Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda
Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Dar es salaam
Serikali imesema kuwa
kumekuwa na mitazamo tofauti miongoni mwa wadau kuhusu sababu ya kuwepo kwa changamoto
na matatizo sugu ya ushirika na namna ya kushughulikia na kutatua changamoto
hizo.
Wadau wengi wa Ushirika
nchini wamekuwa na mtazamo wa kwamba changamoto na matatizo sugu ya Ushirika
nchini yanatokana na sababu mbalimbali na miongoni mwa sababu hizo ni mapungufu
ya sheria inayosimamia sekta ya ushirika nchini, ambapo sheria hiyo ni ile ya
Vyama vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof.
Adolf Mkenda amesema kuwa sasa serikali imekuja na muarobaini wa kutatua
changamoto hizo.
Ameyasema hayo leo tarehe 17
Septemba 2021 Jijini Dar es salaam wakati akifungua kikao cha wadau wazoefu wa
ushirika kujadili mapendekezo na marekebisho ya sheria ya vyama vya Ushirika Na
6 ya mwaka 2013.
Waziri Mkenda amesema kuwa kufuatia
mtazamo wa wadau na dhamira ya kutatua changamoto sugu za ushirika zinazotokana
na mapungufu ya sheria, Mwaka 2019 serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilielekeza
Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanza mchakato wa kufanya mapitio ya Sheria ya
Vyama Vya Ushirika Na 6 ya mwaka 2013.
Katika mkutano huo Waziri
Mkenda amempongeza Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson
Ndiege kwa kufanikiwa kuwaalika wadau wote wazoefu katika kikao hicho kwa ajili
ya kutoa maoni.
Kadhalika, Waziri Mkenda
ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika pamoja na Wizara ya Kilimo kuhakikisha
kuwa maoni yatakayotolewa na wadau katika kikao hicho yanazingatiwa katika
mchakato wa marekebisho ya sheria ya Vyama vya Ushirika unaoendelea.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment