METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, February 25, 2016

Hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa kwenye Mazishi ya Mzee Gaitani Mgongolwa kada wa CCM

Mamia ya wakazi wa mkoa wa Iringa wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera  wakiupokea mwili wa marehemu Mzee Gaitani Mgongolwa mara baada ya kuwasili nyumbani kwake kwa ajili ya kuagwa



Waheshimiwa Mapadri mliopo kwenye ibada hii
Mke wa Marehemu
Watoto wa marehemu
Viongozi wa vyama
Viongozi wa kimila
Viongozi wa serikali
Wazee wote
Wombolezaji wote mliopo;

Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani kwa kupewa nafasi kuzungumza katika msiba huu mzito. Ni changamoto kubwa kwangu kuzungumza mbele ya watu wenye majonzi si jambo jepesi. Naomba mnisamehe pale nitakapo teleza au kumkwaza yoyote.


Ndugu wafiwa na waombolezaji kwa ujumla kifo sio kuzimika kwa mwanga bali ni kuzimika kwa taa tu wakati jua likiwa limetuama na taa inabidi ipumzike. Sote tunajua mwanga bado upo. Sote tunaamaini kuwa Marehemu Gaitani ni mwanga ulitia nuru kwenye familia ya Mwammgongolwa hasa kwa utumishi wake uliotukuka kama hakimu.

Serikali na wana Iringa kwa ujumla tunawapa pole sana kwa msiba huu mzito. Ukizingatia mbali na kuwa hakimu Marehemu aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi za shule mbili na pia MwEnyekiti wa kata CCM.

Ninayo furaha kutamka mbele yenu kuwa nilipata bahati ya kuongea na Mzee Gaitani akiwa amelazwa hospitali ya rufaa Iringa. Tulizungumza mengi ikiwemo kuwaenzi machifu wetu waliopita.
Ndugu waombolezaji

Maisha sio idadi ya miaka unayo ishi bali muda uliotenga kuwasiaida wenzako wenye shida na wale wenye mahitaji. Kila mmoja wetu hapa duniani hufa lakini sio kila mmoja wetu huishi na kubaki mioyoni mwa watu. Umri mkubwa sio tija bali jinsi gani umeweza kuishi na watu.

Ndugu wafiwa tunapo kubali kuwepo kwa usiku na mchana hatuna budi kukubali kuwa kuna kuzaliwa na kufa, hii itusaidie kupokea kwa wepesi na subira habari za kifo. Ingawa msiba hauzoeleki, hatuna budi kupeana moyo.

Naelewa wengi mmeguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine. Naomba mniruhusu nijaribu kufikiri je kama Mzee Mgongolwa anatusikiliza angejibuje maswali haya??

Wako wanalia na kuomboleza wakisema “kwa nini umeondoka sasa??” Mzee Mgongolwa angejibu “ Ulitaka iwe lini??”

Wako wanalia na kusema “umetuacha na nani? Mzee Mgongolwa anajibu “kama mnajisikia upweke njooni huku niliko ambapo njia yake ya kufika ni kama hii iliyo nilaza hapa sandukuni”

Wako wanaolia na kusema “ Mzee tutakosa busara zako nani atatuamulia kesi zetu “ Mzee Mgongolwa anajibu “ kama miaka 84 hamkuchota busara yoyote, miaka 84 hamkunielewa hamuwezi kunielewa kamwe. Mimi sina haja ya kuamua kesi zenu kwani na amini hamtagombana.”

Wako rafiki zake kama wakiona Malangalila , Mungai na wengine wanauliza mbona umetutoka mapema?” Mzee anajibu “mlitaka mpaka tugombane ndio niwatoke??”

Watoto na wajukuu wanalia “baba, babu mbona hukutuaga??” Mzee Gaitani anajibu “anaye taka kuagwa si aje aungane nami huku niliko niweze kumuaga vizuri”

Mama analia “mume wangu mbona umeniacha??” Mzee Mgongolwa anajibu “wala sijakuacha Mpenzi huku niliko nimetangulia kuja kujenga nyumba ili siku yako ifikapo tukae pamoja kwa raha, lakini bado niko nawe mchana hata usiku”

Baba yetu Mzee gaitani Mwammgongolwa sisi sote hapa tulikupenda sana lakini mwenyezi Mungu amekupenda zaidi hatuna budi kuenzi mapenzi ya Mungu na kuendelea kusherekea uhai alikupa ambapo tumepata bahati ya kuwa nawe.

Muhimu tulio hai siku yetu itakapo fika watu waseme maneno mema juu yetu.

Poleni sana familia ndugu na jamaa.
Bwana alitoa na kutupa nafasi ya kushi na wewe kwa miaka hiyo na sasa bwana ametwaa na JINA LAKE LIHIMIDIWE MILELE….PUMZIKA KWA AMANI MZEE GAITANI MGOGONGOLWA.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com