METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, July 15, 2021

WAZIRI MKUU MAJALIWA AISHUKURU BENKI YA AFRIKA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kitabu cha maelezo kuhusu Benki ya Afrika ambacho alikabidhiwa na Rais wa Benki hiyo, Othman Benjelloun  kwenye hoteli ya Sofitel Jijini Rabat, Morocco,

Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa ameishukuru Benki ya Afrika (BOA) kwa jitihada zake za kuendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta mbalimbali za maendeleo.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano Julai 14, 2021) wakati alipozungumza na Rais wa benki hiyo Othman Benjelloun kwenye hoteli ya Sofitel, Rabat Nchini Morocco.

Amesema kuwa uwepo wa Benki hiyo nchini Tanzania umewawezesha wananchi kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo, “kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tunaishukuru Benki ya Afrika kwa jitihada hizi”.

Aidha, Waziri Mkuu alimshauri Rais Benjelloun kuendelea kupanua wigo wa huduma za benki hiyo nchini ili kuwafikia watanzania wengi zaidi hasa katika sekta  za Elimu, Kilimo, Mifugo na Madini.

Waziri Mkuu aliahidi kuwa ataandaa utaratibu wa kuukutanisha uongozi wa Benki hiyo na sekta binafsi nchini Tanzania ili kuona namna watakavyoweza kushirikiana  katika kuwahudumia Watanzania.

Kwa upande wake, Rais Benjelloun amesema lengo la benki hiyo ni kuendelea kukuza uwekezaji wake  nchini Tanzania. “Sisi tupo tayari kuwekeza katika maeneo mbayo viongozi wa taifa la Tanzania watatushauri lengo likiwa ni kutoa mchango wetu katika kujenga uchumi”. 

Naye, Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa benki hiyo isaidie kukuza mahusiano ya Tanzania na Morocco katika sekta ya kilimo hasa kwenye mazao kama vile  Mchele, Tumbaku, kahawa na mazao mengine.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar Leila Muhamed Mussa amesema yapo maeneo ya fukwe ambayo hayajawekezwa mpaka sasa hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuyatumia na kwamba  Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefungua milango kwa wawekezaji. 

Pia aliiomba benki hiyo kuona namna ya kuwawezesha wakulima wa viungo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com