Ridhiwani Kikwete
NA LUQMAN MALOTO
UKIPANDA
daladala huwa hakuna mfumo unaoeleweka, siku nyingine utakutana na
kelele kama sokoni, wale wanaongea yao, hawa wanabishana hivi, hapa napo
kuna ubishi wa soka.
Siku
nyingine ndani ya daladala kama mnasindikiza msiba, kimya kinatawala.
Wakati mwingine kuanzia mwanzo wa kitu mpaka mwisho ni ugomvi tu kati ya
kondakta na abiria. Kimsingi daladala huwa haina utaratibu maalum.
Nikipanda
daladala huwa napenda kukaa siti ya mbele au karibu na dereva ili
nijifunze jinsi ya kuendesha. Si unajua tena, wanasema ukiwa karibu na
mahakama lazima utajua vifungu vya sheria. Matunda ya ujirani hayo.
Nikiwa
namtolea macho dereva jinsi anavyobadili gia kwa mbwembwe, abiria
aliyekuwa amekaa pembeni yangu akanifinya, nilipogeuka akanipa ishara
nitazame mlangoni. Kulikuwa na mrembo anaingia.
Yule
abiria jirani yangu alimfuatilia yule mrembo mpaka alipokwenda kuketi,
kisha akanigeukia na kuniambia: “Kama umeona mambo ya Ridhiwani
Kikwete?”
Nikawa sijamuelewa, nikamuuliza: “Ridhiwani Kikwete amefanya nini hapo?”
Akasema: “Kaka si unaona mwenyewe mwanamke alivyo mzuri, ameumbika. Yule siyo wa kawaida.”
Nikamuuliza tena: “Sasa kuumbika kwa huyo mwanamke kunahusiana nini na Ridhiwani?”
Akanijibu:
“Kumbe wewe ndugu yangu umechelewa mjini, nilivyokuona nilidhani
mchangamfu mwenzangu wa jiji. Kwa taarifa yako misemo yetu sisi watoto
wa mjini ni kwamba vitu vizuri tunaita mambo ya Ridhiwani.
“Magari
yote mazuri mjini ni Ridhiwani, vituo vya mafuta vikubwa vyote
Ridhiwani, maghorofa makubwa ni Ridhiwani, ndiyo maana na wanawake
wazuri wote mjini tunasema ni mambo ya Ridhiwani.”
Aliposema
hivyo, alinikumbusha kitu. Ikabidi niingie kazini kufanya mahojiano,
maana habari za Ridhiwani na utajiri wake ni nzito na zimekuwa
zikizungumzwa kwa kitambo kirefu sasa.
Nikamuuliza yule abiria: “Lakini ndugu yangu wewe si una mke? Ni mzuri au mbaya?”(P.T)
Akajibu:
“Wewe unaniona mimi wa kuja? Siwezi kuoa mwanamke mbaya. Mke wangu
chuma, kisu kikali, mrembo hasa, tena niliwahi kugombana na Hashim
Lundenga alipotaka kumchukua kumuingiza kwenye mashindano ya Miss
Tanzania.”
Hapahapo ndipo nilikuwa napataka, nikamuuliza: “Wewe mkeo akiitwa wa Ridhiwani utafurahi?”
Haraka sana alijibu: “Thubutu, patachimbika siku hiyo.”
Uzuri
alikuwa anajileta mwenyewe, nikampiga swali lingine: “Sasa mbona wewe
unaona sawa kusema wake wa wenzako kuwa ni mali ya Ridhiwani?”
Safari
hii kwa utulivu akasema: “Umeniuliza swali lenye maana kubwa, unajua
mjini watu wanakuza sana maneno. Kuna kipindi nilikuwa nikisikia jina la
Ridhiwani nilikuwa naogopa, siku nilipomuona nikashangaa, kumbe mtu
mwenyewe ana umbo dogo tu, tena wa kawaida.”
Aliposema
hivyo, siti ya nyuma yetu alikuwepo mtu ambaye alikuwa anafuatilia
mazungumzo yetu, akauliza: “Samahani kaka, kama sijakosea nimekusikia
ukisema Ridhiwani ana umbo la kawaida, tena dogodogo, hivi ni kweli?”
Abiria pembeni yangu akajibu: “Wa kawaida ndiyo, kwani ulifikiriaje?”
Abiria
wa siti ya nyuma akasema: “Jamani hii dunia kumbe unaweza kumuogopa mtu
mdogo ambaye unaweza hata kumzaa. Mwenzenu kwa jinsi stori za Ridhiwani
zilivyo na jinsi anavyozungumzwa, mimi nilifikiri ni jitu kubwa la
miraba minne mara 10.
“Tena
niseme ukweli, mimi nilikuwa nafikiri Ridhiwani ni mkubwa kama zimwi,
yale madude ya kutisha ya kwenye hadithi za kale. Nashangaa leo
unaniambia kumbe Ridhiwani wa kawaida tu. Kusema ule ukweli leo
nimestaajabu.”
Abiria
mwingine naye akachangia, sasa mada ilikuwa imeshakua na kupanuka ndani
ya daladala. Huyu alikuwa mzee. alisema: “Nyie vijana, mimi mwenyewe
nilikuwa nasikia sana habari za Ridhiwani kuwa anamiliki mali nyingi, na
nikawa naamini kweli na nikawa natangaza.
“Juzi
hapa nikashangaa kuna nyumba yangu ghorofa moja nilijenga wakati mambo
yangu yakiwa mazuri, nimeshindwa kuimaliza kwa sababu fedha zimekata,
ghafla nakuta watu wanaijadili kuwa ile nyumba yangu ni ya Ridhiwani
ameisahau ndiyo maana hajaimaliza.
“Tena
wale watu walikuwa wanasema Ridhiwani ana nyumba nyingi mpaka nyingine
anazisahau. Niliwaambia ile nyumba ni yangu, hakuna aliyenielewa, tena
waliniambia nimetumwa.”
Sauti
ya kike kutoka nyuma ikasikika: “Kila kitu wanasema cha Ridhiwani,
magari, majumba, makontena, migodi, bado kidogo wataanza kutangaza na
wake zao ni mali ya Ridhiwani. Ikifika kipindi hicho tukumbushane.”
Mwanamke
mwingine akadakia: “Bado kidogo wapi? Mwenzenu usiku leo nimepokea
mkong’oto wa maana kutoka kwa mume wangu, kanipiga kweli. Hatukuwa na
ugomvi wowote, kafika ananiuliza kama namfahamu Ridhiwani, nikamjibu
ndiyo. Hapo ndiyo ikawa chanzo cha ugomvi.
“Akaniuliza
tena namfahamu kivipi, nikamjibu kupitia kumsoma kwenye magazeti na
kumuona katika televisheni. Mume wangu hakuamini, akasema hana imani na
mimi kwa sababu anasikia wanawake wote wazuri ni wa Ridhiwani.
Nikamwambia aache wivu wa kijinga, hapo ndipo nilianza kupokea
mkong’oto. Mwili wote unauma hapa nilipo.”
Gari
lilikuwa limefika Posta, nilipokuwa nashuka nikapata wazo la kuendelea
na usaili wangu. Nikamuuliza mpigadebe mmoja: “Unamfahamu Ridhiwani
Kikwete?”
Akanijibu:
“Namfahamu sana Ridhiwani, yule ni kibosile. Kwanza ni mwili nyumba,
bajeti ya serikali yote inamtegemea yeye. Hapahapa mjini ana majumba
kibao.”
Mpigadebe
akaanza kunionyesha nyumba za Ridhiwani, akasema: “Unaona hii hapa?
Mwenyewe ni Ridhiwani. Ila unajua Ridhiwani huwa hapendi sifa za
kujulikana kama ana utajiri mkubwa, ndiyo maana hii hapa imeandikwa
Benjamin William Mkapa Pension Tower. Huyu Benjamin amewekwa kama
geresha tu. Mwenye mali Ridhiwani.”
Akanizungusha,
akasema: “Unaona hii?” Ni jengo la PPF Tower, akasema: “Huyu PPF Tower
naye amewekwa tu kama geresha, hili ghorofa la Ridhiwani.”
Tukasogea
mbele, tukakutana na jengo la Golden Jubilee Tower, akasema: “Kama
umeona Ridhiwani alivyo mjanja, yaani majengo yake yote ameyapa majina
tofauti. Huyu Golden Jubilee Tower naye kawekwa tu hapa, mwenye mali ni
Ridhiwani.”
Tukiwa
tumesimama nje ya jengo la Golden Jubilee, mpigadebe akanionesha jengo
la Viva Tower, akasema: “Lile pia la Ridhiwani. Viva Tower naye kama
wenzake, amewekwa tu. Nimeshakwambia Ridhiwani hapendi sifa.”
Tukiwa
tunatembea kwa miguu kunionesha mali za Ridhiwani ambazo mpigadebe huyo
anazijua, alisema: “Ila ukitaka kujua kama Ridhiwani ni mjanja, majengo
yake yote jina la mwisho ameita tower ili wasimuibie. Tower ni jina la
mtoto wake.”
Tukajikuta
tumesimama nje ya majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT),
mpigadebe akaniambia: “Kama nimekwambia kuna watu wana fedha hapa
nchini, unaona haya maghorofa mawili mbele yetu yanayofanana? Yote haya
ni ya Ridhiwani.”
Hapo nikaguna, nikamuuliza: “Mbona haya majengo ni ya BOT?”
Naye akaniuliza: “BOT ndiyo nini?”
Nikamjibu: “BOT maana yake ni Benki Kuu.”
Huku
akitabasamu, akasema: “Unaona sasa, bila shaka utakuwa umeamini haya
majengo ni ya Ridhiwani kwa sababu hata hiyo Benki Kuu unayoisema ni ya
Ridhiwani.”
Mpigadebe
akanipeleka kwenye majengo pacha marefu kuliko yote Afrika Mashariki na
Kati, PSPF Commercial Twin Tower, tukaenda Rita Tower, Uhuru Heights,
Umoja wa Vijana Complex na mengine mengi, kote huko alisema: “Mambo ya
Ridhiwani kaka, huyu mtu ni kiboko.”
Kwa
kutumia simu yangu, ‘niligugo’ na kupata picha ya Ridhwani,
nikamuonesha yule mpigadebe kisha nikamuuliza kama anamfahamu, akanijibu
ni sura ngeni, hamtambui kabisa.
Nikamwambia
huyo ndiye Ridhiwani, yule mpigadebe nusura anichape makofi, akasema:
“Toa ujinga wewe, huyo mtoto mdogo anawezaje kuwa Ridhiwani? Ridhiwani
ni jitu lenye mwili wake, kwanza haonekani hovyohovyo.”
Alipoona
nimekaa kimya, akaniambia: “Huyu alikuwa rais wetu, Jakaya Kikwete si
unamjua?” Nikamjibu ndiyo, akasema: “Kwa taarifa yako Ridhiwani ndiye
baba wa Kikwete, ndiye amemfanya Kikwete awe rais, ana hela Ridhiwani
mpaka mpaka yeye mwenyewe zinampa homa.”
Nilipoachana
na yule mpigadebe, moja kwa moja nilikwenda Kariakoo, nikakutana na mtu
amejiinamia, nilipomuuliza kama anamfahamu Ridhiwani, akanijibu
harakaharaka: “Umenitajia hilo jina nahisi kama nakaribia kuuaga
umaskini.”
Nikamuuliza: “Kivipi?”
Jawabu
lake lilikuwa hili: “Natamani kukutana naye anipe kazi, si unajua
anamiliki miradi mingi? Hesabu Daraja la Kigamboni, Mradi wa Mabasi
Yaendayo Kasi, ana mabasi na malori mpaka idadi haitambui, majumba na
viwanja. Jumlisha Uwanja wa Taifa na ule wa Uhuru baada ya kuununua,
sasa hivi yupo anaufanyia marekebisho ili uwe wa kisasa.”
Nilimaliza
usaili wangu nikiwa nimechoka kabisa. Niliporudi nyumbani jioni,
nilimuuliza mtoto wangu, Captain Nyambo: “Captain unamjua Ridhiwani?”
Captain Nyambo alijibu: “Unamzungumzia Ridhiwani mbunge wa Chalinze, mtoto wa Dk. Jakaya Kikwete?”
Sikuona
sababu ya kumjibu swali lake, maana aliniuliza kwa mtindo wa majigambo
kuwa anamfahamu sana, nikamuuliza lingine: “Vipi kuhusu utajiri wa
Ridhiwani?”
Akanijibu
kwa kuniuliza: “Ukitaka stori za Ridhiwani kama changamsha genge,
unaweza ukashangaa hata mimi mtoto wako mpendwa naambiwa ni wa
Ridhiwani, kwa sababu kila kitu kizuri kimekuwa cha Anko Rizi.”
Nikamwangalia
Captain Nyambo, mwenyewe wala hakutetereka, akasema: “Captain Mkuu si
mwenyewe huwa unaona mambo yangu ya shuleni? Wabongo hawashindwi kusema
Captain Nyambo ana akili sana, atakuwa mtoto wa Ridhiwani.”
Alipoona
sifurahishwi na maneno yake, Captain Nyambo aliniambia: “Wewe ndiye
baba yangu, Ridhiwani hana ubavu wa kunipata, Mungu amenifanya wewe
ndiye uwe baba yangu, ndiyo maana nakupenda halafu tunaelewana sana.”
“Captain
Mkuu eeeh,” Captain Nyambo aliniita, nilipoitika alisema: “Tuache hizo
stori za Ridhiwani, hazina tija kwetu. Ila kiukweli baba Tanzania ni ya
ajabu sana, yaani kama kila kinachosemwa ni cha Ridhiwani kingekuwa
kweli, basi huyu mtu angekuwa tajiri kuliko tajiri namba moja
ulimwenguni, Bill Gates.”
By Luqman Maloto
+255 713 355 717
0 comments:
Post a Comment