Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Sh. 500,000/= mwanariadha wa zamani Gidamis Shahanga ikiwa ni ishara ya kutambua heshima kubwa aliyolipatia taifa letu kwa kuwa mshindi pekee wa medali mbili za dhahabu katika mashindano ya Jumuiya ya Madola(Commonwealth Games), mwaka 1978 na 1982 mita 10,000. Mheshimiwa Majaliwa alitoa zawadi hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Mogitu – Katesh wilayani Hanang na kuwasalimia wananchi katika viwanja vya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Katesh, Januari 23, 2022. Kushoto ni Naibu Waziri wa Michezo na Utamaduni, Sanaa na Micheo, Pauline Gekul.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkpatia ufunguo wa pikipiki ya miguu mitatu (guta), Emmanuel John wakati alipokabidhi pikipiki na guta kwa kikundi cha vijana kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri ya wilaya ya Hanang’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Manyara. Tukio hilo lilifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Katesh wilayani humo, Janauri 23, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji katika halmashauri zote nchini waongeze ubujifu na waanzishe miradi inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vinavyohitaji mikopo hiyo ili viweze kupata maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa alitoa kauli hiyo jana (Jumapili, Januari23, 2022) wakati akikabidhi pikipiki na guta kwa kikundi cha vijana kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 kutoka halmashauri ya Hanang’ akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Manyara.
Alisema kuwa kitendo cha kuwakusanya vijana na kuwatafutia jambo la kufanya na lenye tija ni hatua nzuri kwa sababu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza viongozi kuwa na maono ya mbali yanayoangalia Watanzania na mahitaji yao.
Akizungumza kwa niaba ya vijana walionufaika na mkopo huo, Damian Kalist alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba kupitia halmashauri ya wilaya ya Hanang’ ambayo ilitoa shilingi milioni 385 kwa vikundi 87.
“Mkopo huu ni nafuu na umetuwezesha kuondokana na mikopo kandamizi yenye riba kubwa iliyokuwa ikitolewa na baadhi ya taasisi mbalimbali za kifedha. Mikopo hii imetusaidia kutuinua kiuchumi na kutuongezea pato la familia na nchi kwa ujumla.”
Alisema kuwa kupitia mikopo hiyo wameweza kupata ajira binafsi pamoja na kutoa ajira kwa vijana wengine, hivyo kuwafanya vijana kuondokana na utegemezi wa kipato.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa alikagua ujenzi wa vyumba vinne ya madarasa katika Shule ya Sekomdari ya Wasichana ya Nangwa, ambapo aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimamia maelekezo ya ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anakwenda shule.
“Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha na amesambaza katika wilaya zote nchini, hapa Nangwa mmepata shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa haya manne na yana madawati ndani, viwango vya majengo haya ni bora kabisa.”
Alisema kuwa Wilaya ya Hanang’ imenufaika kwa kujengewa madarasa mapya 92 ambayo yatawawezesha watoto wote waliofaulu kwenda kidato cha kwanza kuanza masomo yao kwa pamoja. “Hii ni nia njema ya Rais wetu, anawapenda Watanzania na watoto wa kitanzania.”
Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ afuatilie watoto wote wenye umri wa kwenda shule lakini hawaendi shule. “Lazima kila mtoto wa kitanzania aliyefikia umri wa kwenda shule apate elimu.”
Mheshimiwa Majaliwa aliongeza kuwa nia ya Mheshimiwa Rais Samia ni kuwafikia watanzania, kusikiliza kero na kuwahudumia. “Mheshimiwa Rais amejikita katika maeneo ambayo yanagusa maisha ya Watanzania ikiwemo maji, elimu, barabara, afya na umeme”
Naye, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nangwa, Mwalimu Adelina Manya alimshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwapa fedha za ujenzi wa madarasa hayo manne kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19.
Alisema madara hayo yameondoa changamoto ya upungufu wa miundombinu ya vyumba vya madarasa shuleni hapo. Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1976 na ina tahasusi sita ambazo ni HKL, HGL, HGE, CBG, HGK na PCB zenye jumla ya wanafunzi 596, kati yao kidato cha tano ni 349 na kidato cha sita ni 247.
0 comments:
Post a Comment