METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 29, 2016

Mapigano yasitishwa rasmi Colombia

Wananchi wa Colombia wakisheherekea hatua ya utiaji saini wa makubaliano ya kusitisha mapigano
Wananchi wa Colombia wakisheherekea hatua ya utiaji saini wa makubaliano ya kusitisha mapigano
Utekelezaji wa makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Colombia na waasi wa FARC umeanza rasmi na hivyo kuhitimisha mapigano yaliyodumu nchini humo kwa muda wa miaka 52.

Kamanda wa waasi wa the Revolutionary Armed Forces of Colombia, au FARC Rodrigo Londono alitangaza kuwa wapiganaji wake wangeanza utekelezaji wa hatua hiyo ya kusitisha mapigano usiku wa kuamkia leo ( 29,08,2016 ) kufuatia makubaliano ya amani yaliyofikiwa na pande zote mbili katikati ya wiki iliyopita.

Aidha kwa upande wake Rais wa Colombia Juan Manuel Santos alitoa tangazo la aina hiyo akisema jeshi la nchi hiyo litasimamisha mashambulizi yake dhidi ya waasi wa FARC kuanzia jumatatu.

Kiongozi wa waasi wa FARC Rodrigo Londono, anayefahamika pia kama Timochenko alitoa tangazo hilo mjini Havana ambako waasi na wajumbe wa upande wa serikali walijadiliana katika mazungumzo yaliyochukua muda wa miaka minne kabla kufikia makubaliano ya kumaliza moja ya mgogoro mkubwa duniani uliochukua muda mrefu.

" Haitatokea tena ambapo wazazi watakuwa wanawazika watoto wao waliouawa katika vita, uhasama wote kati yetu sasa utabaki kuwa historia " alisema bwanaLondone.

Makubaliano ya mwisho kusainiwa mwezi Septemba

Viongozi hao wanatarajiwa kusaini makubaliano ya mwisho kati ya Septemba 20 na 26 mwaka huu na kuanzia hii leo wapinaji wa kundi la waasi wa FARC wanaokadiriwa kufikia 7,500 wataanza kuelekea katika maeneo maalumu nchini humo kwa ajili ya kusalimisha silaha chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos aliwaambia waandishi wa habari kuwa wale wote kutoka miongoni mwa wapiganaji hao wa msituni watakaokataa kusalimisha silaha watakabiliwa kwa nguvu zote na vikoi vya serikali ya nchi hiyo.

Kura ya maoni kuitishwa mwezi Oktoba

Colombia inatarajiwa kuitisha kura ya maoni nchini kote Oktoba 2, mwaka huu ili kutoa nafasi kwa wapiga kura kuidhinisha makubaliano hayo ambayo sasa yatamaliza machafuko ya kisiasa ambayo yamewaua watu zaidi ya 220,000 na kuwalazimisha zaidi ya milioni 5 kuyahama makazi yao katika kipindi cha zaidi ya miongo mitano. Makamanda wa ngazi ya juu wa waasi wa FARC wanapanga kukutana katikati ya mwezi ujao ili kuidhinisha makubaliano hayo.

Chini ya makubaliano hayo yenye kurasa 297, wapiganaji wa FARC wanatarajiwa kusalimisha silaha ndani ya kipindi cha miezi sita baada ya mkataba huo kusainiwa ambapo pia waasi hao watapewa viti visivyopungua kumi katika mabunge ya nchi hiyo vitano katika baraza la wawakilishi na vitano vingine katika bunge la seneti katika vipindi viwili wakati ambapo viti 16 vya baraza la wawakilishi vitatengwa kwa ajili ya wanaharakati wa ngazi za chini kulingana na mfumo wa utawala nchini humo ambapo vyama vya kisiasa havitaruhusiwa kuweka wagombea.

Kwa mujibu wa mkataba huo baada ya mwaka 2026, uataratibu huo utakoma na hivyo waasi hao wazamani kulazimika katika kipindi hicho kuonyesha nguvu yao ya kisiasa kupitia katika sanduku la kura. 

DW
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com