METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 29, 2016

Profesa Lipumba, Sakaya wasimamishwa CUF


BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi CUF, limewasimamisha uanachama wanachama 11 akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa, Profesa Ibrahimu Lipumba na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, Magdalena Sakaya.

Wanasiasa hao wamesimamishwa uanachama hadi watakapojieleza katika Baraza Kuu. Wanachama wawili Rukia Kassim Ahmed na Athumani Henku wamepewa karipio kali. Uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF umetolewa jana Jumapili wakati wa mkutano mkuu wa dharula.

Baraza hilo limemfuta uanachama aliyekuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee wa CUF (JUWACUF), Shashu Lugeye.

“Baraza Kuu limechukua hatua mbili kubwa ambazo ni kutoa karipio kali, kusimamisha na kufukuza uanachama wahusika wote walioshiriki kuchochea vurugu zilizotokea wakati wa mkutano wa dharura Agosti 21, mwaka huu,”amesema Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui.

Mazrui imewataja wanachama 11 waliosimamishwa uanachama hadi watakapojieleza katika kamati ya uongozi ni Prof Ibrahim Haruna Lipumba, Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya, Ashura Mustafa, Omar Mhina Masoud, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Maftaha Nachumu, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Inadaiwa kuwa walishiriki katika vurugu zilizosababisha kuvunjika Mkutano Mkuu wa dharura wa chama hicho Agosti 21 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

“Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika kwamba watu hao waliokuwa vinara wa vurugu na njama hizo ovu walipewa nafasi mara kadhaa kujirekebisha dhidi ya mwenendo wao huo dhidi ya chama lakini waliendelea na vurugu na hujuma zao hizo. Kwa hatua iliyofikia, Baraza Kuu limeona halina njia nyengine ya kukinusuru chama isipokuwa kuchukua hatua kali na madhubuti kukilinda chama ambao ni wajibu wake kikatiba,”amesema Mazrui.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com