METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 5, 2023

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAZIDI KUJIZATITI KUTOA ELIMU YA UHIFADHI KWA JAMII


Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na jitihada za kuelimisha jamii ikiwa ni pamoja na kutembelea Ofisi za Vyama katika kila Mkoa na kuelezea juu ya umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa rasilimali za Taifa pamoja na fursa zitokanazo na Sekta ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kukuza uchumi kwa wananchi. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa uliofanyika leo  jijini Mwanza.

"Moja ya maelekezo tuliyoyapata kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa ni wahifadhi kushuka kwenda kila mkoa kuzungumza na chama kuelezea fursa zilizopo katika maeneo yote ya hifadhi tunayoyasimamia na changamoto tunazozipata" Mhe. Masanja amesema.

Amefafanua kuwa lengo la uelimishaji huo ni kuelezea shughuli zinazofanywa na Taasisi za Uhifadhi, kufafanua kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya  pamoja na namna ya kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji katika Utalii.

Amesema endapo elimu ya uhifadhi na fursa za utalii ikielezewa kwa ufasaha vijana wataweza kujiajiri wenyewe na hivyo  kuchangia  uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla. 

Amezitaja mojawapo ya  fursa zilizopo kuwa ni pamoja na upandaji miti na uanzishwaji wa mashamba ya miti ambapo Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania ( TFS)  imekuwa ikigawa miche hiyo  ya miti kwa watu binafsi.

Amesema kupitia shughuli za upandaji miti wananchi wanaweza kujiongezea kipato na pia kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com