Zikiwa zimebakia siku saba kufanyika marudio ya Uchaguzi Mkuu wa
Zanzibar, kumejitokeza viasharia vya uvunjifu wa amani kwa kuharibiwa
majengo ya Serikali na nyumba za watu binafsi.
Usiku wa kuamkia
jana, Kituo cha Afya cha Kiuyu Minungwini, Maskani ya CCM Junguni pamoja
na nyumba za wananchi katika maeneo ya Kangagani, Makangale, Msuka,
Tumbe na Shumba, zimeteketezwa kwa moto na watu wasiofahamika.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti alipotembelea waathirika, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud mohamed alilaani kitendo hicho.
Alisema
kinachoonekana, hujuma hizo zinapangwa na watu wasioitakia mema
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa lengo la kutaka kuwajengea hofu
wananchi, nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa marudio, Machi 20.
Hata
hivyo, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali kupitia vyombo vya ulinzi
na usalama, itachukua hatua za haraka ili kuwabaini wote waliohusika na
hujuma hiyo.
“Hivi ni vitendo vya makusudi, haiwezekani matukio
hayo yote yatokee siku moja katika maeneo tofauti na kwa wakati mmoja,
tutahakikisha wahusika tunawasaka na kuwafikisha mahakamani,” alisema.
Mkuu
wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman ambaye pia ni Mwenyekiti
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, amevitaka vyombo vya ulinzi na
usalama kuongeza doria ili kuhakikisha amani na utulivu unadumishwa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir Ali aliahidi kuwasaka
na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika kwa matukio hayo.
Alitoa rai kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.
“Tusiwaonee
haya hawa watu, wanachangia kurudisha nyuma maendeleo yenu, mkiwaficha
mtakuwa mnajiumiza wenyewe,” alisema kamanda huyo.
0 comments:
Post a Comment