METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, March 5, 2022

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA YAFANYA TATHMINI UTEKELEZAJI WA SHERIA ZA KISEKTA


Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume  Bwana Khalist Michael Luanda wakati akiwasilisha mada kuhusu maisha baada ya kustaafu katika ukumbi wa BOT Tawi la Mbeya wakiwa katika baraza la wafanyakazi.

 


Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume  Bwana Khalist Michael Luanda akieleza mikakati mbalimbali walijiwekea ili kufanikisha malengo ya Tume ya kurekebisha sheria katika kikao kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa BOT Mbeya.


Mchumi  kutoka tume ya kurekebisha sheria Tanzania Bi Fatma Saidi Alawi akiwasilisha mada kuhusu mikakati ya miaka mitano inayohusu maendeleo ya Tume.


Wajumbe wa baraza la wafanyakazi wakifuatilia mawasilisho mabalimbali.


Bwana  Wense Evadi dereva kutoka tume ya Kurekebisha sheria akichangia mada

Na Bashiri Salum Mbeya

 

Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania, imefanya tathmini ya utekelezaji wa sheria katika sekta mbalimbali zikiwemo sheria ya adhabu mbadala, sheria ya sekta ya utalii, na Sheria ya mifugo na uvuvi  lengo likiwa ni kubaini changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake na kuzifanyia tathmini kama malengo yaliyokusudiwa wakati wa kutungwa kwa sheria hizo yamefikiwa.

 

Akifafanua leo machi 5 2022 katika kikao cha Baraza la wafanyakazi  kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Tawi la Mbeya  katika wasilisho lililotolewa katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume  hiyo Khalist Michael Luanda alibainisha kuwa tathimini hiyo imefanyika kwa kupitia sheria nyingi zinazotumika katika sekta mbalimbali ambapo Tume inatarajia kukamilisha taarifa nne (4) za tathmini ya utekelezaji wa sheria.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo alieleza mikakati ya Tume hiyo katika kuimarisha mawasiliano kwa kutumia vyombo vya habari  ili kuitangaza taasisi hiyo ambapo kwa sasa wanajipanga kuandaa na kurusha vipindi vya redio na  runinga kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa umma.

Luanda alibainisha kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria imejipanga kutoa elimu kupitia vyombo vya habari  juu ya Ushiriki wa wananchi katika mchakato wa maboresho ya Sheria  hapa nchini .

Sheria nyingine ambazo Tume imetoa elimu ni Sheria ya Mtoto, Sheria za Ajira Tanzania, Sheria za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi na Haki za walaji”.Alisisitiza katibu Mtendaji  Khalist Luanda.

Kwa upande wake Mchumi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Bi Fatma Saidi Alawi alieleza mikakati ya miaka mitano ya  Taasisi hiyo amesema kipindi cha Julai, 2021 hadi Februari, 2022, Tume imechambua hukumu hamsini (50) za Mahakama ya Rufaa ya Tanzania na kuzibainisha Kanuni za Kisheria (Legal principles) mbalimbali zilizotumika katika kufanya uamuzi.

Aidha Bi Fatma ametoa  wito kwa wadau mbalimbali  wanaohitaji kutumia Kanuni hizo kutembelea  tovuti ya Tume kwa ajili ya kurahisisha watumiaji kufuatilia maendeleo ya Sheria mbalimbali kupitia maamuzi ya Mahakama.

Bi. Fatma alifafanua kuwa Katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Februari, 2022, Tume imeshiriki katika kutafsiri sheria 17 zinazosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili. 

Katika nyongeza ya maelezo yake Bi Fatma alisema kwamba Tume  imeandaa Miongozo ya usuluhishi wa migogoro ya ardhi katika Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji.

Baraza la wafanyakazi  limehitimishwa leo  baada ya wajumbe kutumia siku mbili kujadili mambo mbalimbali ya kiutumishi pamoja na mikakati ya kuboresha uendeshaji wa Taasisi hiyo.

 

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com