Mkuu wa Wilaya Singida Mhandisi Pasikas Muragili akipanda
mti pembezoni mwa ziwa Kindai hivi karibuni
Zoezi la upandaji miti likiendelea ziwa Kindai Mkoani Singida
Mkuu wa Wilaya Singida Mhandisi Pasikas Muragili akimwagilia mti
ambao ameupanda pembezoni mwa ziwa Kindai hivi karibuni.
Na Bashiri Salum - Singida
Ukisoma vitabu mbalimbali
vya dini utabaini kwamba kabla ya kuumbwa kwa mwanadamu yaliumbwa mazingira
ikiwepo mimea ambako humo ndipo alipowekwa Adamu kwenye bustani maalum ambapo
aliishi kwa kula matunda.
Kwa kuwa mimi sio msomi
mzuri wa elimu ya dini siku moja nikalazimika kuwasiliana na Mwalimu wa dini ya
kiislamu Shekhe Mteti Huseni wa Usangi Mwanga Kilimanjaro nikitaka kujua
uhusiano wa dini na mazingira na mchango wake katika kulinda mazingira.
Shekhe Mteti akanieleza
kwamba kuna uhusiano mkubwa baina ya dini na mazingira huku akibainisha kwamba Mwenyezi
Mungu amewataka waja wake kupanda miti ya matunda na kivuli na kwamba atakuwa
na malipo makubwa kwa mwenyezimungu kwa yeyote atakaye panda miti na wengine wakayatumia
matunda hayo au kivuli kupumzika.
Upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa ujumla ni sehemu ya ibada kwa mwanadmu hivyo kwa atakayeyaharibu mazingira kwa namna yeyote atakuwa anatenda makosa makubwa ambalo angetakiwa kutubu kwa Mwenyezimungu.
Kwa maelezo hayo ya Shekhe
yanamaanisha kwamba kama mtu atakayeharibu mazingira anatenda dhambi ni dhahiri
kwamba atakaye tunza mazingira kwa namna yeyote ile atakuwa anafanya ibada na atapata
malipo kwa Mwenyezimungu.
Kwa kipindi cha hivi karibuni viongozi wa Mkoa wa Singida walifanya ibada kubwa kwa kudhamiria kubadilisha mazingira na muonekano wa mkoa huu kwa kusimamia zoezi la upandaji miti katika maeneo ya hifadhi, sehemu za kupumzikia, majumbani, kingo za barabara na mashuleni lengo likiwa ni kuondoa hali ya jangwa ambayo ilikuwa ikinyememelea mkoa huo.
Viongozi hao akiwemo Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilithy Mahenge na wakuu wa wilaya za Mkoa huo walitangaza kila jumamosi kuwa siku ya
usafi na upandaji wa miti zoezi ambalo lilizinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Singida
Mhandisi Pasikas Muragili katika maeneo ya ziwa kindai kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa
ambapo kwa siku hiyo pekee miti 2,000 ilipandwa.
Akiwa katika uzinduzi huo Mhandisi Muragili
akawataka wananchi kutumia mbinu mbadala
za kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na athari za
mabadiliko ya Tabianchi ili kupata
Mazingira Safi na kuondoa
uwezekano wa kupata Upungufu wa chakula katika ngazi ya Kaya.
Hii inatokana na ukweli kwamba athari za
ukosefu wa miti hautatenganishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha
upungufu wa mvua na kusababisha changamoto za kuwa na kilimo kisichokidhi
mahitaji ya walaji.
Ni katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya alipotangaza mkakati wa kupanda miti ambapo kila kaya ilitakiwa kuwa na miti isiyopungua mitatu (3) hadi mitano (5) katika maeneo ya miji, na miti kumi (10) hadi kumi na tano (15) kwa maeneo ya mipaka ya mashamba lengo likiwa ni kubadilisha hali ya hewa .
Wakati wa uzinduzi huo DC Mhandisi
Muragili akawaomba wananchi wa Singida kutokubali kutenda dhambi ya uharibifu
wa mazingira na badala yake wafanye ibada hiyo ya kupanda miti na kuhakikisha
wanaitunza.
Katika utekelezaji wa Mkakati
wa upandaji na utunzaji wa miti mkoani singida Kaimu Mkuu wa Idara ya Mazingira Manispaa ya
Singida Bi Shuku Kaishwa anasema wameandaa
Mpango wa kuhamasisha jamii na taasisi
kuanzisha mashamba ya Miche pamoja kueleza jamii faida zitokanazo na mazao ya
miti pamoja na upandaji wa miti aina ya
mihimbo katika vyanzo vya maji.
Jitihada za kuelimisha
wadau mbalimbali wa mazingira zimekuwa zikitajwa kufanyika hasa kwa wafugaji
ambao wamekuwa wakilaumiwa kuwa Ng’ombe wanakula na kuvunja miti lakini pia
baadhi ya wafugaji kukata miti hovyo wakiamini kwamba wanafukuza wadudu
wajulikanao kama mbung’o ambao wanasababisha magonjwa kwa mifugo yao.
Ni kutokana na sababu hiyo
Afisa Mazingira huyo akatoa wito kwa
jamii ya wafugaji na wataalamu wa mifugo kuendelea kuielimisha jamii juu
ya ufugaji wa ndani (zero Grazing) ili kuepuka kusambaza kwa mifugo nje na
kuharibu miti iliyopandwa huku akiwataka wananchi kuhamasika na kuanza kutumia
nishati mbadala ambayo itapunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Ukweli ni kwamba Singida
ina ukubwa wa kilometa za mraba 49.438 ambapo kati ya eneo hilo Km 95.5 ni yale
maeneo yanayozungukwa na maji ya maziwa ya Eyasi,Kitangiri,Singidani na Kindai hii inafanya enoeo la nchi kavu
kubaki Kilomita za mraba 49342.5.
Katika taarifa ya
utekelezaji ya ilani ya Ccm ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015-2020 katika kipindi
cha mwaka 2017/2018 Mkoa wa Singida ulidhamiria kukuza uchumi kwa kupitia
shughuli za upandaji wa miti na hifadhi ya misitu ya asili kwa kupanda miti
10,500,000.
Lengo likiwa ni kuongeza
kiwango cha mavuno ya asali kupitia miti kutoka tani 286 mpaka tani 350 kwa
mwaka pamoja na uongezaji wa mazao yatokanayo na miti ikiwemo mbao, Gundi
matunda na hewa safi.
Ambapo ilikadiriwa
kuongeza hifadhi ya misitu kutoka hekta 308,000 hadi hekta 333,000 ikiwa ni
mpango wa uhifadhi wa rasilimali za misitu na kuongeza mazao ya nyuki .
Kwa kuwa mkoa wa Singida unakadiriwa kuwa na Kaya 255,613 kwa mujibu wa
sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ili kufikia idadi ya miti milioni kumi na
laki tano kila kaya ilitalazimika kupanda miti 41 ili kufikia idadi inayotakiwa.
Kwa mujibu wa kitabu kilichofahamika
kwa jina la Singida region investment
guide ya mwaka 2020 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi inaonesha
kwamba eneo la vijijini linakadiriwa kuwa na kaya 219,827 sawa na 86% na mjini
kuna kaya 35785.2 sawa na 14%.
Kama kila kaya katika maeneo
ya mjini Mkoani hapa watapanda miti mitatu (3) watakuwa na jumla ya miti 880.2
bila kuhusisha miti ya taasisi kama mashule ,pamoja na miti mingine iliyopo
kando ya barabara na kwenye sehemu za
umma.
Kwa upande wa vijiji kama
kila kaya kati ya kaya 219,827 itapanda miti kumi (10) kutakuwa na idadi ya
miti 2,198,270 hivyo kufanya mkoa mzima wa singida kuwa na miti mipya
2,199,150.2 ifikapo 2025
Kwa kiasi hicho cha miti
kinadhihirisha kwamba baada ya miaka mitatu mkoa wa Singida utakuwa umechangia
kwa kiasi kikubwa katika kupunguza hewa ukaa hapa nchini na dunia kwa ujumla na
kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.
Ni kweli kabisa kwamba ipo
mikoa ambayo ishafanya zoezi hili la upandaji wa miti lakini haikuweza
kufanikiwa kwa sababu mbalimbali baadhi ya watu walioulizwa ni kitu gani kifanyike ili mkoa wa singida
uweze kuwa na miti endelevu wakawa na haya ya kusema
Mhandisi Pasikasi Muragili
mkuu wa wilaya ya singida alisema ili zoezi hili liwe la kudumu na liweze
kufanikiwa wananchi wahakikishe kwamba
wanatekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi ili kusaidia kuifikia dhamira ya singida ya
kijani
Aidha Muragili akawashauri
viongozi wa ngazi za vijiji na kata kusimamia
ipasavyo kwa kutoa taarifa sahihi zitakazo saidia kukamilisha mipango hiyo.
Ili kuboresha na kutunza
mazingira ni muhimu kuanzisha vilabu mbalimbali vya mazingira katika mashule
ili kupandikiza mawazo ya kimazingira kwa vijana nakuwashirikisha viongozi wa
dini katika kuhamasisha utunzaji wa
mazingira.
0 comments:
Post a Comment