Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Dkt.Mch. Godwin Lekundayo akihubiri katika ibada ya kumshukuru Mungu kwa kulivusha Taifa katika Janga la Corona pamoja na kusaidia Uchaguzi Mkuu kumalizika kwa amani hapa nchini iliyongozwa na Askofu huyo, iliyofanyika Desemba 05, 2020 katika Kanisa la Waadventista Wasabato Bariadi kwa niaba ya Waumini wa kanisa hilo hapa nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka katika ibada ya kumshukuru Mungu kwa kulivusha Taifa katika Janga la Corona pamoja na kusaidia Uchaguzi Mkuu kumalizika kwa amani hapa nchini iliyongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Dkt.Mch. Godwin Lekundayo, iliyofanyika Desemba 05, 2020 katika Kanisa la Waadventista Wasabato Bariadi kwa niaba ya Waumini wa kanisa hilo hapa nchini.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania, Dkt.Mch. Godwin Lekundayo ameongoza viongozi na mamia ya waumini wa kanisa hilo katika ibada maalum ya kumshukuru Mungu kwa kulivusha Taifa katika Janga la Corona na Uchaguzi Mkuu kumalizika kwa amani hapa nchini.
Ibada hiyo imefanyika Desemba 05, 2020 katika Kanisa la Waadventista Wasabato Bariadi mjini, Waumini wa kanisa hilo na wengine kutoka mikoa ya Mwanza na Mara wamewawakilisha waumini wengine hapa nchini, ambapo ibada hiyo imehudhuriwa pia na viongozi wa Chama na Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
“Nilikuwa naangalia takwimu za hali ya janga la Corona ilivyo duniani leo asubuhi (yaani Desemba 05, 2020) hadi sasa zinaonesha watu 66, 281,000 wamepatwa na Corona, waliokufa mpaka sasa 1,525,294; ikiwa ulikuwa umechukulia kiurahisi, hizi takwimu zikuamshe kwamba Mungu ametupendelea sana Tanzania na tunamshukuru sana Mungu kwa niaba ya Watanzania wenzetu,” alisema Dkt. Lekundayo.
“Moja ya vitu ambavyo namshangaa Mungu ni kwa namna alivyotupendelea Watanzania maana na sisi ni wenye dhambi kama ilivyo kwa nchi zinazotuzunguka, sisi ni wenye dhambi kama ilivyo kwa mataifa mengine, lakini Mungu ametupendelea Tanzania na hivyo tunayo sababu ya kumshukuru Mungu maana amekuwa mwema sana kwetu” aliongeza Dkt. Lekundayo.
Awali akitoa mahubiri kabla ya maombi hayo pamoja na kuwasihi waumini kumshukuru Mungu kuwapitisha katika janga la Corona, Askofu Lekundayo pia ametoa wito kwa waumini kuendelea kumshukuru Mungu kwa namna ambavyo amelipitisha Taifa katika Uchaguzi Mkuu ambao umemalizika salama.
Akitoa salamu za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amesema Tanzania kupitishwa katika Janga la Corona haikuwa bahati bali ni neema ya Mungu, hivyo akawashukuru viongozi wa Dini kukubali wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuliombea Taifa kwa juhudi na Mungu akajibu na kulivusha Taifa letu.
Aidha, Kiswaga amesema Serikali inaheshimu mchango wa kanisa na itaendelea kushirikiana nalo katika majukumu yake ya kitume na kimaendeleo, huku akitoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake ili waweze kufanya kazi kwa manufaa na ustawi wa Watanzania.
“Katika neno la Mungu kuna habari ya wale wakoma kumi ambao waliponywa na Bwana Yesu lakini aliyerudi kushukuru ni mmoja tu, ninaamini maombi haya ya shukrani yataendelea kuiponya nchi yetu na majanga ambayo yanaonekana kwa macho na ambayo hayaonekani, ninawaomba viongozi wetu wa dini muendelee kuliombea Taifa, kumuombea Mhe. Rais na wasaidizi wake pia” alisema Kiswaga.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Mhe. Samweli Kiboye amesema baadhi ya watu walimbeza Mhe Rais Magufuli alivyotangaza kumtanguliza Mungu wakati wa janga la Corona kwa kutangaza siku tatu za kuliombea Taifa, lakini anaamini kuwa baada ya kuona matokeo ya maombi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika, wameshuhudia kuwa maamuzi yake yalikuwa sahihi na kuahidi kuwa kanisa litaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais.
0 comments:
Post a Comment