METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 14, 2021

WAZIRI MABULA ASIKILIZA KERO 120 ZA ARDHI NDANI YA SIKU MBILI MOROGORO

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitatua changamoto za ardhi kwa wananchi waliojitokeza kuwasilisha kero zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Mafiga katika manispaa ya Morogoro jana. 

Sehemu ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro wakiwa wamepanga mstari kwa ajili ya kusikilizwa kero zao za ardhi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Mafiga mkoani Morogoro jana. 

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela akizungumza wakati wa uwasilishaji kero za ardhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kwenye mkutano wa hadhata eneo la stendi ya Mafiga Morogoro jana. 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitatua changamoto za ardhi kwa wananchi waliojitokeza kuwasilisha kero zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika stendi ya Mafiga katika manispaa ya Morogoro jana.

Na Munir Shemweta, Morogoro

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikiliza jumla ya kero 120 za ardhi ndani ya siku mbili na kuzipatia ufumbuzi baadhi ya kero hizo ikiwa ni utekelezaji wa magizo ya rais Samia Suluhu Hassan.

Naibu Waziri Mabula ambaye alianza kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi juzi katika wilaya ya Kilosa na jana alikutana na wananchi wenye kero hizo kwenye mkutano wa hadhara eneo la stendi ya Mafiga manispaa ya Morogoro.

Akiwa ameambatana na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shigela, Katibu Tawala Mariam Mtunguja na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe pamoja na Wataalamu wa sekta ya Ardhi kutoka manispaa ya morogoro, Naibu Waziri Mabula alimpa fursa kila mwananchi mwenye kero ya ardhi aliyefika kuwasilisha kero yake kwa uwazi na kuwataka wahusika kujibu hoja za wananchi kabla ya yeye kutoa maamuzi.

Kero nyingi za ardhi zilizowasilishwa kwa Naibu Waziri wa Ardhi katika Manispaa ya Morogoro wananchi wake walilalamikia kudhulimiwa maeneo, umilikishaji ardhi mara mbili pamoja na udaiji fidia uliotokana na wananchi kuchukuliwa maeneo yao kutokana na shughuli za kimaendeleo.

Akizungumnza wakati wa kuzipatia ufumbuzi kero ambazo baadhi yake ni za miaka ya tisini Naibu Waziri Dkt. Mabula aliwataka wananchi kuwa makini wakati wa kuuziwa maeneo na kuhakikisha wanapotaka kununua ardhi waulizia ofisi za ardhi ili kujua wamiliki pamoja na matumizi ya eneo hilo.

‘’Mnapotaka kununua eneo lazima mkaulizie ofisi za ardhi ili kujua kama eneo hilo limemilikishwa kwa mtu mwingine au matumizi ya eneo hilo ni yapi maana unaweza kuuziwa eneo kumbe ni la wazi’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi alitoa maelekezo kwa waendaji wa sekta ya ardhi kudhibiti ujenzi holela sambamba na kuhakikisha hakuna mtu anayejenga bila kuwa na kibali na ujenzi wowote unaofanyika unazingatia mipango miji ya eneo husika.

‘’Lazima mdhibiti ujenzi holela katika halmashauri na mshirikishe watendaji wa mitaa kwa kuwa zoezi la urasimishaji linaloendelea siyo la kudumu na hatuwezi kufanya urasimishaji huku ujenzi holela unaendelea’ alisema Dkt Mabula.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando alimpongeza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuweza kusikiliza kero 120 za ardhi katika wilaya mbili za Kilosa na Morogoro na kusema hatua hiyo inafanya wilaya yake kuongeaza juhudu za kushughulikia kero za ardhi tofauti na malengo yake ya kusikiliza kero mia tano kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Msando, wilaya ya Morogoro imejiwekea malengo ya kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero mia tano za ardhi katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe alieleza katika mkutano huo kuwa, migogoro mingi ya ardhi kwenye mkoa huo imesababishwa na ununuzi holela wa ardhi unaofanywa na wananchi hasa kupitia watendaji mitaa au wenyeviti wa vijiji.

“Migogoro mingi hapa morogoro imesababishwa na wananchi kununua ardhi kiholela bila kupitia ofisi za ardhi ambazo ndizo zenye kumbukumbu za wamiliki” alisema Frank.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alimaliza ziara yake jana mkoani Morogoro na anaendelea katika mkoa wa Dodoma eneo la Kibaigwa ikiwa ni utekelezaji wa  maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyemtaka kwenda kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi  baada ya kupokea  malalamiko kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com