METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, April 24, 2015

HAUSIGELI ADAIWA KUFARIKI, AIBUKIA MAZISHINI







Sophia Omari anayedaiwa kufa na kuibukia mazishini


Ndugu wa karibu wa Sophia Omari akihojiwa.


Wananchi wakifuatilia tukio hilo la kushangaza.

Dustan Shekidele, Morogoro

Maajabu! Dada mmoja msaidizi wa kazi za ndani maarufu kama Hausigeli, aitwaye Sophia Omari (24) ambaye ndugu zake walitangaza kuwa alifariki kwa kunywa sumu, aliibuka nyumbani kwao mtaa wa Tuelewane, Kihonda mjini Morogoro Jumanne wiki hii wakati wanandugu wakijiandaa kwa ajili ya mazishi ya mwili wake, Ijumaa lina mkasa kamili.

Sophia aliyetinga nyumbani hapo akiwa kwenye bodaboda pamoja na babu yake, alisababisha waombolezaji waliojitokeza msibani hapo, kutimua mbio kwa kutokuamini walichokiona mbele yao.Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo la aina yake, awali Sophia alikuwa akiishi kwenye nyumba aliyopangiwa na mwanaume mmoja mume wa mtu aliyezaa naye, lakini baada ya mke wa mume huyo kujua na kwenda kumfanyia vurugu, binti huyo alikimbilia Mazimbu kwa dada yake ambako alikuwa akifanya kazi za ndani kwa majirani.

Babu wa binti huyo ambaye wazazi wake walifariki akiwa na umri mdogo, Juma Sigwa alisema Sophia alilelewa na bibi yake lakini naye alipoaga dunia, alimchukua na kumlea yeye kabla ya kumfukuza nyumbani kufuatia mabadiliko ya tabia yake.

"Jana (Jumatatu) nimepokea meseji kutoka kwa Tausi kwamba Sophia kanywa sumu, kafa tukaangua vilio, baadaye tukafunga turubai huku baadhi ya majirani wakienda kuchimba kaburi, ndugu wa mbali wamefika, leo nikaamua kwenda Mazimbu kuuchukua mwili."Cha ajabu, nafika Mazimbu namkuta Sophia yuko jikoni anapika uji, nikashangaa, baadaye nikawajulisha wenzangu, wakaniambia nimlete msibani, nikakodi bodaboda na kuja naye, watu walipomuona wakatimua mbio kwa woga," alisema mzee huyo.

Inadaiwa kuwa Sophia na dada yake Halima wanaoishi pamoja Mazimbu, wote hawana simu, isipokuwa walikuwa wakiwasiliana na jamaa zao kupitia kwa jirani yao, namba ambayo ndiyo ilituma sms kwa ndugu kuwafahamisha kuhusu kufariki kwa msichana huyo.

Sophia mwenyewe akizungumzia juu ya sakata hilo, alisema ni uchuro unaoendelea katika maisha yake kwani amekuwa ni mtu wa majanga."Tukio hili ni muendelezo wa majanga ninayoendelea kuyapata, wazazi wangu walikufa nikiwa darasa la tatu, ndugu wakashindwa kunisaidia, nikaacha shule darasa la tatu, nikaishi na bibi mzaa mama naye akafa, babu akanichukua na baadaye kanifukuza, nikiwa na umri wa miaka 16 nikatembea na mume wa mtu anaitwa Seif, akanipa mimba, akanipangia chumba nikajifungua mtoto Khadija," alisema binti huyo.

Alisema mwaka jana mtoto wake alivyotimiza miaka miwili, mke wa Seif alijua na kuanza kumtafuta hadi akampata na kumfanyia vurugu kubwa, kabla ya kesho yake mumewe kufika hapo na kumchukua mtoto wake ambaye alimpeleka Dodoma kwa mama yake mzazi ambako hajaonana naye tena wala kuwasiliana maana alibadili namba















Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com