hayo nchini India.
Kuhusu ujenzi wa kiwanda
cha magari cha Tata, Balozi Sandeep Arya amesema mchakato unaendelea na
kwamba tayari wameoneshwa eneo la kujenga kiwanda hicho lililopo Kibaha
Mkoani Pwani na matarajio ni kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utakamilika
mwaka ujao.
Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa
na uwepo wa miradi hiyo itakayoleta manufaa kwa pande zote mbili yaani
Tanzania na India na ametoa wito kwa pande zote kuharakisha majadiliano
ili utekelezaji wa miradi hiyo uanze haraka.
Aidha, Rais Magufuli
amewakaribisha wawekezaji wa India kuja kujenga hospitali kubwa za
matibabu ya binaadamu na kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za
binadamu huku akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za
matibabu kwa watanzania na wananchi wa nchi nyingine jirani na Tanzania
wanaolazimika kusafiri hadi nchini India kufuata matibabu.
"Wambie
wafanyabiashara wa India walio tayari kujenga hospitali kubwa, waje na
mimi nitawapa ardhi ya kujenga hospitali, wasipoteze muda waje sasa"
Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
30 Agosti, 2016
Tuesday, August 30, 2016
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
📌 Asema Rais, Dkt. Samia anafanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Watanzaia 📌 Atak...
-
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Kata ya Ndungu katika Jimbo la Same Mashariki baada ya kukagua maboresho ya Kituo cha...
-
Mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha zimeleta athari maeneo mbalimbali...
-
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson akizungumza katika Uzinduzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili d...
-
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI, Dkt. Respicious Boniface akizungumza na Waandishi wa Habari (ha...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment