METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, March 4, 2023

JITIHADA ZA SERIKALI KUSISITIZA USAFI ZALETA MATUNDA KUTOKOMEZA UGONJWA WA KIPINDUPINDU

Na Saida Issa,DODOMA

IMEELEZWA kuwa jitihada za serikali za kusisitiza usafi wa mazingira zimeleta mafanikio makubwa ikiwemo kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ambao  hadi sasa haujaripotiwa kwa miaka saba mfulululizo.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dk.Samweli Gwamaka wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa baraza hilo  katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita.

“Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha usafi wa mazingira  ikiwa ni pamoja na kuhamasisha usafi wa kila jumamosi na  elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo jitihada hizo zimesaidia kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu ambao haujasikika nchini kwa miaka saba mfulululizo ikilinganishwa na miaka  ya nyuma  ikifika kipindi cha mvua lazima wapatikane wagonjwa,”amesema.

Dk. Gwamaka amesema kutokana na elimu inayotolewa  jamii imegundua kuwa ikiwa katika mazingira machafu na magonjwa yanaweza kuiandama.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema NEMC  imepanga kuanzisha klabu za utunzaji wa mazingira kuanzia  ngazi ya shule za msingi na sekondari ili kuwajengea watoto  msingi mzuri wa namna ya kutunza na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao.

Amesema NEMC inaanzisha klabu za mazingira na kuzilea  kwasababu watoto  wakianza kufundishwa wakiwa katika umri mdogo ni rahisi zaidi kuelewa umuhimu wakutunza mazingira na faida zake kijamii,kiuchumi na kiafya.

“Tunaenda  kuelimisha na kukikamata kizazi cha watoto wadogo kuanzisha shule za msingi na sekondari ili wachukulie suala la utunzaji wa mazingira ni jukumu lao la kila siku katika mwenendo mzima wa maisha yao.Tunaamini watakapo kuwa wakubwa tabia itakuwa imejengeka ,"amesema .

Dk.Gwamaka ameeleza kuwa NEMC imeendelea kupokea na kushughulikia malalamiko taklibani 369 ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kutoka kwa wananchi ikiwemo kuvuja kwa mafuta kutoka kwenye bomba,kuchoma taka hatarishi chini ya kiwango,uchafuzi wa vyanzo vya maji,utiririshaji wa maji taka na uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwanda.

Ametaja malalamiko mengine wanayoyapokea kuwa ni kelele za mziki,kushamiri kwa gereji bubu maeneo ya makazi ya watu,kushamiri kwa vituo vya mafuta katikati ya makazi ya watu,matumizi ya mifuko ya plastiki, na kutoa elimu sahihi na suluhisho kuhusu jambo husika.

“Tumeendelea kufanya ukaguzi katika maeneo taklibani 2133 ya uwekezaji na mazingira yakiwemo maeneo ya mafuta na gesi, matanuru ya kuchomea takahatarishi,maeneo ya machimbo ya makaa yam awe,  pamoja na maeneo ya miradi mikubwa lengo ni kujiridhisha na uzingatiaji wa matakwa ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004,

NEMC imepata mafanikio makubwa ndani ya serikali hii ya awamu ya sita ikiwemo kutokomeza mifuko  ya plastiki ambayo ilikuwa ni kikwazo chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hasaan na Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango,"amesema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com