METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 11, 2016

PRF MBARAWA AWATAKA TISPA KUONGEZA WATOA HUDUMA ZA MTANDAO

TIS1
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisisitia umuhimu wa Chama cha Watoa Huduma za Mitandao (TISPA)  kuongeza watoa huduma hao ili kupunguza gharama za mitandao lakini kuongeza kasi ya mtandao.
TIS2
Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Mitandao (TISPA) Vinay Choudary akimhakikishia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa namna chama chake kilivyojipanga kuongeza watoa huduma za mtandao wakubwa ili kupunguza gharama za mtandao na kuuwezesha kufanya kazi kwa kasi.
TIS3
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikata utepe ishara ya kufungua moja ya mtambo utakaowezesha kasi ya mtandao hapa nchini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amekitaka Chama cha Watoa Huduma za Mtandao nchini (TISPA), kuhakikisha watanzania wananufaika na fursa za uwepo wa mkongo wa taifa.

Amesema Serikali imejenga kilomita 7,560 za mkongo wa taifa nchi nzima ili kuhakikisha huduma za mtandao zinakuwa kwa haraka na zinapatikana wakati wote ili kuhuisha huduma na uchumi wa wananchi.

Akizungumza mara baada ya kufungua moja ya mitambo ya kuongeza kasi ya mtandao unaosimamiwa na TISPA, Prof. Mbarawa amesema huu ni wakati wa watanzania kunufaika kwa kutumia mtandao wenye haraka na wa bei nafuu.

“Hakikisheni mnaleta watoa huduma za mtandao wengi ili huduma hiyo ipatikane kila mahali, kila wakati na kwa bei nafuu”, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa amesema Serikali imetumia dola za kimarekani Milioni 12.2 kwa ajili ya kuboresha huduma za mtandao na kupeleka huduma kwa wananchi hivyo watu watumie fursa hiyo kujiletea maendeleo.

“Tumieni mtandao kupata elimu na kukuza uchumi, tuachane na matumizi yasiyo na tija yanayotupotezea muda na kutufundisha vitu vinavyoweza kuathiri maadili yetu kwa mtu mmoja na taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Amekemea vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kutumia mtandao kwa masuala yasiyohusika na kazi wakati wa kazi na hivyo kupoteza muda hali inayodhorotesha utendaji wa siku kwa siku.

Prof. Mbarawa ameitaka TISPA katika kipindi cha mwaka mmoja kuhakikisha inaleta kampuni kubwa za mtandao hapa nchini ili kuwa na maudhui ya kimataifa, kuwa na mtandao wenye kasi, na kuwezesha huduma za mtandao kuwa za bei nafuu.

Takribani watu milioni 17 hapa nchini wananufaika na huduma za mtandao, ikiwa ni ongezo la watu milioni 3 katika kipindi cha miaka miwili.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com