METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 8, 2021

SHIRIKA LA WOTE SAWA LAIOMBA SERIKALI KURIDHIA MKATABA WA KIMATAIFA WA WAFANYAKAZI MAJUMBANI

Na Maganga James  Gwensaga – Mwanza

Shirika la Wote sawa linalojishughulisha na utetezi wa haki za wafanyakazi wa majumbani na upingaji wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu hasa watoto la Jijini Mwanza limeiomba Serikali kupitia Bunge kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa wafanyakazi wa Majumbani kwani ndo suluhu ya kudumu ya matatizo yao.

Akizungumza na Wazo huru Blog Disemba 7, 2021  Jijini Mwanza mwanasheria wa shirika hilo Jose Mukoji alisema mkataba huu unalenga na  kuhamasisha kazi za staha kwa wafanyakazi za nyumbani yakiwemo mazingira salama ya mfanyakazi.

“ Sisi kama Tanzania wafanyakazi wa nyumbani ni waajiliwa kama waajiliwa wengine wa sekta zozote zile na ulinzi wake wa kisheria si kwamba haupo upo ila upo kwa ujumla tu kama wafanyakazi wengine wanavyolindwa.”Alisema Bw Mukoji

Alisema kwenye ajira ya nyumbani kuna mazingira yana mambo ya upekee sana hivyo kwenye ulinzi wake unahitaji upekee sana ili kuwalinda Zaidi hasa kulingana na umri wao, hali yao ya kitaaluma, wanatoka wapi lakini vilevile kuna wale wafanyakazi wa nyumbani wahamaji ambao wanafanya kazi kutoka nchi moja kwenda kufanya kazi nchi nyingine.

“ Katika kuwalinda hawa, ule mkataba wa kimataifa wa wafanyakazi wa nyumbani wenyewe unaonyesha namna gani nchi wanachama  wanavyotakiwa kuwatendea hawa wafanyakazi wahamaji, mishahara yao, vilevile namna gani wanaweza kupata mafao yao mfano akihama nchi kwenda nchi nyingine pamoja na masuala ya ulinzi na usalama mahali pa kazi” aliongeza Bw Mukoji

 “ Sisi Lengo letu ni nini, huu mkataba utakaporidhiwa tunategemea yale mambo ya msingi ambayo sisi kwenye sheria zetu hakuna yanaweza kuleta mabadiliko yakabadilishwa ili yaweze kuingia kwenye sheria zetu kwa kufuata vipengele muhimu vya kwenye mkataba wa Kimataifa.” Alisema Bw Mukoji

Aidha alisema kuwa kupitia mkataba huo Serikali inaweza kuona  ni vyema kuwa na sheria ya wafanyakazi wa majumbani peke yao kulingana na umuhimu wao ulivyo kwani sheria za ajira kwa sasa zinalinda watu kwa makundi, kwahiyo sisi tunaona ili mfanyakzi alindwe Zaidi ni vyema akawa na sheria yao inayokidhi mahitaji yao.

 “ Ikiwepo hiyo sheria maana yake ni kwamba ni rahisi hata kuleta  usimamizi  na ulinzi kwa sababu kwenye unyanyasaji wafanyakazi wamekuwa wakinyanyaswa sana na kuridhiwa mkataba huu ni sehemu moja ya kupunguza haya manyanyaso wanayopata hata kama hatukumaliza  tutakuwa tumepunguza.” Aliongeza Bw Mukoji

Aidha aliiomba Serikali kupitia Bunge kuona Serikali inapeleka muswada Bungeni kwa ajili ya kuridhia huo mkataba wa kimataifa wa wafanyakazi wa nyumbani namba 189 wa mwaka 2011 na endapo tutaridhia itatusaidia sana kuweza kuboresha sheria zetu kuwahusu wafanyakazi wa majumbani.

“Kupitia siku hizi 16 za kampeni za kupinga ukatili basi ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa jambo hili ili Tanzania nasi tuwe miongoni mwa nchi zilizoridhia mkataba huu tena ikiwezekana tunapouanza mwaka mpya 2022 suala hili lipewe upekee wake.” Alimaliza kusema Bw Mukoji  

Mkataba wa Kimataifa wa wafanyakazi wa Majumbani namba 189 wa mwaka 2011 uliridhiwa na kupitishwa nchini Geneva-USWIS huku baadhi ya Nchi za Afrika zikitajwa kuridhia ikiwemo nchi ya Afika Kusini.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com