METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 23, 2023

MWANZA: Zaidi ya shilingi Bilioni 1.6 zakamilisha miradi ya elimu Ukerewe

Zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zimekamilisha ujenzi wa miradi ya elimu katika shule za msingi kupitia mpango wa BOOST katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, hatua ambayo itawaondoa adha ya wanafunzi katika mwaka ujao wa masomo unaonza mwezi Januari 2024.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Shelembi amesema miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vyumba 50 vya madarasa, matundu 68 ya vyoo, madawati 660, viti 140, majengo mawili ya utawala na nyumba moja yenye muundo wa kutumika na waalimu wawili (2 in 1).

Shelembi amezitaja shule zilizonufaika na miradi hiyo kuwa ni pamoja na Murutilima, Nakasahenge, Mandela, Nyerere, Kalendelo, Mulezi, Namagubo, Bugorola pamoja na shule mpya za Kivukoni na Kilimabuye.

"Katika sekta ya elimu tumepunguza adha kwa wanafunzi wetu, hasa kutembea umbali mrefu kutoka visiwani jambo ambalo ni hatari ziwani. Pia itaondoa msongamano changamoto ya msongamano wa wanafunzi darasani kutoka wanafunzi 120 hadi 45" amesema Shelembi.

Amebainisha kuwa kati ya shilingi bilioni 1,670,700 zilizopokelewa kupitia BOOST, miradi iliyokusudiwa imekamilika kwa ubora na kufakiwa kubakiza chenchi ya shilingi milioni 60 pamoja na vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 10 zitakazoelekezwa kuboresha miundombinu yenye changamoto.

Pia Shelembi ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha anatatua changamoto mbalimbali za wananchi na kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu na afya.

"Kwa miaka miwili 2021/22 na 2022/23 tumepokea jumla ya shilingi bilioni 20.258 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Ni kazi kubwa inafanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo kazi yetu ni kumsaidia kwa kazi nzuri anayoifanya kwa watanzania" amesema Shelembi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe, Joshua Manumbu katika kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri hiyo imesimamia kwa asilimia 100 bajeti yake na kufanikiwa kukamilisha miradi ya wananchi ikiwemo zahanati, vituo vya afya na madarasa.

"Kipekee kabisa nimpongeze sana DC aliyepita (Denis Mwilla), Mungu ambariki huko Mbarali. Tulifanya kazi pamoja tukishirikiana na Mkurugenzi Shelembi na Kamati ya Siasa ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile. Tumetekeleza miradi yote kwa ubora na hakuna mradi uliokwama baada ya kupitiwa na mwenge" amesema Manumbu na kuongeza;

"Lakini pia nimpongeze Mhe. DC Hassan Bomboko ambaye bado ana muda mfupi Ukerewe, tunaona ufuatiliaji wake wa miradi ni mzuri, tuendelee kushirikiana ili kusimamia fedha za miradi ya maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25" amesema Manumbu.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile amesema Serikali iko kazini na Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25 inatekelezwa. "Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, Mkurugenzi Emmanuel Shelembi amekuwa ni mfano wa watendaji bora katika kusimamia miradi ya maendeleo" amesema Mambile.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Hassan Bomboko amesema miradi ya maendeleo ikiwemo ya elimu imetekelezwa kwa ubora katika Wilaya hiyo na kukamilika kwa asilimia 100 ikiendana na thamani ya fedha iliyotumika.
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Shelembi akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe, Joshua Manumbu akieleza namna Halmashauri hiyo imetekeleza kwa viwango miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ukerewe, Ally Mambile akiwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Ukerewe kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Hassan Bomboko akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo.
Mwonekano wa jengo la utawala katika Shule mpya ya msingi Kilimabuye iliyopo Kata ya Namagondo wilayani Ukerewe.
Mwonekano wa baadhi ya vyumba vya madarasa yaliyojengwa kupitia mradi wa BOOST wilayani Ukerewe.
Mwonekano wa nyumba ya waalimu (2 in 1) katika shule ya msingi Kilimabuye.
Mwonekano wa madarasa ya wanafunzi wa awali katika shule mpya ya Kivukoni iliyopo Kata ya Kakukuru wilayani Ukerewe yaliyojengwa kupitia mradi wa BOOST.
Mwonekano wa baadhi ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa kupitia mradi wa BOOST wilayani Ukerewe.
Mwonekano wa ndani wa vyumba vya madarasa  katika shule ya msingi Nyerere wilayani Ukerewe.
Mratibu miradi ya BOOST Wilaya ya Ukerewe, Rasul Amiri akieleza namna miradi hiyo itaondoa changamoto kwa wanafunzi.
Mwalimu Mkuu shule ya msingi Nakasahenge, Mwl. Jenifer Damian ambaye alikuwa akisimamia ujenzi wa shule mpya ya msingi Kilimabuye iliyogharimu shilingi milioni 448.5.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mandela iliyopo Kata ya Mukituntu, Mwl. Jacob Maranya amesema ujenzi wa vyumba sita vya madarasa pamoja na matundu matatu ya vyoo katika shule hiyo utasaidia kuondoa mrundikano wa wanafunzi katika shule ya Kazilankanda.
Diwani wa Kata ya Namagondo wilayani Ukerewe, Thomas Ng'afu amesema utekelezaji wa miradi ya BOOST imepokelewa vyema na wananchi kwani imewaondolea adha ya kuchangishana fedha kujenga madarasa hivyo wajibu walio nao ni kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule na kuzingatia masomo yao.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com