Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Dkt. Akwilina
Kayumba akiongea na Waandishi wa Habari ( hawapo pichani)
kuhusu utaendesha wa zoezi maalum la upimaji afya za waliokuwa
wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu ambao waliachishwa kazi na mgodi huo
mnamo mwaka 2007 bila kupimwa afya zao kinyume na Sheria ya Usalama na
Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
Baada ya ukikwaji huo wa sheria kuripotiwa kwa Wakala, hatua stahiki zilichukuliwa ikiwemo kufanya kaguzi maalum za usalama na afya katika eneo la mgodi na kutoa onyo kali kwa mwajiri wa walalamikaji pamoja na kugharimia upimaji afya za waathirika wote.
Katika kushughulikia tatizo hilo, vikao vya mashauriano vilivyojumuisha serikali, mwajiri (Mgodi wa Bulyanhulu) na waathirika kupitia chama chao, TAMICO, vilifanyika na utaratibu wa kushughulikia suala hilo ukawekwa. Katika utaratibu huo, TAMICO ilipewa jukumu la kuwatafuta waathirika wote popote walipo na kuwasilisha majina yao kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Wakala ulikuwa na jukumu la kuyapeleka majina hayo kwa mwajiri kwaajili ya uhakiki na kuratibu upimaji afya wa waathirika hao baada ya majina yao kuhakikiwa.
Hadi
kufikia sasa tayari waathirika 315 kati ya 371 ambao mwajiri
alithibitisha kwamba walikuwa wafanyakazi wake wameshapimwa afya zao.
Waathirika 56 waliobaki hawakujitokeza wakati wa upimaji afya licha ya
kupewa taarifa juu ya zoezi hilo.
Waathirika watakaopimwa kwasasa ni wale ambao vipimo vyao vya awali vilionesha kwamba wanahitaji vipimo zaidi kutoka kwa madaktari bingwa.
Maandalizi
ya upimaji huu yamekamilika na zoezi hili litafanyika katika hospitali
ya Taifa ya Muhimbili siku ya Jumamosi tarehe 20/08/2016 na katika
hospitali ya rufaa ya Bugando mnamo tarehe 22/08-15/09/2016. Katika
zoezi hili waathirika ambao orodha ya majina yao imeambatanishwa katika
taarifa hii wataonana na madaktari bingwa wa magonjwa ambayo wana dalili
nayo ili kubaini kama wana matatizo kiafya na hatimaye kuweza kutazama
kama matatizo waliyo nayo yametokana na kazi walizokuwa wakifanya
mgodini.
Kwa
waathirika ambao madaktari watathibitisha kwamba matatizo yao ya kiafya
yamesababishwa na kazi walizokuwa wanafanya, Wakala utashauri namna
ambavyo wanapaswa kufidiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Waathirika
ambao watakutwa na matatizo ya kiafya ambayo hayatokani na kazi,
watashauriwa kuendelea na matibabu katika hospitali zilizopo karibu
nao.
Aidha kwa waathirika ambao hawatakutwa na matatizo yoyote ya kiafya watapatiwa vyeti vyao (certificate of fitness) ambavyo hutolewa kwa wafanyakazi wanaopimwa afya zao baada ya kukoma kwa ajira zao kwa mujibu wa kifungu Na.24 (2) cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.
Ikumbukwe
kwamba, upimaji huu ni mwendelezo wa hatua mbali mbali zinazochukuliwa
na serikali katika kushughulikia tatizo hili ambalo lilitokea mwaka 2007
ambapo waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu waliachishwa kazi
na mwajiri wao baada ya kugoma kufanya kazi. Hata hivyo mwajiri wao
(Mgodi wa Bulyanhulu) haukuweza kuwapima afya zao kama Sheria ya Usalama
na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 inavyomtaka.
0 comments:
Post a Comment