METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, September 14, 2022

ARUSHA YANUFAIKA NA MFUMO WA MAJITAKA

 

Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Arusha

Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi, ambapo kupitia Mradi wa Kuboresha Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha unaogharimu Shilingi bilioni 520 unatajwa kunufaisha wakazi wa jiji hilo kupitia  mfumo wa majitaka.

Akizungumza jana, jijini humo wakati alipotembelea mabwawa ya kutibu majitaka yaliyopo katika eneo la Terrat, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba ameeleza kuwa mradi huo ni muhimu kwa kuwa asilimia 80 ya majisafi yanayotumika yanakuwa majitaka.

“Majitaka yanayozalishwa ni zaidi ya lita milioni 200 kwa siku, hivyo lazima kuwe na sehemu ya kuhifadhi maji, kwa sababu hiyo tumejenga mabwawa makubwa 18 kwa ajili ya kupokea majitaka na mradi huu uligharimu Shilingi bilioni 15 ambapo mabwawa haya yana uwezo wa kutibu majitaka lita milioni 22 kwa siku”. Ameeleza Mkurugenzi Rujomba.

Amefafanuwa kuwa, wateja 4000 wameshaunganishwa na mfumo wa majitaka na amewaomba wakazi wa jiji hilo kujiunga na huduma hiyo.

Aidha, kupitia mradi huo AUWSA inatoa huduma ya majitaka katika miji ambayo bado haijaunganishwa na mfumo kwa kubeba majitaka kwa kutumia magari yake hadi kwenye mabwawa ya kutibu majitaka.

Fauka ya hayo, mradi huo umejenga bwawa eneo la mjini ambalo linatumika kuhifadhi majitaka yanayokuwa yamebebwa na magari binafsi yanayotoa huduma ya kubeba majitaka kutoka katika makazi ya watu ili kupunguza umbali wa kilomita 20 sehemu ambayo mabwawa hayo makubwa yamejengwa.

Awali, jiji hilo lilikuwa na mabwawa ya kuhifadhi majitaka katika maeneo ya Lemara yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni tano kwa siku na kufanya jiji hilo kuzidiwa kwa kutokuwa na miundombinu ya kutosha. Vilevile, majitaka hayo yalikuwa yakimwagwa kwenye mashamba na kuchafua mazingira.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com