METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 11, 2016

Katibu Mkuu Atakayerithi Mikoba Ya Dr. Slaa Kujulikana Leo


Katibu mkuu mpya wa Chadema atajulikana leo wakati Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe atakapowasilisha jina la mtu anayempendekeza kushika wadhifa huo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalim alisema jana kuwa jina hilo linatarajiwa kuwasilishwa mbele ya kikao cha Baraza Kuu kinachoanza jijini  Mwanza leo.

"Moshi mweupe kuhusu jina la katibu mkuu mpya utaonekana Jumamosi mchana (leo). Mimi na Naibu Katibu Mkuu mwenzangu John Mnyika tuko tayari kumpokea bosi mpya,” alisema Mwalimu.

Katika kikoa chake na waandishi wa habari kilichohudhuriwa na Mnyika, Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema hadi sasa, hakuna yeyote miongoni mwa viongozi na wanachama wa Chadema anayejua kwa hakika nani atarithi mikoba hiyo iliyoachwa na Dk Willibrod Slaa zaidi ya Mbowe.

Alipoulizwa jana, Mbowe hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi ya kuahidi kumteua katibu mkuu atakayemudu kubeba dhamana ya kuivusha Chadema salama katika harakati za kushika dola katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema: “Tunaweza kufikia uamuzi kwa maridhiano bila hata wajumbe kulazimika kupiga kura. Hilo naweza kukuhakikishia kwa sababu mimi ndiye mwenyekiti wa kamati ya maridhiano.”

Pamoja na kupitisha jina la katibu mkuu, vikao vikuu vya Chadema ambavyo kwa mara ya kwanza vimefanyika nje ya Dar es Salaam, pia vinatarajiwa kujadili na kuamua mpango mkakati wa kisiasa wa miaka mitano kuanzia sasa hadi 2021, kupitisha bajeti ya chama kwa kipindi hicho na kufanya marekebisho ya katiba, kanuni na miongozo ya mabaraza.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com