METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 27, 2022

MRADI WA MAJI TAWI FURSA KWA WANANCHI KATA YA MBWARA RUFIJI

Mafundi Ramadhan na Rajabu Salumu wa kijiji cha Tawi kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, wakiwachotea kokoto Habiba Said na Wastara Habibu kwa ajili ya ujenzi wa tenki la maji kijijini kwao.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, Mhandisi Tluway Ninga  akielezea hatua waliofikia katika  ujenzi wa tenki la Maji Kijiji cha Tawi.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, Mhandisi Tluway Ninga akionesha namna ya kupanga vyuma ili kunaza ujenzi wa tenki la Maji Kijiji cha Tawi.
Mtendaji wa Kijiji cha Tawi, Kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani, Abdallah Kilimba akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mradi wa maji kijijini hapo.
Muonekano wa mitaro miwili ambapo mmoja utaleta maji kwenye tenki na mwingine utatoa maji kwenda kwa wananchi, katika Mradi wa Maji Tawi wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Mwananchi wa Kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani,  Wastara Habibu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu faida anazopata kwa kushiriki ujenzi wa mradi wa maji kijijini kwao.
Mwananchi wa Kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Habiba Said akielezea faida anazopata kwa kitendo cha RUWASA kuwapeleka mradi wa maji kijiji. kwao
Mwananchi wa kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Habiba Said na Wastara Habibu wakimwaga kokote za ujenzi wa tenki la maji kijijini kwao.

Mwananchi wa Kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Habiba Said na Wastara Habibu wakiwa wamebeba kokote za ujenzi wa tenki la maji kijijini kwao.

Na Selemani Msuya, Rufiji

UAMUZI wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kupeleka Mradi wa Maji Kijiji cha Tawi Kata ya Mbwara umetajwa kuwa fursa ya kiuchumi, maendeleo na jamii kwa wananchi wa kijiji hicho.

RUWASA wamepeleka maji kijiji cha Tawi ikiwa ni kutimiza kauli mbiu yao ya Maji Bombani na kumtua ndoo mama kichwani, ambayo ni kutekeleza Sera ya Maji inayotaka kila mwananchi achote maji kwa umbali usiozidi mita 400.

Mradi huo umefikishwa kijiji cha Tawi kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, kwa fedha za mkopo usio na riba wa Sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Akizungumzia mradi huo Mwananchi wa kijiji cha Tawi kata ya Mbwara wilayani Rufiji mkoani Pwani, Wastara Habibu amesema kwa sasa ana uhakika wa kipato, hali ambayo inamsaidia kutekeleza mipango yake ya kifamilia.

“Mradi huu kwangu ni fursa za kiuchumi, kwani naweza kujipatia huduma za kijamii kama kununua sabuni, nguo, chakula na mengine,” amesema.

Mwanamama huyo amesema wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji katika mabonde ambayo sio safi na salama, hivyo ujio wa mradi huu utawaondolea adha hiyo.

Naye Habiba Said amesema ameamua kushirikia kazi ya kutekeleza mradi huo kwa kuwa ameweza kujipatia kipato cha uhakika.

Said amesema kitendo cha kupatikana kwa maji kijijini hapo shughuli nyingi za maendeleo zitatekelezwa kwa ufanisi.

“Mimi nimeamua kushiriki mradi huu kwa sababu, unanisaidia kupata fedha ambazo zinasaidia familia yangu. Ila ninamuahidi Rais Samia Suluhu Hassan kuwa hatutamuangusha,” amesema.

Kwa upande wake Ramadhan Salum amesema mradi huo umewapunguzia baadhi ya changamoto za maisha ambazo walikuwa wanapitia.

Salum amewataka vijana wanzake kujitokeza kushiriki shughuli za maendeleo kwa faida ya kijiji na familia zao.

Naye Rajabu Salum alisema mradi huo umewawezesha kuachana na kazi ya kukata mkaa ambayo ilikuwa inaharibu mazingira.

“Miradi ya maji ilikuwa mijini, ila sasa na sisi tumekumbukwa, tunaahidi kufanya kazi na kulinda mradi huu,” amesema.

Mtendajii wa Kijiji cha Tawi, Abdallah Kilimba amesema amefanya kazi kijijini hapo kwa miezi 10 ambapo ameshuhudia wananchi wakiteseka kupata maji.

Kilimba amesema changamoto ya maji kijiji cha Tawi kimesababisha wananchi wengi kuhama katika makazi yao ya asili na kuhamia mabondeni.

“Tumejipanga vizuri kupitia kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha mradi huu unalindwa ili uwe endelevu kwa vizazi vijavyo. Hii kwetu ni neema ya kiuchumi, kijamii na maendeleo,” amesema.

Meneja wa RUWASA, Wilaya ya Rufiji, Mhandisi Tluway Ninga amesema wananchi wa Tawi wamekuwa wakiteseka kutafuta maji safi na salama kwa takribani miaka 38 ila ni imani yao mwishoni mwa mwezi Mei watakunywa maji safi na salama.

Mhandisi Ninga amesema Mradi wa Maji Tawi ulisanifiwa mwaka 2020/2021 ambapo wamepokea Sh.milioni 562 kuutekeleza kwa muda wa miezi sita.

Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 75,000, utasambazaji wa mabomba kilomita 11.52, ujenzi wa ofisi ya kamati ya maji, nyumba ya kuweka pampu na vituo 13 vya kuchotea maji ambapo hadi sasa wapo zaidi ya asilimia 40 ya utekelezaji.

“Sisi hapa mradi huu unaelekea mwisho kwa sababu tumeshakamilisha kazi muhimu kama kusambaza bomba, ujenzi wa vituo, nyumba ya pampu na kamati ya maji. Ujenzi wa tenki utakamilika ndani ya wiki chache zijazo,” amesema.

Mhandisi huyo amesema mradi huo ukikamilika utawezesha kijiji cha tawi kupata maji safi salama kwa asilimia 92, ila kiwilaya watafikia asilimia 89 ikiwa ni sawa na kata 13, vijiji 34 kati 38 na vitongoji 56 kati 78.

Ninga amesema mradi huo utanufaisha 1,270 katika, 1,385 wa vitongoji vyote vilivyopo kijiji cha Tawi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com