Mhe Mavunde (Mb) akisikiliza kwa makini namna ya kulima mahindi kwa mbinu bora na za kisasa ili kuwa na mavuno yenye tija Mhe Mavunde alipotembelea banda la ushonaji la Jeshi la kujenga Taifa JKT katika Maonesho ya Nane nane kabla ya kuyafunga rasmi
Mhe Mavunde alipotembelea banda la maonesho ya wanyama aina ya mbuzi, Ng’ombe na Kondoo la kampuni ya Ranchi za taifa (NARCO LTD) Naibu waziri ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akipokea zawadi ya mboga za majani kutoka kwa vijana wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) mara baada ya kutembelea banda hilo
Mhe
Mavunde alipotembelea banda la Maonesho ya kilimo cha Vitunguu
Naibu waziri ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akisikiliza maelekezo katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kuhusu umuhimu wa matumizi ya dawa katika kilimo cha kisasa
Mhe Mavunde akitazama ubora wa matrekta yaliyofikishwa
katika Maonesho ya wakulima ya Nanen nane
Naibu waziri ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana na
Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi
mbalimbali walioshiriki katika maonesho ya Nane nane katika uwanja wa Nzuguni
Kanda ya kati Dodoma
Na Mathias Canal, Dodoma
Maonesho na Mashindano ya mifugo
Kitaifa sanjari na Maonesho ya Kilimo yametoa changamoto ya kuleta mapinduzi
katika Ufugaji, Uvuvi, na Kilimo na kutoa ajira hususani kwa vijana kuwaongezea
zaidi kipato na kuondoa umasikini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi
ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana na Ajira Mhe
Antony P. Mavunde wakati akifunga maonesho ya wakulima Nane nane Kanda ya
Kati Dodoma yaliyokuwa yanafanyika katika uwanja wa Nzuguni kwa kauli mbiu ya
"Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni nguzo ya Maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu
(Hapa Kazi Tu).
Amesema kwa kuwa serikali ya awamu
ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais John Pombe Magufuli inatekeleza azma ya
kuhamishia makao makuu mjini Dodoma ameishauri Wizara ya Kilimo, Mifugo, na
Uvuvi na ile ya Biashara na masoko kuangalia uwezekano wa kuanzisha rasmi
maonesho ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi ya Kimataifa (International Agriculture
Trade Fair) katika uwanja wa Nzuguni ambao ndio uwanja wenye eneo kubwa kwa
maonesho ya Kilimo hapa nchini.
Aidha ametoa wito kwa Wizara,
taasisi/Makampuni ya umma na binafsi, Mabenki na wadau wote wa kilimo na mifugo
kuendelea kuwasaidia wakulima na wafugaji hapa nchini ili kuongeza uzalishaji
kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vinavyokusudiwa
kuanzishwa.
"Naomba niwaambie wakulima na
wafugaji wetu kuwa maonesho ninayoyafunga hii leo ni muafaka na fursa nzuri
kwao hususani vijana kwenda kuanza mara moja kutumia mlichojifunza na kuleta
mapinduzi yenye maendeleo chanya yanayotarajiwa kiuchumi, hivyo napenda
kuchukua nafasi hii kuzikumbusha Halmashauri za serikali za mitaa zote
kuwahamasisha wakulima, Wafugaji na wadau wengine kutumia teknolojia
zilizooneshwa hapa kuongeza ufanisi wao katika Kilimo, Mifugo na Uvuvi” Alisema
Mavunde
Naibu waziri huyo pia ametoa zawadi
kwa washindi katika Halmashauri za Mkoa wa Dodoma na Singida, Wizara za
serikali, Taasisi za uzalishaji wa serikali, Makampuni ya pembejeo za Kilimo na
Mifugo, Makampuni ya zana za Kilimo na Mifugo, Taasisi za serikali na Mashirika
ya Umma, Taasisi za fedha na Mabenki, Taaisisi za mafunzo na utafiti, Taaisisi
zisizo za kiserikali (NGOs na CBOs), Taasisi za mawasiliano ya kibiashara,
Mamlaka za udhibiti, Vyombo vya habari, na Kampuni za nishati mbadala kwa
kufanya vizuri katika maonesho hayo.
Pia zawadi hizo zimetolewa pia kwa
watu wenye mashamba makubwa ya ufugaji ng'ombe wa maziwa, Wafugaji wadogo wa
ng'ombe wa nyama, Wafugaji bora, na Wakulima bora.
Sambamba na hao pia Jeshi la Kujenga
Taifa JKT limeibuka kidedea kwa ushindi wa jumla likifuatiwa na Jeshi la
Magereza ambapo nafasi ya tatu imechukuliwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvu.
Akitoa maelezo ya awali kuhusu
maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa Malengo ya maonesho hayo ni
utoaji elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wadau wengi kwa muda
mfupi lakini pia wadau kujionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali,
mashirika ya umma na binafsi.
Mtaturu alisema
kuwa mpaka tarehe 7 hapo jana jumla ya watu waliokuwa wametembelea inakadiriwa
kuwa 40,000 huku matarajio ya siku ya ufungaji ikitarajiwa kuongezeka watu
12,000 na kufikia idadi ya watu 52,000.
Dc Mtaturu
amesema kuwa Teknolojia/Bidhaa zilizooneshwa ni pamoja na zana za Kilimo, Mbegu
bora za mazao mbalimbali, Uzalishaji wa mazao katika mazingira yaliyodhibitiwa
(JKT Kondoa) Taasisi za kitafiti ambazo zimeonyesha teknolojia mbalimbali za
kuongeza tija zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali, Utengenezaji wa
chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, Uboreshaji wa viasilu ili kupata mifugo na
mazao ya kilimo yanayostahimili hali ya hewa ya kanda ya kati na udhibiti wa
magonjwa.
Pia uzalishaji bora wa mazao ya
nafaka, ubunifu wa teknolojia rahisi za kutotoa mayai, Kuongeza thamani mazao
ya mifugo, Makampuni ya mawasiliano, Taasisis za elimu zimeonyesha ubunifu wa
kumsaidia mfugaji, Tiba za asili, Wasindikaji wakubwa na wadogo wa mazao ya
Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Asali, na Nta.
Akitoa salamu za shukrani kwa niaba
ya waandaaji wa Maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo
amemshukuru mgeni rasmi Antony P. Mavunde kwa kuitikia wito wa kufunga maonesho
hayo ambapo pia ameishukuru Benki kuu ya Tanzania (BOT), Halmashauri ya Wilaya
ya Ikungi, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, LAPF, Mkuu wa Mkoa wa Singida na
Chuo kikuu cha Dodoma kwa uwakilishi na uchangiaji kwa ajili ya maonesho hayo.
Maonesho ya sikukuu ya wakulima
Nanenane Kanda ya kati Dodoma yaliyohusisha shughuli za wakulima, wafugaji wa
mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira, wasindikaji wa bidhaa za
mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya umma, makampuni binafsi,
mabenki, Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali
yalifunguliwa tarehe 03 Agosti 2016 na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew
Mtigumwe.
0 comments:
Post a Comment