METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 19, 2023

SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA MAGHALA YA KUHIFADHI MAFUTA-MAKAMBA


Na.Godfrey Mwemezi-Dodoma

Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba amesema kuwa serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kupata wawekezaji watakaojenga Ghala kuu la kupokelea mafuta kwa pamoja ili kuwezesha nchi kuwa na uhakika zaidi wa upatikanaji wa mafuta.

Makamba ameyasema hayo tarehe 19 Januari, 2023, wakati Wizara ya Nishati ikitoa taarifa ya mwenendo wa upatikanaji wa mafuta nchini kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Amesema kuwa, uwepo wa ghala hilo utawezesha shehena kubwa za mafuta kupakuliwa kwa haraka na hivyo kupunguza gharama za uagizaji, ucheleweshaji wa meli na kuendelea kuleta unafuu wa bei za bidhaa za mafuta nchini.

“Serikali imeanza kutumia ghala la TIPER kwa ajili ya kupokea mafuta ya dizeli yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza muda wa kupokea mafuta hayo kutoka katika meli. Amesema Makamba

Ameeleza kuwa, Serikali itajenga pia gati kubwa la kupokea mafuta ya petroli na kuboresha gati kubwa la kupokea mafuta ya dizeli.

Gati hizo zitaakisi mahitaji ya sasa na miaka ya baadaye ikiwemo kujenga gati kubwa lenye mabomba ya kupakua mafuta na kuwezesha kupokea meli kubwa zenye uwezo wa kubeba tani 100,000 za petroli, tani 200,000 za dizeli na tani 40,000,000 za gesi ya mitungi (LPG).

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kufuatilia mwenendo wa bei ya mafuta  katika soko la dunia na gharama za uagizaji ili kuweza kuchukua hatua stahiki zitakazopunguza makali ya bei kwa wananchi na katika uchumi wa nchi.  

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe.Dunstan Kitandula ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazochuliwa katika shughuli za upatikanaji wa mafuta nchini pamoja na unafuu wa bei za bidhaa za mafuta katika soko la ndani.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha.Felchesmi Mramba, pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya kuhifadhi mafuta ya TIPER  pamoja na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com