Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akizungumza na
wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu mikakati
ya uendeshaji wa Wizara hiyo inayojenga Miundombinu ya kisasa ili
kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Katibu
Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga akifafanua jambo kuhusu
mikakati ya Ujenzi wa Barabara, Nyumba za Serikali na Huduma za Ufundi
na Umeme katika kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano.
Naibu
Katibu Mkuu (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Maria Sasabo akifafanua jambo
katika kikao kazi cha Watumishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Watumishi
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakifuatilia kwa makini
hotuba ya Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
wakati wa Kikao kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.(P.T)
Waziri wa
Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame akiwa na baadhi ya Mbarawa
na wafanyakazi wa Wizara hiyo mara baada ya kikao kazi jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka
wafanyakazi wa wizara yake kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kutumia sekta ya miundombinu kukuza
uchumi wan chi na kufungua fursa za kiuchumi.
Akizungumza katika kikao kazi kilichohusisha Sekta za Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Mbarawa amesema kila mtu afanye kazi kwa umoja, uwazi na uadilifu ili kufikia lengo la kuanzishwa kwa wizara hiyo na kujihakikishia nafasi ya kuendelea kuwa mtumishi wa umma.
“Huu sio wakati wa kufanya kazi kwa mazoea, dunia imebadilika tutumie teknolojia ya habari na mawasiliano kufanya kazi kwa muda mfupi na kwa tija”, amesema Prof. Mbarawa
Amesema kila mfanyakazi atapewa malengo na atapimwa kulingana na malengo aliyopewa ili kuona kama utumishi wake unakidhi mahitaji ya Serikali kuwahudumia watanzania inayojiandaa kuwa nchi ya kipato cha kati.
“Kazi yetu ni moja tu kuwajengea miundombinu ya kisasa itakayowezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi kukutana mara kwa mara kujadiliana masuala muhimu ili kuwa na uelewa wa pamoja katika kazi zinazowakabili.
Amesema Wizara hiyo ina andaa mtandao wa video (Video Conference Facility) utakaotumika kuwaunganisha watumishi wa wizara hiyo nchini kote kujadili na kuyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu hapa nchini.
Aidha Prof. Mbarawa amewataka Makatibu Wakuu wa wizara hiyo Eng. Joseph Nyamhanga (sekta ya ujenzi), Eng. Dkt. Leonard Chamuriho (sekta ya uchukuzi) na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Maria Sasabo (sekta ya mawasiliano), kuimarisha ushirikiano baina ya watumishi wa sekta hizo ili kuiwezesha wizara kufanya kazi kama timu moja.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amewataka wafanyakazi kuwa na maono katika majukumu yao na kujitathimini kila wakati ili kubaini mafanikio na changamoto na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inaundwa na sekta tatu na inasimamia taasisi 29 zenye muelekeo wa ujenzi na usimamizi wa miundombinu na inatarajiwa kuiandaa Tanzania kuwa na miundombinu ya kisasa itakayowezesha kuhimili changamoto za kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.
0 comments:
Post a Comment