METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, August 15, 2022

TUZIPENDE HALMASHAURI ZETU

Adeladius Makwega-Makole-DODOMA

Agosti 11, 2022 niliandika matini niliyoipa kichwa kuwa “Siasa hazina Ukatekista” huku nikipata maoni mengi yenye mantiki na nimeona yanahitaji mno kutolewa majibu katika matini hii.

Katika matini ile kuna jambo nilizungumzia kidogo sana, baadhi ya wasomaji wangu makini waliliona na kuniuliza maswali, pia wakati nikiandika matini hii, gafla nilisoma maoni ya mheshimiwa Erick Shigongo mbunge wa Buchosa, akisema kwamba,

“Mheshimiwa Rais anajitahidi sana kutafuta pesa za maendeleo lakini kwenye Halmashauri kuna mchwa wa fedha za umma. Ushauri Rais aunde taasisi iitwe Tanzania Monitoring&evaluation Instutute, ifuatilie pesa zote na iripoti moja kwa moja. Tutaokoa mabilioni (fedha) ya miradi ya maendeleo.”

Niliposoma maoni haya kwa kina niliona kuna haja ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufahamu kuwa wao ni sehemu ya Halmashauri za wilaya popote walipo wakiwa ni wajumbe halali wa vikao vyote vya baraza la madiwani.

Wabunge popote walipo kwanza wajitahidi mno kuwa sehemu ya watu wanaozisemea vizuri halmashauri za wilaya zao. Kuzilalamikia halmashauri kila kukicha kwa mbunge ni kujilalamikia mwenyewe. Wanapozisemea vibaya halmashauri jambo hilo linaweza kusababisha jamii ya Tanzania kuamini hilo na pengine hilo kumeza fikra za viongozi wa Serikali Kuu na kutokuona umuhimu wa kupeleka pesa za umma katika wilaya zetu.

Kwa ufafiti wangu mdogo sana  dhana ya kuwa halmashauri kuna mchwa kwa sehemu kubwa inazigharamu mno halmashauri zetu za wilaya, kwa mfano tangu mwaka 2015 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuondoka madarakani, mradi mkubwa uliofanywa ulikuwa ni kuhimiza wananchi kujenga maabara tatu kila shule ya sekondari hasa hasa zile za kata, maabara hizo zilijengwa kwa nguvu ya wananchi zikiwa katika hatua mbalimbali, mpaka sasa zinangoja fedha ya maendeleo ya serikali kumalizia.

2021/2022 Tanzania imepata fedha za UVIKO imepelekwa katika halmashauri kujenga madarasa mapya baadhi ya watu wanadhani fedha hiyo ingetumika kumalizia maabara zote zilizoachwa wakati wa Jakaya Kikwete kuliko kujenga madarasa mapya.

Ndiyo kusema kama ilivyo kwa fedha za UVIKO 2021/2022 zilivyotumika katika miradi mipya ndivyo ilivyokuwa tangu mwaka 2016- 2021. 

Ndugu zangu akina Shigongo wanapaswa kuwa makini sana na wafahamu kuwa katika nchi hii pahala penye ufuatiliaji wa karibu kuliko sehemu yoyote ni Halmashauri, kuliko hata wizarani. Mathalani mkurugenzi Mtendaji anawajibika kwa Baraza la Madiwani, anawajibika kwa katibu tawala wa mkoa na anawajibika kwa mkuu wa wilaya(masuala ya ulinzi na usalama). 

Katika kila wilaya kuna taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, kuna Jeshi la Polisi ambavyo vyote hivyo ni vyombo vya uchunguzi ambavyo vinapokea taarifa kupitia vyanzo mbalimbali, Isitoshe TAKUKURU na kama hilo halitoshi kuna Idara ya Usalama wa Taifa zote zipo chini ya Ofisi ya Rais.

Ndiyo kusema kuunda chombo kingine ni kuzitusi taasisi hizo kuwa hazifanyi kazi yake vizuri wakati si kweli na hilo halikubaliki na pia ni kuiongozea mzigo serikali yetu bure.

Kwa sasa ukisema halmashauri kuna mchwa ninapingana nalo, inawezekana pakawepo na uzembe wa mtu binafsi labda kuchelewa kuzipeleka fedha benki lakini katika mfumo wa mapato fedha hizo tayari zinaonekana zimeingia na jambo hilo linatatulika maana yule ambaye atachelewa kufanya hivyo mfumo wa malipo unamtambua kwa jina lake na pahala alipo.

Fedha za miradi ya maendeleo kama miradi ya maji zinalipwa baada ya kazi kufanyika na kujazwa fomu maalumu ya ukaguzi ambayo mkurugenzi mtendaji ushiriki wake ni mdogo sana.

Nionavyo mimi kila mbunge anapaswa kutambua yeye ni diwani na anapaswa kushiriki vikao vyote vya halmashauri yake bila ya kukosa ili awe mjumbe mwema wa halmashauri yake.

Hapa lazima pawepo na msisitizp mkubwa wa wabunge kushiriki vikao vya madiwani bila ya kujali nafasi walizo nazo kama ni uwaziri au cheo kingine. Nitolee mfano wa vikao vya kupitisha fedha za mfuko wa jimbo ukifuatilia baadhi ya wabunge huwa hawashiriki vikao hivyo vizuri, bali huwa wanatoa mapendekezo yao kupitia makatibu wao tu.

Hata leo hii ikifuatiliwa mihutasari ya vikao hivyo takwimu hizo zitatoa majibu hayo. Si kwa vikao hivyo tu bali hata vikao vingine vya Halmashauri ya wilaya kila mara utaambiwa mheshimiwa ana udhuru. Swali la kujiuliza vipi kwa wale wenye majukumu ya kitaifa kama mawaziri na nafasi nyingine? Hapo hali inakuwa mbaya zaidi. Kubwa na la msingi ni kuwaomba kushiriki vikao hivyo na kuwa mawakala wema wa halmashauri za wilaya zao, hao ndiyo ndugu zao, jamni tuzisemee mazuri halmashauri zetu.

Kwa wale wanaozifuatilia nyaraka za TAMISEMI kutoka kila halmashauri watabaini kuwa ndugu hawa wenye majukumu ya kitaifa wengine wameingizwa katika kamati za halmashauri za wilaya. Nilichojifunza mwenyekiti wa halmashauri anapanga hizo kamati na kuwaingiza wabunge wenye majukumu ya kitaifa ili wamsaidie kwa karibu kutoa ushauri na mapendekezo yao kama wanavyotoa ushauri wao katika bunge na baraza la mawaziri..

Kikao cha madiwani kikiwa na hoja yoyote kwa Serikali Kuu kama wana naibu waziri, wana waziri, wana waziri mkuu na hata kama wana naibu spika au spika majibu yatapatikana kwa haraka kwa kuwa ndugu huyu ni mjumbe wa vikao vya juu vya serikali na hata bunge.

Hata kama jambo hilo ni la Sera na Miongozo anaweza hata akatoka nje ya kikao akampigia simu,

 “Haloo mheshimiwa Silinde kuna jambo linatusumbua hapa kikaoni je limekaaje?” 

Mfano Naibu Spika Musa Azn Zungu ndiye aliyempigia simu naibu waziri wa TAMISEMI atapewa majibu kwa haraka kabisa, majibu yakipatikana litaeleeweka kwa urahisi mno katika kikao.

“Yaani mheshimiwa Zungu alimpigia simu mheshimiwa waziri tukapata majibu wakati huo huo.” 

Natambua mheshimiwa Zungu kwa kuwa alikuwa diwani wa kata Mchikichini hapo awali, anatambua umuhimu mkubwa wa mabaraza ya madiwani na vikao vyake na mara nyingi nimemuona akishiriki vizuri sana vikao hivyo na yeye anatambua sana kuzizungumzia vizuri halmashauri zetu

Hapo kutajengeka umoja na udugu baina ya wabunge, madiwani, wakurugenzi watendaji na hata watumishi wengine wa ngazi zote katika halmashauri za wilaya. Maneno kama mchwa, wezi, mafisadi yataondoka tutaijenga nchi yetu.Huku fedha lukuki zitapelekwa katika halmashauri zetu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com