METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 3, 2015

January: Mchujo ugombea urais CCM uwe wa haki

 
Naibu waziri wa Mawasiliano Syansi na Teknolojia ,January Makamba. 

Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema kuwa ana imani vikao vya kuwachuja wagombea wa urais vitafanya uamuzi kwa msingi wa kujiamini na siyo kwa hofu.
Makamba alisema hayo mjini Dodoma jana baada ya kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
“Kama chama tumepata nafasi ya kupitia michakato mingi migumu kuliko hata huu, tumefanya uamuzi katika mambo mengi na makubwa na bado tumeendelea kubaki kuwa wamoja. Nina imani hata katika hili pia tutavuka salama,” alisema Makamba.
Alisema wananchi wengi hasa vijana wanaangalia CCM itamteua mgombea wa aina gani na wanataka aina mpya ya uongozi ambao unaangalia mbele na unaoakisi matarajio yao.
Makamba alisema wana-CCM, kama walivyo wananchi wote, wanachukizwa na rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na wanachukizwa na chama chao kuhusishwa na masuala hayo.
Alisema CCM wanataka wagombea kwa nafasi za ngazi zote ambao wana mvuto kwa watu na ambao itakuwa rahisi kuwanadi bila kuwatolea maelezo au utetezi kwanza.
Alisema katika kuomba nafasi hiyo ni vyema kutosahau kwamba bado yupo Rais ambaye amefanya kazi nzuri na anaendelea kuifanya iwe nzuri zaidi.
“Tusizungumze kana kwamba hakuna kilichofanyika. Yeyote atakayepata heshima ya kuliongoza Taifa letu ataanzia alipoishia Rais Jakaya Kikwete,” alisisitiza.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema nafasi ya urais ni ya hadhi, heshima na dhamana kubwa hivyo ni muhimu kujitafakari kwa kina kabla ya kuiomba.
Lakini pia ni muhimu kuiomba kwa staha, unyenyekevu na hekima na kwa namna inayoendana na hadhi, heshima na dhamana ya nafasi yenyewe.
“Anayeiomba nafasi hii kwa namna tofauti hastahili. Binafsi nimejitafakari kwa kina. Nimejiandaa na nimeandaliwa vizuri kiuongozi na kimaadili kwenye chama chetu, Serikali, bungeni na kwenye utumishi wangu ndani ya Ikulu,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com