Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 18 Agosti, 2016 amekutana
na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Balozi Liberat Mfumukeko Ikulu Jijini Dar
es Salaam na kumsihi ahakikishe Jumuiya inajielekeza kukabiliana na
matatizo ya wananchi na kupunguza matumizi ya fedha yasiyo ya lazima.
Dkt. Magufuli amesema ni vema Jumuiya hiyo itilie mkazo katika kuziwezesha nchi wanachama kukabiliana na matatizo muhimu ya wananchi yakiwemo upatikanaji wa maji, uboreshaji wa miundombinu kama vile barabara na reli, kuimarisha huduma za afya, kujenga viwanda vitakavyozalishaji ajira na kuongeza mapato, na kukuza biashara na uwekezaji.
"Itakuwa
ni manufaa zaidi endapo nyie watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
mtafanya juhudi kubwa kuhakikisha nchi wanachama zinajikita kukabiliana
na matatizo ya wananchi, mkifanya hivyo na mkaepuka matumizi makubwa ya
fedha kwenye mambo yasiyo ya lazima tutanufaika zaidi" Amesema Rais
Magufuli.
Aidha,
Mhe. Dkt. Magufuli amempongeza Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki, aliyeshika wadhifa huo kuanzia Mwezi Aprili mwaka huu (2016)
kwa mipango na mikakati mizuri aliyoanza nayo katika kutekeleza malengo
ya Jumuiya ikiwemo kupunguza matumizi, kuvutia wawekezaji na kusimamia
kwa ukaribu utekelezaji wa miradi na programu iliyo chini ya Jumuiya
hiyo.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Liberat
Mfumukeko pamoja kumshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa
anaoutoa kwake ameahidi kutekeleza wajibu wake vizuri na kwa manufaa ya
wana Afrika Mashariki.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli ameagana na aliyekuwa Mwakilishi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya idadi ya watu hapa
nchini (UNFPA - Tanzania) Dkt. Natalia Kanen ambaye hivi karibuni
ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la UNFPA.
Dkt.
Magufuli amempongeza Dkt. Natalia Kanen kwa kuteuliwa kushika wadhifa
huo na amesema anaamini kuwa Dkt. Natalia Kanen atakuwa Balozi mzuri wa
Tanzania hususani katika kuongeza mkazo kwa Umoja wa Mataifa kuisadia
Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo ongezeko la
wakimbizi, umasikini na huduma za mama na mtoto.
Kwa
upande wake Dkt. Natalia Kanen ambaye amekuwa hapa nchini kwa kipindi
cha takribani miaka miwili ameishukuru na kuipongeza Tanzania kwa kuwa
nchi ya amani na jinsi ilivyojitoa kuwahudumia wakimbizi kutoka mataifa
mbalimbali yanayokumbwa na matatizo ikiwemo mapigano.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
18 Agosti, 2016
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo wakati akizungumza na Katibu
Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi wa Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya Watu UNEPA, Dkt. Natalia
Kanem na ujumbe wake
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akitazama vitabu alivyopewa na mgeni wake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake
Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Naibu Mkurugenzi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya Watu UNEPA, Dkt. Natalia
Kanem mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es
Salaam.wengine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli akimkaribisha Katibu Mkuu wa jumuiya ya Afrika
Mashariki Balozi Liberat Mfumukeko Ikulu jijini Dar es salaam Agosti
18,2016.PICHA NA IKULU
0 comments:
Post a Comment