METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 16, 2016

Waziri Kitwanga Afanya Mazungumzo Na Wakuu Wa Vyombo Vya Ulinzi Na Usalama Zanzibar


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa visiwani Zanzibar kujitokeza kwa wingi Machi 20, 2016 ili waweze kupiga kura kwa amani na utulivu bila kubughudhiwa na mtu yeyote.
 
Kitwanga amesema kuwa ulinzi umeimarishwa na kuwataka wananchi visiwani humo kujitokeza kwa wingi kuja kumchagua kiongozi wanaompenda siku ya uchaguzi huo na watarejea nyumbani kwao salama mara baada ya kumaliza kupiga kura.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na baadaye kuzungumza na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Waziri Kitwanga alisisitiza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaa vizuri na wananchi waondoe shaka kwani hawatakubali vurugu ya aina yoyote itokee.
 
“Jitokezeni kupiga kura siku ya uchaguzi kwani ni haki yenu, nawahakikishia usalama upo na wa hali ya juu, asijitokeze mtu yeyote akawatisha kutokuja kupiga kura, tumejipanga vizuri na lengo letu kubwa kabisa ni kuwalinda wananchi,” alisema Kitwanga.
 
Hata hivyo Waziri Kitwanga alisema hakuna mwananchi yeyote anayehama kwakuogopa vurugu siku ya uchaguzi bali watu wanasafiri kwasababu mbalimbali ikiwemo hiki ni kipindi cha maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka.

“Hali ya Pemba ni shwari na pia nataka kusisitiza nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani sijapata taarifa yoyote rasmi kama kuna watu wanakimbilia nchi jirani. Lakini hata hilo la watu kukimbilia msituni inabidi tujiulize Pemba kuna msitu mkubwa wa watu kwenda kujificha? Haya mambo ni ya kuzusha, watu waende wakajionee wenyewe,” alisema Kitwanga. 
 Alisema hakuna dalili yoyote ya  watu wanaokimbia kutoka Zanzibar kukimbilia Tanzania Bara kutokana na idadi ya wasafiri kati ya Bara na Zanzibar kuwa ya kawaida.
 Alisema kama kuna ongezeko lolote basi ni kutokana na sherehe za Pasaka kukaribia na si suala la kuogopa uchaguzi kama inavyoelezwa. 
Waziri Kitwanga alisema yupo hapa Zanzibar ili kuhakikisha maandalizi yote ya uchaguzi wa marudio Jumapili unafanyika kama ulivyopangwa. 
 “Vitisho vinavyoendelea tulivitegemea, tunajua kama kuna watu hawataki uchaguzi na wanatumia mbinu mbalimbali ikiwamo ya milipuko kutisha watu. Wito wangu kwa watu wanaotaka kupiga kura wajitokeze kwa wingi na usalama wao upo,” alisema waziri huyo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com