![]() |
Uzinduzi wa Mwongozo wa ufaugaji nyuki ukiendelea kwenye kilele cha Siku ya Nyuki Duniani. |
![]() |
Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa akikabidhi tuzo kwa wadau mbalimbali wa nyuki na Misitu. |
![]() |
Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa pamoja na Naibu Waziri Marry Masanja wakionyesha bidhaa zitokanazo na nyuki wakati walipokuwa wakitembelea mabanda kwenye maadhimisho ya nyuki mkoani Singida. |
![]() |
Ugawaji wa Tuzo na zawadi mbalimbali ukiendelea. |
Na Hamis Hussein - Singida
WAZIRI wa
Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amewataka watendaji wa sekta ya Misitu
na Nyuki kukamilisha mkakati wa kuongeza uzalishaji wa asali toka tani 35000 za
sasa hadi tani 138000 katika kipindi cha miezi miwili alioupa jina la mkakati
wa “achia shoka kamata mzinga” huku akitaka eneo la misitu na asali kufanyiwa
utafiti wa kutosha ili litumike kama zao jipya la utalii.
Mchengerwa
ameyasema hayo leo Mei 21, 2023 kwenye Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki
Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida.
Akizungumza kwenye
kilele cha maadhimisho hayo amesema pamoja na uwepo wa maeneo makubwa
yaliyohifadhiwa na yanayofaa kwa ajili ya kuzalisha mazao ya nyuki yenye
viwango bora bado takwimu zinaonesha uzalishaji ni 23% ikilinganishwa na uwezo
uliopo wa kuzalisha tani 138,000 kwa mwaka.
“Tuongeze uzalishaji maeneo haya ya
uhifadhi wa nyuki ili asali tunayotengeneza hapa nchini ipate soko kimataifa,
hii ndio kazi kubwa watalamu tunapaswa kufanya, Wizara iandae mpango ili tutoke
kwenye uzalishaji wa 23% tutoke kwenye uzalishaji wa tani 35000 na tufike
138000 na huu mkakati Naibu Waziri niupate ndani ya Miezi Miwili”, Alisema Waziri Mchengerwa.
Katika
kuhakikisha mkakati huo unakuwa na tija Waziri Mchengerwa ameagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na
Mfuko wa Misitu kuhakikisha wanawezesha wananchi hasa wale wanaopakana na
maeneo ya hifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki wenye Tija pamoja na mizinga ya kisasa ili maeneo ya
uhifadhi yaweze kuwanufaisha wananchi.
Akitolea mfano
amesema Mkoa wa Singida umebarikiwa kuwa
na uoto wa kipekee ujulikanao kwa jina maarufu kama Vichaka vya Itigi (Itigi
Thicket) ambao upatikana katika nchi mbili tu duniani, yaani Tanzania na nchi
ya Zambia ambao katika kipindi cha miaka
ya hivi karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya ukataji na uondoaji wa uoto huu kwa
shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Hali hii
imesababisha sehemu kubwa ya ardhi iliyokuwa na uoto huu kubaki wazi na pia
kumebainika kuwepo kwa mimea vamizi pale ambapo uoto huu ulipoondolewa kutokana
na hali hiyo ameielekeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha
kuwa maeneo yote yaliyobaki ambayo yenye uoto huo yanatambuliwa na kuhifadhiwa
kisheria, pia wananchi waliopo kwenye maeneo hayo wanapewa elimu kuhusu
utunzaji wa mazingira na ufugaji nyuki kibiashara.
Aidha amesema
pamoja na faida nyingi tunazopata kutoka kwa mdudu nyuki bado nyuki anaweza
kutumika kutupatia zao jipya la utalii ambapo amesema katika nchi ya Slovenia
mdudu nyuki hutumika sana kwa ajili ya shughuli za utalii.
“Katika nchi ya Slovenia nyuki anatumika
kwaajili ya utalii kwa kuwavutia watalii wa nchi mbalimbali kutembelea eneo
hilo, hivyo niwaomba TFS Kuandaa baadhi ya maeneo ya Misitu yatumike kama kule
ya Slovenia ili na sisi tuweze kutengeneza zao jipya la utalii, hatupaswi
kushindwa na mataifa mengine tunapaswa kuwa namba moja katika uzalishaji wa
nyuki na asali Duniani”,
Alisisitiza Mchengerwa.
Naye Naibu Waziri
wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akielekeza na kusisitiza kulinda
Maliasili na kuendeleza utalii.
Aidha,
amempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohammed Mchengerwa kwa
kutembea takriban nchi nzima kuhamasisha utunzaji wa maliasili, mazingira na
uendelezaji utalii.
Awali akitoa
taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya Nyuki Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida
ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson alisema kuwa Mkoa huo
umehifadhi Hekta 476,361 za misitu ya asili pamoja na vichaka vya itigi vyenye
ukubwa wa hekta 61,436.28 ambao ni uoto unaotoa asali asilia duniani.
DC Apson amesema
kuwa Mkoa umeongeza wafugaji wa nyuki kutoka 5,675 mwaka 2017/ 2018 hadi wafugaji
12,133 mwaka 2022 ikiwa ni sawa na Asilimia 113.8% ambapo katika kipindi cha
miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2022 Mkoa umeshuhudia ukiingiza kiasi cha
shilingi 890 zilizotokana na uzalishaji wa asali tani 89 na shilingi 140
zitokanazo na tani 20 za nta.
0 comments:
Post a Comment